White ambadili Alexander-Arnold kikosi cha England Euro 2020

White ambadili Alexander-Arnold kikosi cha England Euro 2020

Muktasari:

  • Gareth Southgate amemchagua Ben White kuchukua nafasi ya Trent Alexander-Arnold katika kikosi cha England kitakachoshiriki fainali za mataifa ya Ulaya, Euro 2020, baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa kirafiki ulioisha kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Romania.

London, Uingereza (AFP). Gareth Southgate amemchagua Ben White kuchukua nafasi ya Trent Alexander-Arnold katika kikosi cha England kitakachoshiriki fainali za mataifa ya Ulaya, Euro 2020, baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa kirafiki ulioisha kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Romania.

Beki huyo wa kati wa Brighton mwenye umri wa miaka 23 alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na England wiki iliyopita waliposhinda kwa bao 1-0 dhidi ya Austria na akaongeza kuaminika kwake kwa kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa Jumapili dhidi ya Romania.

Alexander-Arnold aliondolewa kikosini baada ya kuumia misuli ya paja katika mechi dhidi ya Austria na ilimchukua muda Southgate kuamua mchezaji gani kati ya waliokuwa katika orodha ya akiba aingie katika timu yake.

White alicheza vizuri msimu huu akiwa na Brighton -- ambayo ni klabu yake ya kwanza Ligi Kuu -- baada ya kuwa nguzo muhimu wakati Leeds United ikipanda daraja msimu wa mwaka 2019/20, alipokuwa akiitumikia klabu hiyo kwa mkopo.

Southgate ameamua kumchukua beki huyo wa kati katika kipindi ambacho nahodha wa Manchester United, Harry Maguire anapambana kurudi katika hali ya kawaida baada ya kuumia kifundo cha mguu.

Beki wa Everton, Ben Godfrey na nahodha wa Southampton, James Ward-Prowse ni wachezaji wengine waliokuwa katika orodha hiyo ya kusubiri na wote walikuwa katika kikosi kilichoanza mechi dhidi ya Romania, wakati Jesse Lingard na Ollie Watkins pia walikuwa katika orodha ya kusubiri, lakini sasa watarejea nyumbani.

England itaanza mechi zake za Euro 2020 Jumapili itakapopambana na Croatia kwenye Uwanja wa Wembley. Croatia iliilaza England katika nusu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018.