Yanga warejea Dar, waingia kambini kujinoa kuwamaliza Simba

Muktasari:

KIKOSI cha Yanga, kimerejea asubuhi ya leo Julai 19, kutokea Dodoma walipocheza mechi ya mwisho ya msimu Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji.

KIKOSI cha Yanga, kimerejea asubuhi ya leo Julai 19, kutokea Dodoma walipocheza mechi ya mwisho ya msimu Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji.

Mechi hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa Jamuhuri ulimalizika kwa suluhu na kuifanya Yanga kumaliza nafasi ya tatu msimu huu wakati Dodoma nafasi ya nane na pointi zao 44.

Kocha wa Yanga, Nabi Nasreddine ameonyesha kutotaka mzaha katika kikosi chake kuelekea mechi ya fainali kombe la Shirikisho (ASFC), ambayo watacheza dhidi ya Yanga.

Iko hivi, kikosi cha Simba mara baada ya kushinda bao 4-0, dhidi ya Namungo na kukabiziwa taji lao la ubingwa kocha, Didier Gomes alitoa mapumziko ya siku moja mpaka kesho Jumanne.

Kwa upande wa Nabi, wala hakutaka mzaha kwani mara baada ya kutoka kumalizana na Dodoma wamerejea hapa Dar, na moja kwa moja wachezaji wameingia kambini kwa ajili ya mchezo huo.

Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh alisema kikosi chao baada ya kutoka Dodoma kimeingia moja kwa moja kambini kwa ajili fainali ya kombe la ASFC, dhidi ya watani zao Simba.

"Hatujavunja kambi kutokana tunaenda kucheza mechi kubwa na siku zipo chache," alisema Saleh nakuongeza;

"Kuhusu tutaondoka Dar kwenda Kigoma itakuwa siku gani hilo sifahamu kama ambavyo tutaondoka na wachezaji wote au wengine watabaki."