Ya Mondi, Hamisa Rick Ross atawezana

Muktasari:

Inaelezwa mahusiano ya Diamond Platnumz na Hamisa Mobetto yalianza kwa siri wakati mwimbaji huyo akiwa na mrembo Zari The Bosslady lakini baadaye hilo likaja kubainika baada ya Hamisa kujaliwa mtoto wa pili, Daylan.

Inaelezwa mahusiano ya Diamond Platnumz na Hamisa Mobetto yalianza kwa siri wakati mwimbaji huyo akiwa na mrembo Zari The Bosslady lakini baadaye hilo likaja kubainika baada ya Hamisa kujaliwa mtoto wa pili, Daylan.

Kwa mujibu wa Zari The Bosslady, jambo hilo ni miongoni mwa mambo makubwa yaliyosababisha kuachana na Diamond wakiwa tayari wamejaliwa kupata watoto wawili.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye ukurasa wa Instagram Februari 14, 2018 (Valentineís Day) Zari The Boss Lady alitangaza rasmi kuachana na Diamond kutokana na kuchoshwa na habari za kusalitiwa alizodai alikuwa akizisikia mara kwa mara.

Machi 2018 kwenye Mahojiano na kipindi cha 10 Over 10 cha Citizen TV Kenya, Zari alieleza kukereka zaidi na kitendo cha Diamond kwenda kuzaa nje ya mahusiano yao na kusema ni mtu ambaye alimvunjia utu wake.

Zari alienda mbali zaidi na kusema hawezi kumzuia mwanaume kuchepuka lakini anapochepuka basi atumie kinga (kondomu), lakini mwanaume (Diamond) anayeenda kuzaa nje ina maana hatumii kinga kitu ambacho ni hatari sana kwani kinaweza kumletea magonjwa ndani.

Baada ya hilo kupita na kabla ya Diamond kukutana na Tanasha Donna kutoka Kenya, iliaminika Chibu angetulia kwa Hamisa na pengine hata kumwoa lakini ghafla upepo ulibadilika. Kwani vipi?.

Ni baada ya kuvuja kwa sauti mtandaoni zilizotajwa kuwa za Hamisa akiongea na mganga ili apatane na familia ya Diamond, hasa Bi. Sandra (Mama Dangote).

Kitendo hicho kilimkasirisha sana Diamond na kudai kama Hamisa anaweza kwenda kwa mganga kuloga ili apatane na mama yake, basi ashindwi kumuua mama yake ili aolowe.

Diamond alieleza hayo akihojiwa na kipindi cha Refresh kinachoruka Wasafi TV, hiyo ilikuwa Septemba 5, 2018. Ilipofika Septemba 21, 2018 Hamisa Mobetto alivunja ukimya kuhusu tuhuma hizo za kutaka kumlonga Diamond na mama yake mzazi.

Akizungumza na kipindi cha The Playlist cha Times FM, kwanza Hamisa alikiri sauti zilizovuja mtandaoni zilikuwa za kwake, ila alikanusha vikali kuwa alikuwa ana mpango wa kumloga Diamond na Mama yake. Mrembo huyo mwenye taji la Miss XXL alisema kwanza alikuwa haongei na mganga kama ilivyodaiwa, bali ni Sheikh ambaye alikuwa anataka amfanyie dua ili aweze kupatana na familia ya Diamond.


Wapi Walikosana?

Wengi wakawa wanajiuliza ni wapi Hamisa alikosana na Familia ya Diamond hasa Mama Dangote?

Inadaiwa baada ya Diamond kumpa ujauzito Hamisa wakati ndio penzi lake na Zari limeshamiri, familia ya Mwimbaji huyo ilipanga kufanya siri Zari asijue lakini waendelee kumhudumia Hamisa kitu ambacho Mrembo huyo hakikumuingia akilini.

Hamisa alitaka kila mtu ajue amezaa na Diamond na alikuwa akidokeza kila wakati mtandaoni mtoto ni wa Diamond kitu kilichoibua vita kali ya maneno kati yake na Zari.

Baada Hamisa kujifungua, akiwa bado yupo Hospitalini alikuwa akipelekewa chakula na Mama Diamond kwa siri.

Ghafla kipindi cha Shilawadu cha Clouds TV kikarusha kipande cha video kikimuonyesha mama Diamond akienda hospitalini na hapo ndio ukawa mwanzo wao kukosana. Iliaminika Hamisa ndiye aliyewang’ata sikio Shilawadu mama Diamond angefika hospitalini hapo kumjulia hali.

Kuruka kwa video hiyo inadaiwa ni moja ya mambo ya mwanzo ambayo yalitia doa uhusiano wa Mama Diamond na Zari The Bosslady ambaye walikuwa wameivana sana.


Hamisa alionywa Mapema

Ukweli mwingine ambao wengi hawaujui ni kamba Hamisa Mobetto alikuwa amepewa onyo mapema kuingia kwenye mahusiano na Diamond ni jambo ambalo litamsumbua.

Meneja wa Diamond, Babu Tale akiongea na Wasafi TV, Juni 5, 2018 alisema kabla ya Hamisa kuzaa na Diamond alishawaonya kwani wakati huo Diamond alikuwa katika mahusiano na Zari.

“Kabla Hamisa hajapata ujauzito, tulikuwa tunashuti video ya Salome nikamwambia Zari sio adui yako, kama una mapenzi na Diamond mpende ila kama unataka kumkomesha, kamkomeshe Lulu, ila kama unataka kufanya hivyo haipendezi,” alisema. “Nikamwambia pia Diamond kama unafanya ujana, inatakiwa pia uangalie ujana wako yule demu (Zari) amekuja huko from no where amekuzalia mtoto pia,” alisema Tale.


Hamisa na Diamond

Kwa mujibu wa Hamisa Mobetto, anadai alijuana na Diamond kitambo tangu akiwa mwanafunzi wa sekondari na Diamond hajatoka kimuziki. Yaani ukaribu wao ulianza kabla hata ya Hamisa hajazaa mtoto wake wa kwanza na Majizo.

Septemba 2018 Hamisa alimweleza Mtangazaji wa kipindi cha Mambo Mseto kinachoruka Citizen Radio Kenya, Mzazi Willy Tuva alimjua Diamond kipindi ambacho hana hata simu ya mkononi.

Ingawa wengi wanaamini penzi la Diamond na Hamisa lilianza mwaka 2016 pale Mrembo huyo alipotokea kwenye video ya wimbo wa Mwimbaji huyo inayokwenda kwa jina la Salome akishirikiana na Rayvanny. Hata hivyo, ukweli ni Hamisa alikuwepo kwenye maisha ya Diamond ya kimuziki tangu mwaka 2013 alipofanya ‘back vocal’ za wimbo wa Diamond uitwao Nikifa Kesho kitu ambacho wengi pia hawakijui.

Pia sauti ya kike inayosikika kwenye wimbo wa Diamond, Mbosso na Lava Lava ‘Jibebe’ ni ya Hamisa. Ndiyo!, ni ya Hamisa, zile ‘I like’ zinazosikika kwenye ngoma hiyo ni sauti ya Bibie.

Sasa Hamisa anatajwa kuwa na mahusiano na Rapa wa Marekani, Rick Ross mara baada ya hivi karibuni kuonekana wakijiachia Dubai.

Maswali yamekuwa ni mengi ikiwa wawili hao watakuwa kwenye mahusiano, yatakuwa ni ya namna gani ukizingatia umbali baina yao, kazi na umaarufu wao.