UEFA kuondoa sheria ya bao la ugenini

UEFA kuondoa sheria ya bao la ugenini

Muktasari:

  • Chama cha Soka Ulaya (UEFA) kinapanga kufanya mabadiliko makubwa katika sheria ya bao la ugenini katika michuano yake kuanzia msimu ujao.

Chama cha Soka Ulaya (UEFA) kinapanga kufanya mabadiliko makubwa katika sheria ya bao la ugenini katika michuano yake kuanzia msimu ujao.


Chini ya sheria hiyo inayopendekezwa na ambayo inategemewa kuidhinishwa Ijumaa, mabao ya ugenini yatakuwa na thamani hadi dakika tisini za mchezo wa marudiano zitakapomalizika.
Na baada ya hapo, bao lolote litakalofungwa katika muda wa ziada halitakuwa na faida ya bao la ugenini.


Hata hivyo, ripoti zinaeleza kuwa mpango wa kufuta kabisa sheria hiyo ya bao la ugenini umekataliwa.
Magazeti ya Uingereza, The Sun na The Daily Mail, yameripoti leo Jumatano kuwa pendekezo la mabadiliko hayo linaungwa mkono na klabu kubwa za barani Ulaya.


Habari zinasema kuwa UEFA iko tayari kubadilisha sheria hiyo ya mabao ya ugenini katika michuano yake ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na Ligi ya Europa kuanzia mwakani.


Gazeti la The Sun, mbali na kudai kuwa pendekezo hilo jipya linaungwa mkono na klabu kubwa, limewataja vipngozi wawili wa klabu za Uingereza-- Ed Woodward (makamu mwenyekiti mtendaji wa Manchester United) na Ferran Soriano (ofisa mtendaji mkuu wa Manchester City)-- kuwa miongoni mwa wanaokubaliana na mabadiliko hayo.


Imeripotiwa kuwa UEFA itaidhinisha mabadilioko hayo kuanza rasmi msimu ujao baada ya sheria hiyo kuchambuliwa katika michuano hiyo miwili ambayo yote iliathiriwa vibaya na janga la virusi vya corona.


Sheria ya bao la ugenini, ambayo ilianzishwa rasmi msimu wa mwaka 1965-66, ilikosolewa kwa kiwango kikubwa baada ya mechi za nyumbani na ugenini kuhamishiwa katika viwanja visivyo na mwenyeji msimu huu kutokana na masharti ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona katika nchi zabarani Ulaya.


Chelsea, Arsenal, Liverpool, Tottenham na City zililazimika kuchezea mechi zao za nyumbani nje ya nchi, kitu kilichoibua malalamiko na hoja kwamba sheria hiyo sasa haina umuhimu.
Katika hatua nyingine, UEFA inaendelea na mpango wake wa kupanua Ligi ya Mabingwa kutoka kushirikisha klabu 125 kw amsimu hadi klabu 225, lakini klabu kadhaa zinaupinga.


Kwa miezi kadhaa, UEFA imekuwa katika mazungumzo na klabu, ligi za nchi na vyama vya soka, lakini haitataka kuruhusu upigwaji wa kura za kuidhinisha mageuzi ya Ligi ya Mabingwa hadi itakapokuwa na uhakika kuwa yatakubaliwa.

Mpango huo pia unahusu kupanua Ligi ya Mabingwa kutoka timu 32 hadi 36 na hivyo kuongeza idadi ya mechi hadi kufikia 100, na kuzipa upendeleo maalum wa kuingia mashindano hayo klabu kubwa kuanzia mwaka 2024.

UEFA inapingwa na Chama cha Soka cha England (FA), Ligi Kuu ya England, pamoja na vyamawanachama, ligi za nchi na klabu zenye ukubwa w kati na ndogo.