Uzoefu, makosa binafsi yametuangusha- Julio

Muktasari:

  • Kocha wa Ngorongoro Heroes, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amedai kuwa kukosa uzoefupamoja na makosa yaliyofanywa na wachezaji wake ndiyo chanzo cha timu hiyo kupoteza kwa mabao 4-0 katika mechi ya kwanza ya makundi ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana(Afcon U20) dhidi ya Ghana.

Dar es Salaam. Kocha wa Ngorongoro Heroes, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amedai kuwa kukosa uzoefupamoja na makosa yaliyofanywa na wachezaji wake ndiyo chanzo cha timu hiyo kupoteza kwa mabao 4-0 katika mechi ya kwanza ya makundi ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana(Afcon U20) dhidi ya Ghana.

Julio alisema timu yake ilikuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo lakini makosa ya wachezaji wake kutotumia vyema nafasi walizopata pamoja na kutokuwa wazoefu kuliwagharimu.

“Timu yetu imejitahidi imecheza vizuri na kama unavyofahamu ni mara ya kwanza kushiriki mashindano haya. Lakini pamoja na yote tumeweza kutawala mchezo lakini nafasi tulizopata hatukuweza kuzitumia vizuri.

Nyingine zimegonga mwamba na nyingine wameokoa lakini pamoja na kuwaheshimu Ghana sio kwamba wametuzidi sana mpira isipokuwa wao wamepata nafasi wametumia, sisi hatukuzitumia nafasi vizuri.

Mwisho wa siku kundi letu lina timu tatu,. Tunaamini mechi nyingine zitakazokuja tutafanya vizuri. Hatukufanya vibaya sana. Vijana wangu wamecheza vizuri na ninawapongeza. Lakini kingine ugeni wa mashindano ndio umechangia kwa sababu wenzetu wana uzoefu mkubwa ndio maana wanatumia nafasi wanazopata . Yote kwa yote nawapongeza Ghana kwa kupata ushindi,” alisema Julio.

Katika mchezo huo wa juzi, mabao manne ya Ghana yalipachikwa na Percious Boah aliyefunga mawili huku mengine yakiwekwa kimiani na Abdul Fatawu pamoja na Joselpho Barnes Ushindi huo umeifanya Ngorongoro Heroes ishike mkia katika Kundi C linaloongozwa na Ghana, ambayo ina pointi tatu sawa na Morocco inayoshika nafasi ya pili.