Yanga: Njooni muone, Kisinda ndani

HAKUNA namna. Ndivyo unavyoweza kusema wakati watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga watakapoikabili Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ushindi kwa vigogo hao bila ya shaka utakuwa na maana kubwa kwa timu hiyo kutokana na sababu nne tofauti.

Timu hizo zitavaana kuanzia saa 1:00 usiku, huku Ruvu ikiwa ndiye mwenyeji wa mchezo huo wa raundi ya tano wa ligi hiyo ambayo kabla ya mechi ya jana usiku, Namungo ilikuwa kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 11 baada ya juzi kulazimishwa suluhu nyumbani na KMC.

Sababu ya kwanza kwa Yanga ni kutaka kurejea kileleni mwa msimamo, huku ya pili ikiwa ni kujiweka sawa kisaikolojia kabla ya mechi yao ya awali ya nyumbani ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan itakayopigwa Jumamosi hii hapo hapo Kwa Mkapa.

kadhalika matokeo ya ushindi yataifanya izidi kuboresha rekodi ya kucheza idadi kubwa ya mechi za Ligi Kuu bila kupoteza kwani itafikisha michezo 42 tangu ilipofungwa na Azam Aprili 25 mwaka jana.

Sababu ya nne ni kuifanya isiwe na presha kubwa itakaporudi kwenye ligi Oktoba 23 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba ambao usiku wa jana walikuwa uwanjani kuvaana na Dodoma Jiji.

Kuanzia leo inapokabiliana na Ruvu hadi Oktoba 29, Yanga itakuwa na mechi sita itakazocheza huku ikiwa na muda mfupi wa mapumziko kutoka moja hadi nyingine na iko wazi itapaswa kuzichanga karata vizuri katika michezo hiyo, ndivyo inavyoweza kujiweka katika mazingira mazuri ya kutamba msimu huu au kufanya vibaya.

Baada ya Ruvu, Yanga itakuwa na siku nne za kujiandaa na dhidi ya Al Hilal na baada ya hapo itasafiri kwenda Sudan kwa mchezo wa marudiano itakayochezwa Oktoba 16 na siku sita baadaye itakabiliana na Simba Oktoba 23 kabla ya kuvaana na KMC Oktoba 16 na kuimaliza Oktoba kwa kuifuata Geita Gold ugenini mechi itakayopigwa Oktoba 29.

Ndani ya uwanja leo zinakutana timu mbili zilizoimarika zaidi msimu huu kulinganisha na msimu uliopita jambo ambalo hapana shaka litafanya mchezo huo kuwa na ushindani wa aina yake.

Matokeo ya mechi za mwanzo za msimu huu yanaweza kudhihirisha hilo, kwani Yanga katika mechi nne za mwanzo imepata ushindi mara tatu na kutoka sare moja, huku Ruvu ikishinda tatu na kupoteza mbili.

Wakati Yanga ikipaswa kumchunga zaidi Rashid Juma aliyefunga mabao mawili kati ya matano ya Ruvu, huku maafande hao, jicho la ziada litakuwa kwa Fiston Mayele mwenye mabao tisa hadi sasa katika mechi za mashindano yote, yakiwamo matatu ya Ligi Kuu na sita ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo wa leo, Yanga itamkosa Stephane Aziz Ki aliyechelewa kutua nchini baada ya kukwama Morocco alikoenda kuitumikia Timu ya Taifa ya Burkina Faso kwa kubainika kuambukizwa Uviko-19.

Yanga imekuwa na historia nzuri ya ubabe dhidi ya Ruvu mara zinapokutana hasa katika mechi za Ligi Kuu Bara na kuthibitisha hilo, katika mechi tano zilizopita baina yao, Yanga imeshinda michezo minne na kutoka sare mara moja.

Kocha wa Ruvu, Charles Boniface Mkwasa alisema anatambua ubora wa Yanga na ugumu wa kukabiliana nao lakini wamejipanga kuhakikisha watapata ushindi.

“Tunacheza na watu wenye ubora lazima tucheze kwa tahadhari kubwa na umakini zaidi ili tuweze kuwadhibiti. Sisi wa benchi la ufundi tumeandaa mpango wetu wa kukabiliana na Yanga,” alisema Mkwasa, nyota na kocha wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.

Mbali na mchezo huo wa Kwa Mkapa, leo Jumatatu pia kutakuwa na mechi nyingine mbili ikiwamo ya mapema itakayozikutanisha Coastal Union na Kagera Sugar itakayopigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga na usiku Azam iliyotoka kupoteza Mbeya mbele ya Tanzania Prisons itaialika Singida Big Stars Uwanja wa Azam Complex, kuanzia saa 2:15 usiku.