Yanga yafunga kazi Mbeya, kituo kinachofuata!

Tuesday November 30 2021
yangaaapic
By Saddam Sadick

Mbeya. Kwa mara ya kwanza Mbeya Kwanza umepoteza uwanja wa nyumbani baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga.

Ushindi huo unaifanya Yanga kuendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo wowote katika Ligi Kuu lakini kujihakikishia nafasi ya kubaki kileleni kwa pointi 19.

Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa, Yanga ilionekana kutakata zaidi kipindi cha kwanza ambacho kiliweza kuipa mafanikio kwa kufunga mabao mawili.

Bingwa huyo wa kihistoria ilijipatia mabao yake kupitia kwa Saido Ntibazonkiza dakika ya 16 kwa mpira wa adhabu baada ya Feisal Salum kuchezewa madhambi na beki wa Mbeya Kwanza, Miza Christom huku Fiston Mayele akipigilia msumari wa pili dakika ya 25 ya mchezo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Mbeya Kwanza kuonesha uhai zaidi kwa kutengeneza mashambulizi lakini safu ya ushambuliaji iliishiwa mbinu za kusawazisha mabao baada ya kukutana na ngome ya Yanga.

Timu zote zilifanya mabadiliko ambapo Yanga iliwatoa Mayele, Mauya na Ntibazonkiza na nafasi zao kuchukuliwa na Makambo, Yusuph Athuman na Kibwana Shomari, huku Mbeya Kwanza wakiwatoa Hamis Kanduru na Deogras Ambakisye na kuwaingiza Paul Peter na Jimmy Shoji, mabadiliko ambayo hayakubadili matokeo.

Advertisement

Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Harerimana Haruna amesema kutokana na uzoefu wa Yanga, nguvu ya mashabiki ndio iliwanyima ushindi.

"Tumepoteza umakini lakini tulipambana, wapinzani ni wazoefu lakini zile nguvu za mashabiki wao ziliwapa nafasi kucheza kwa kujiamini, hatujakata tamaa na niwaombe mashabiki wetu waendelee kutupa sapoti" amesema Haruna.

Kwa upande wake Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto amesema baada ya ushindi huo wanaenda kujipanga upya na mechi inayofuata akitamba kuwa matarajio yao ni kushinda dhidi ya Simba.

"Kila mechi ina maandalizi yake lakini tunaamini tutajipanga vizuri kuhakikisha tunapata pointi tatu dhidi ya Simba, tuko vizuri na imara na tayari kwa kila mechi" amesema Mwamunyeto.

Advertisement