Wawa, Taddeo kuwakosa Merrikh

WACHEZAJI wawili wa kikosi cha kwanza cha Simba, beki Pascal Wawa na kiungo mkabaji Taddeo Lwanga hawatakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza mechi ya marudiano na Al Merrikh Machi 13 jijini Dar es Salaam.

Wachezaji hao wawili watakosekana kutokana na kupata kadi mbili za njano katika mechi tatu za mzunguko wa kwanza ambazo walicheza.

Shirikisho la soka Afrika (CAF), linaelekeza mchezaji yoyote mwenye kadi mbili za njano mechi inayofuata hataweza kucheza.

Kutokana na sheria hiyo Wawa na Lwanga hawataweza kuwa sehemu ya kikosi ambacho kitacheza na Al Merrikh katika mechi ya marudiano pale Dar es Salaam.

Mratibu wa Simba, Abbas Selemani alisema Wawa na Taddeo wote walipata kadi za njano katika mechi na Merrikh lakini huku awali walikuwa na kadi moja moja za njano.

"Wawa na Taddeo hawatakuwa sehemu ya kikosi katika mechi ya marudiano kutokana na changamoto hiyo ambayo wamekutana nayo," alisema Selemani.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema katika mechi ya pili dhidi ya Merrikh ataandaa timu katika mazingira sahihi, ubora na umakini zaidi ya awali.

Gomes alisema kukosekana kwa baadhi ya wachezaji atatafuta njia nyingine ambayo itakuwa mbadala na sahihi kwao ili kwenda kucheza katika subira ule ule na kupata matokeo mazuri.

"Tunarudi nyumbani tutacheza mechi moja ya ligi na baada ya hapo tutaangalia jinsi gani ya kutaharisha timu ili kuwa na kiwango bora zaidi ya huko, tutacheza nyumbani mbinu zetu kitakuwa tofauti na tulizoonyesha ugenini," alisema.

"Wachezaji wangu wote wapo vizuri kukosekana kwa mmoja kuna mwingine ambaye anaweza kuwa mbadala wake na tukafanya vizuri kama ilivyokuwa michezo mingine," alisema Gomes.