Wamepotea, Mastaa hawa benchi lao

KUNA wachezaji walianza kwa kasi Ligi Kuu Bara katika vikosi vya kwanza vya Simba, Yanga na Azam FC, lakini kadri inavyoelekea ukingoni wamekuwa wakianzia benchi kutokana na ushindani wa namba.

Mwanaspoti linakuletea kikosi cha wachezaji hao wanaoonekana moto wao kuanza kupoa tofauti na mwanzo wa michuano hiyo.


David Kisu - Azam (kipa)

Wakati Ligi Kuu inaanza msimu huu, kipa wa Azam FC, David Kisu alikuwa hakosekani kikosi cha kwanza, lakini kadri siku zinavyoendelea anawekwa benchi na Mathias Kigonya.


Paul Godfrey - Yanga (2)

Ujio wa Kibwana Shomary kutoka Mtibwa Sugar unaonekana kumuondoa kikosi cha kwanza beki namba mbili wa Yanga, Paul Godfrey, ambaye siku za nyuma alikuwa anapewa nafasi ya kuanza baada ya kuondoka kwa Juma Abdul.


David Bryson - KMC (3)

Haanzi mara kwa mara kikosi cha kwanza cha KMC kama ilivyokuwa mwanzo. Hii ni kutokana na ushindani wa namba katika nafasi yake ambapo KMC kwa ujumla ipo kwenye kiwango bora.


Lamine Moro - Yanga (4)

Nahodha wa Yanga, Lamine Moro alikuwa panga pangua katika kikosi cha makocha walioondoka Zlatko Krmpotic (mechi tano) na Cedric Kaze (mechi 18), lakini chini ya Juma Mwambusi aliyekaimu nafasi hiyo hakuwa anaanza, badala yake walionekana kupangwa Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Dickson Job.


Bakari Mwamnyeto - Yanga (5)

Yanga kumsajili Mwamnyeto kutoka Coastal Union ya Tanga ilivutiwa na kiwango chake. Hata baada ya kujiunga nao aliendelea kuwa mwiba kwa washambuliaji wa timu pinzani, lakini siku za karibuni ni kama makali yake yanapungua.

Ile bato yake na Moro haijaonekana siku za karibuni, badala yake wanachezeshwa Ninja na Job.


Jonas Mkude - Simba (6)

Ongezeko la kiungo mkabaji Taddeo Lwanga ni kama kunaondoa uhakika wa mwenyeji wake, Mkude, kujimilikisha namba kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa mwanzo ambapo alikuwa panga pangua. Mkude sio mchezaji mbovu uwanjani, isipokuwa anapata ushindani wa Lwanga aliyeanza vyema baada ya kupewa nafasi na kocha Didier Gomes, katika michuano ya Simba Super Cup.


Hassan Dilunga - Simba (7)

Kiwango cha Luis Miquissone kinamchomesha mahindi Diluna pale Msimbazi na kukosa nafasi tofauti na awali ambapo alikuwa anaanza, na kuanzia benchi na aliweza kufanya vyema.


Haruna Niyonzima - Yanga (8)

Mara nyingi Niyonzima anaanzia benchi, huku Feisal Salum ‘Fei Toto’ akijihakikishia kucheza kikosi cha kwanza mbele ya mkongwe huyo anayetokea Rwanda. Hata hivyo sio kwamba Niyonzima amefulia, bado ana ufundi wake miguuni.


Michael Sarpong - Yanga (9)

Siku za mwanzo wakati ligi inaanza angalau Sarpong alikuwa anapata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza, lakini kadri muda unavyokwenda amekuwa akikaa benchi na kucheza mara moja moja.


Meddie Kagere - (10)

Misimu miwili iliyopita straika wa kimataifa wa Simba, Kagere alinyakua kiatu cha dhahabu (2018/19 mabao 23 na 2019/20 mabao 22). Pamoja na hilo hajaonekana kuanza moja kwa moja kikosi cha kwanza kutokana na ushindani wa namba mbele ya John Bocco na Chriss Mugalu. Licha ya kwamba haanzi mara kwa mara Kagere ndiye anayeongoza kwa mabao 11 ndani ya Simba, huku Bocco akiwa nayo 10.


Benard Morrison - Simba (11)

Anacheza namba saba na 11. Akiwa Yanga staa huyo alikuwa tegemeo kikosi cha kwanza, jambo lililowavutia Simba kumsajili msimu huu. Hata hivyo ushindani uliopo Msimbazi unamnyima nafasi ya kuanza moja kwa moja kikosi cha kwanza, licha ya kocha Didier Gomes kukiri kuwa anajua, bali anapaswa kuboresha nidhamu.