Yanga kamili yaifuata Mazembe

Dar es Salaam. Yanga inahitaji pointi zote sita dhidi ya TP Mazembe kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuondoka na kikosi cha wachezaji wote wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya mchezo huo wa Jumapili.

Yanga inaifuata TP Mazembe kifua mbele baada ya kupata matokeo mazuri nyumbani ikiifunga mabao 3-1, huku tayari imefuzu kushiriki hatua ya robo fainali kwenye mashindano hayo.

Akizungumza jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Salehe alisema ni wachezaji wanne tu ambao watakosekana kwenye msafara huo kutokana na matatizo mbalimbali, huku akithibitisha kuwa wengine wote watasafiri leo.

Saleh alisema nyota watakaokosekana kwenye msafara wa leo ni Denis Nkane, Abuutwalib Msheri, Dickson Ambundo na Bernard Morrison, huku wachezaji wengine wote wakiondoka asubuhi ya leo.

“Wachezaji wote isipokuwa wanne ndiyo watakosekana, huku wengine wa kimataifa walioitwa kwenye timu zao za taifa tukiungana nao nchini DR Congo, ambao ni Stephen Aziz Ki, Fiston Mayele, Kennedy Musonda na Djigui Diarra,” alisema mratibu huyo.

Wachezaji walioondoka leo ni makipa Eric Johora, Metacha Mnata mabeki Djuma Shaban, Kibwana Shomari, Joyce Lomalisa, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, David Bryson.

Viungo Salum Abubakar, Khalid Aucho ambaye amejiunga na timu jana akitokea timu ya taifa ya Uganda, Zawadi Mauya, Farid Musa,Yanick Bangala, Jesus Moloko na Jesus Moloko huku washambuliaji Mayele na Musonda wakiungana nao nchini Congo.

Wakati miamba hiyo ikiwa dimbani, tayari Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza waamuzi watakaochezesha mechi hizo na kwa Simba itachezeshwa na Ahmad Heeralall kutoka Mauritania, huku Yanga ikiwa na mwamuzi kutoka Algeria, Lahlou Benbraham.

Rekodi zinaonyesha katika michezo 13 ya kimataifa aliyochezesha Heeralall, ni mechi moja tu ambayo hajatoa kadi ya njano, huku nyekundu ikiwa ni moja.

Kwa upande wa mwamuzi wa mechi ya Yanga, Lahlou amechezesha michezo 10 na kati ya hiyo, ametoa kadi za njano 31 na nyekundu moja tu.

Kwenye michezo hiyo 10 aliyochezesha timu zilizocheza nyumbani zimeshinda mitano, sare miwili huku zile za ugenini zikishinda mechi tatu.

Ushindi mkubwa kwa timu iliyokuwa nyumbani ambayo mwamuzi huyo alichezesha ni ule wa Wydad Casablanca ya Morocco ilipoibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Petro de Luanda ya Angola wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Aprili 3, mwaka jana.