Yanga iige Simba kwa lipi?

ULIPOWASHA televisheni ukaona haiunganishi na king’amuzi, kitu cha kwanza kufanya ni kwenda kuangalia kama waya unaotoka kwenye king’amuzi umeunganishwa vizuri na runinga.

Ukikuta umeunganishwa vizuri, basi utahisi kuna tatizo jingine; labda waya unaotoka kwenye dishi haujaunganishwa vizuri na king’amuzi. Ukikuta umeunganishwa vizuri basi sayansi nyingine itatumika; utatoa kadi kwenye king’amuzi na kuifunga kwenye fulana au shati lako na kuirudisha. Ikishindikana utapiga simu huduma kwa wateja nao wakishindwa kuona tatizo kwenye mitambo yao watakushauri uite fundi, ambaye bila shaka atamaliza tatizo lako.

Ndivyo tunavyotakiwa kufanya kila wakati. Huwezi kuanza kutafuta suluhisho la tatizo kabla ya kuangalia kama mambo ya msingi yamefanyika. Pale unapogundua umetekeleza mambo yote ya msingi lakini hakuna linaloendelea, basi ndio wakati mwafaka wa kuita mtaalamu wa kuiondoa kabisa tatizo.

Yanga imeondolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na karibu vitu vyote muhimu. Ina kocha anayekidhi vigezo vyote muhimu, ina wachezaji wanaostahili sehemu zote muhimu, wenye uzoefu katika soka la kimataifa, wenye kila sifa ambayo kocha yeyote angependa wawe nao, ina viongozi vijana na wabunifu kama dunia ya sasa inavyohitaji.

Lakini haieleweki imekuwaje ikashindwa kwa mara nyingine kuvuka hatua ya kawaida kabisa ya raundi ya kwanza dhidi ya timu ya kawaida kabisa ya Al Hilal ya Sudan!

Hapo ndipo viongozi na wadau wanalazimika kukuna vichwa kujiuliza; kulikoni?

Vijembe vya huko mitaani ni Yanga waiige Simba, ambayo kwa kipindi cha miaka takriban sita imefuzu mara tatu kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, wakati Yanga inajivunia kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufikia hatua hiyo mwaka 1998 wakati muundo wa ligi ulipoanzishwa katika michuano ya Klabu Bingwa.

Baada ya hapo, Yanga ilimudu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016, kwa mara nyingine ikiwa timu ya kwanza ya Tanzania kufikia hatua ya makundi, ikitokea hatua za mwanzo za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Haina mafanikio mengine makubwa, lakini Simba, ambayo mwaka 1993 ilifika fainali ya Kombe la CAF, sasa ni kama inataka ifike nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa imeshazoea upinzani na vikwazo vingi ilivyokumbana navyo katika miaka mitano iliyopita; cha muhimu ikianza kupata ushindi ugenini!

Yanga iige nini kwa Simba ndilo swali ambalo halijatolewa jibu na hao wanaoishauri klabu hiyo ya Jangwani.

Pengine ni wakati wa kuanza kuangalia kama waya unaotoka kwenye dishi umeunganishwa vizuri na king’amuzi na baadaye kuangalia vitu vingine muhimu kama vimeunganishwa vizuri kabla ya kutafuta fundi anayejua zaidi nini hasa kinakosekana na kushauri njia ya kukipata.

Kwa jinsi mechi za raundi ya kwanza dhidi ya Al Hilal zilivyokwenda, utakuwa mtu wa ajabu sana kuwabebesha mzigo wachezaji ama benchi la ufundi kutokana na matokeo ya sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Mkapa na kipigo cha bao 1-0 jijini Khartoum, Sudan.

Wachezaji walijituma kwa dakika zote tisini, ingawa tatizo la kuanguk kwa Dickson Job lilitoa mwanya kwa Hilal kusawazisha na ile chenga aliyopigwa Bakari Mwamnyeto jijini Khartoum na kukosekana watu wa kuziba nyuma yake, ndiyo yaliyoigharimu timu. Lakini ni makosa hayo pekee yanayoweza kuonekana kwa macho makavu au yako mengine ya kiutawala, kiutendaji, kimuundo na mambo mengine ya nje ya uwanja.

Binafsi naangalia utendaji na muundo, ambao unahusisha uchaguzi wa watu wanaopewa dhamana kuiongoza klabu na wanaopewa dhamana kutenda kila kinachostahili na kwa wakati.

Pamoja na mabadiliko ambayo Simba imesema imeyafanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, haijawa na haraka ya kuondoa watu muhimu katika nafasi za juu na ama ushauri.

