Yanga yaipigisha Mazembe kwata kwa Mkapa

Mshambuliaji wa Yanga, Kennedy Musonda akishangilia bao alilofunga dhidi ya TP Mazembe katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika. Picha na Loveness Bernard

Muktasari:

  • Yanga imechukua pointi tatu muhimu wakiifunga TP Mazembe mabao 3-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kupanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa kundi D.

Dar es Salaam. Wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika Yanga, imepata ushindi wa kwanza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe kutokea DR Congo.

Yanga imepata ushindi wa mabao 3-1, kwenye mchezo uliyomalizika usiku huu ikitumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani kwa kushinda mechi ya pili kwenye hatua ya makundi.

Mabao ya Yanga yakifungwa na Kennedy Musonda, Mudathir Yahya na Tuisila Kisinda aliyeingia kipindi cha pili.

Zifuatazo ni dondoo zilizotokea kwenye mchezo huu uliyokuwa ukifuatiliwa na wapenzi wengi wa soka ndani na nje ya Tanzania;

Yanga ilipata mabao mawili kipindi cha kwanza ndani ya dakika 11 na kwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao 2-0.

Bao la kwanza la Yanga lilifungwa dakika 7, na mshambuliaji mpya, Kennedy Musonda baada ya kuunganisha mpira wa faulo iliyochongwa na Djuma Shabani.

Mudathir Yahya aliifungia Yanga bao la pili dakika 11, baada ya mabeki wa TP Mazembe kufanya uzembe wakizani mfungaji ameotea.

Mazembe ilifanya mabadiliko ya kwanza kipindi cha kwanza dakika 34, ilimtoa Glady Likonza na kuingia Mukoko Tonombe mchezaji wa zamani Yanga.

Mabadiliko hayo yalifanyika kutokana na Mazembe kuzidiwa eneo la kiungo Yanga ikiwa na watano yenyewe ikiwa na viungo wawili asilia.

Kipindi cha kwanza ilitoka kadi moja ya njano aliyoonyeshwa kiungo Khalid Aucho.

Yanga kipindi cha pili ilifanya mabadiliko ya wachezaji wanne waliingia, Tuisila, Azizi Ki, Zawadi Mauya na Clement Mzize.

Mazembe ilipata bao dakika 80, kupitia kwa Alex Ngonga aliyepiga faulo ya moja kwa moja mpira kumshinda kipa wa Yanga, Djigui Diarra.

Kipindi cha pili Diarra alikuwa kwenye kiwango bora zaidi baada ya kuokoa nafasi tatu za kufunga ilizopata wachezaji wa TP Mazembe.

Yanga inaweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutokea Tanzania kuifunga TP Mazembe kwenye mechi za kimashindano.

Yanga mechi ya kwanza ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0, ugenini dhidi ya US Monastir wakati TP Mazembe ilishinda nyumbani mabao 3-1, dhidi ya Real Bamako.

Kutokana na matokeo ya leo Yanga inakwenda nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi ā€˜Dā€™ ikiwa imefikisha pointi tatu, huku Mazembe ikiwa nafasi ya nne ikilingana pointi.

Monastir inakuwa vinara wa kundi baada ya kufikisha pointi nne huku Real Bamako ya Mali ikiwa na pointi moja na inaburuza mkia wa kundi D.

Baada ya mchezo wa leo Februari 19, Yanga itakwenda kucheza mchezo wa tatu katika kundi ugenini dhidi ya Real Bamako na mchezo huo utapigwa kwenye ardhi ya Mali.

Wakati huo TP Mazembe itakuwa na kazi dhidi ya vinara wa kundi US Monastir.