Yanga yafikia rekodi ya Azam ikiichapa Polisi

Yanga yaifikia rekodi ya Azam ikiichapa Polisi

Muktasari:

  • Yanga imefikia rekodi ya Azam ya kucheza mechi 38 za Ligi Kuu bila kupoteza ambapo Azam ilifanya  hivyo  kati ya Feb 23, 2013 hadi Oktoba 25, 2014 huku Yanga ikiweka rekodi hiyo tangu Mei 15,2021 hadi leo Agosti  16, 2022.

ARUSHA. BINGWA mtetezi Yanga imeanza vyema Ligi Kuu Bara msimu wa 2022/23 baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhdi ya Polisi Tanzania katika mchezo ambao ulipigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

Yanga imefikia rekodi ya Azam ya kucheza mechi 38 za Ligi Kuu bila kupoteza ambapo Azam ilifanya  hivyo  kati ya Feb 23, 2013 hadi Oktoba 25, 2014 huku Yanga ikiweka rekodi hiyo tangu Mei 15,2021 hadi leo Agosti  16, 2022.

Haijawahi kuwa mchezo mrahisi pindi timu hizo zinapokutana kwani mara ya sita ambazo zimekutana Yanga imeibuka na ushindi mara mbili pekee huku zikitoka sare mara nne.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilianza kwa kasi kila timu ikishambulia lango la mpinzani wake kwa zamu ambapo ilishuudiwa dakika ya kwanza tu Yanga ikishindwa kupata bao baada ya Fiston Mayele kushindwa kuunganisha krosi ya Dickson Ambundo.

Dakika ya tisa ya mchezo Mayele alikosa mkwaju wa penati baada ya Jesus Moloko kuangushwa katika eneo la hatari na mchezaji wa Polisi Tanzania Shaban Stambuli ambapo mlinda lango wa Polisi Kelvin Igenderezi alifanikwa kuokoa mkwaju huo.

Licha ya kushambuliwa kwa kiasi kikubwa lakini Polisi waliweza kuwashangaza Yanga kwa kufunga bao dakika ya 34 kupitia Salum Kipemba ambaye alipiga shuti iliyomshinda mlinda lango wa Yanga Dgui Diara.

Yanga walisimama na kusawazisha dakika ya 42 kupitia Mayele ambaye aliunganisha mpira uliokuwa unazagaa langoni mwa Polisi Tanzania baada ya mlinda lango Igenderezi kuokoa mpira wa kichwa iliyopigwa na Mwamnyeto ambaye aliunganisha kona ya Shaban Djuma na kufanya dakika 45 za kwanza kukamilika kwa 1-1.

Kipindi cha pili kilianza Yanga wakiishambulia lango la Polisi huku ikikosa umakini kwa mshambuliaji wake Fiston Mayele ambapo hata hivyo dakika ya 85 Yanga ilipata bao la pili kupitia kwa Bakary Nondo baada ya kuunganisha kona iliyochongwa na Bernard Morrison.

Kikosi cha Yanga kilichoanza golini kulikuwa na Dgui Diara, Shaban Djuma, Joyce Lomalisa, Dickoson Job, Bakari Mwamnyeto, Khalid Aucho, Bigirimana, Mayele, Aziz Ki na Ambundo huku akiba wakiwa ni Mshery, Morrison, Bangala, Feisal, Sure Boy, Farid, Makambo, Bacca na Mauya.

Kwa upande wa Polisi kikosi kikosi kilichoanza ni Kelvin Igenderezi, Hassan Kiponda, Juma Ramadhan, Shaban Stambuli, Mohammed Mmanga, Salum Kipemba, Chilo Mkama, Rajab Athuman, Khamis Kinduru, Iddy Kipagwile, Salum Chuku akiba walikuwa ni Green, Better, Ally Omary, Salum, Sylvester Zuberi na Kelvin.

Mabadiliko kwa timu zote kwa upande wa Yanga walitoka Bigirimana, Ambundo, Mayele na Moloko ambapo nafas zao zilichukuliwa na Morrison, Makambo, Farid na Feisal huku kwa Polisi akitoka Shaban Stambuli na kuingia Abdul Karim Yunus.

Yanga itacheza mchezo wake wa pili Jumamosi hii dhidi ya Coastal Union ambao leo inacheza na KMC katika uwanja huo huo wa Sheikh Amri Abeid.