Ukianzia juu kabisa, Mohamed Dewji yuko katika mpira kwa miaka mingi sana na ndiye aliyeiongoza Simba kucheza hatua ya makundi kwa mara ya kwanza mwaka 2003. Nahisi Mo anajua kila kona na kila mazingira ambayo yanatakiwa yashughulikiwe hasa kunapokuwa na mechi muhimu. Huwezi kumuona kila wakati katika masuala ya uendeshaji klabu.

Chini yake kuna watu kama Crescentius Magori, Said Nassor Mkigoma, Salim Try Again, Mulamu Ng’ambi na Mwina Kaduguda ambao wana uzoefu usio na shaka katika soka la kimataifa, achilia mbali la ndani. Wengine ni mwenyekiti Murtaza Ally Mangungu, Seleman Haroub, Hussein Kita, Asha Baraka, Zawadi Kadunda na Rasshid Abdallah Shangazi, mbunge wa Mlalo aliyeteuliwa kushika nafasi ya Barbara Gonzalez.

Awali alikuwepo Hayati Zacharia Hanspope na Sued Nkwabi wakati katika nafasi za uteuzi yuko Kassim Dewji. Ukiangalia safu hiyo ya uongozi ni mchanganyiko wa watu wenye uzoefu katika soka, uzoefu katika uongozi na uzoefu katika biashara.

Sina shaka hawa wanajua mazingira tofauti ya ndani na nje ya uwanja yanayoweza kuvuruga saikolojia ya wachezaji kabla na baada ya mechi kwa kutumia uzoefu tofauti wa yale ambayo wamekuwa wakikutana nayo kwa miaka kadhaa waliotumikia mpira.

Wengi wanaweza kukimbilia kusema mazingira ya nje ya uwanja ni rushwa na uchawi, la hasha! Mazingira ya nje ya uwanja ni mengi. Masilahi ya wachezaji, motisha, saikolojia, mbinu chafu za wapinzani, maandalizi ya timu (safari, malazi, masilahi n.k). Vitu kama kucheleweshwa uwanja wa ndege, kupangiwa uwanja mbovu wa mazoezi, kucheleweshwa kuingia hotelini, uteuzi wa waamuzi na sheria na kanuni kuhusu matayarisho ya mechi.

Wakati Carlos Alberto Perreira alipokuwa anaiongoza Brazil kwenda fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1994 alisema hangependa kuona mchezaji wake yeyote akipata tatizo ambalo lingemvuruga kisaikolojia. Yale matatizo tunayoyaona madogomadogo kama kuchelewa kupata vyumba hotelini, kuzubaa uwanja wa ndege kusubiri basi na kwa huku kwetu, wachezaji kusubiri mzozo baina ya maofisa wa timu na wenyeji ndipo waingie uwanjani, Perreira hakutaka kuyaona.

Leo, vurugu kabla ya timu kuingia uwanjani zimekuwa ni vitu vya kawaida na pengine wasio na uzoefu wanaona ni sifa kupambana getini, kumbe muda huo huvuruga wachezaji kisaikolojia.

Wakati refa wa mechi ya Simba na TP Mazembe anabadilishwa miaka mitatu iliyopita, hakuwa Sued Nkabi aliyepaza sauti kuona kuwa kuna mchezo mchafu, bali Hanspope na alikuwa na hoja zake. Ipo mifano mingi ya kuonyesha uzoefu unavyowasaidia Simba kufanya vizuri kimataifa, achilia mbali jicho lao makini kwa James Phiri, Austine Okrah, Pape Ousmane Sackho, Henock Inonga, Peter Banda na Claoutus Chama, ambao soka la Tanzania hata halikuwahi kuwafikiria.

Ukigeukia Yanga unaona ugeni mtupu. Mwenyekiti Hersi Said ndio kwanza anaanza kuonekana kwenye soka kupitia kwa mdhamini GSM. Huko nyuma hakuwahi kubeba majukumu mazito kama ilivyo kwa kina Magori, Kassim Dewji, Try Again. Ndio kwanza anaanza kupata uzoefu katika nafasi nyeti ya rais wa klabu.

Chini yake yuko Arafat Haji, ambaye ni makamu wa rais. Huyu naye ni mgeni hasa unapoangalia soka la kimataifa, humwona akibeba majukumu mazito ambayo yangemwezesha kupata uzoefu wa kumsaidia katika nafasi yake ya sasa.

Chini ya wawili hao wako Yanga, Makaga, Seif Gulamali, Rogers Gumbo, Munir Seleman na Alexander Ngai. Hawa ugeni wao katika soka la ushindani la kimataifa hauna shaka hata kidogo. Kwa hiyo kwa kundi kama hilo, ni lazima utasubiri ma