Yanga yazuga, Ibenge apaniki

Muktasari:

  • MABAO la Feisal Salum ‘Feitoto’ na nahodha Bakary Mwamnyeto juzi usiku yaliipa Yanga ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mkapa katika mechi ambayo winga, Tuisila Kisinda alianza kwa mara ya kwanza. Bao pekee la Ruvu waliokuwa wenyeji lilifungwa na Roland Msonjo.

MABAO la Feisal Salum ‘Feitoto’ na nahodha Bakary Mwamnyeto juzi usiku yaliipa Yanga ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mkapa katika mechi ambayo winga, Tuisila Kisinda alianza kwa mara ya kwanza. Bao pekee la Ruvu waliokuwa wenyeji lilifungwa na Roland Msonjo.

Katika mchezo huo Yanga mastaa wengi walizuga kwa kucheza viwango vya kawaida wakihifadhi nguvu kwa mechi ya wikiendi dhidi ya Al Hilal ambao baadhi ya maafisa wao walikuwa jukwaani.

Kipindi cha kwanza Ruvu Shooting walicheza mchezo wa kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza huku Kocha wao, Charles Mkwasa akimsimamisha Rashid Juma kwenye eneo la ushambuliaji na kujaza viungo ambao walikuwa na kazi ya kupeleka mashambulizi mbele.


Yanga ambayo ilifikisha pointi 13 sawa na Simba, kupitia kwa Fiston Mayele walikosa mabao kadhaa kipindi cha kwanza, Shooting wao walikuwa wanaanzisha vizuri mashambulizi lakini kwenye kumalizia walikuwa na changamoto ya kutokuwa na mchezaji aliyesimama ndani ya boksi haswa kipindi cha kwanza.

Nidhamu ya kujilinda ilionekana kubwa upande wa Shooting kwani hata walipokuwa wanapoteza mpira ilikuwa rahisi kuiwahi.

Hali hiyo iliifanya Yanga itumie zaidi mbinu ya mipira ya pembeni kwa mabeki wake Joyce Lomalisa (kushoto) na Djuma Shaban (Kulia) kupeleka mashambulizi.

Dakika 47 Ruvu Shooting ilikosa kuandika bao la kwanza baada ya kupigwa pasi za haraka ndani ya boksi na Rashid Juma alifyatua shuti kali na mabeki wa Yanga waliucheza na kuwa kona isiyokuwa na faida.

Dakika 52 Yanga ilipata bao la kwanza kupitia kwa Feitoto aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Mkongomani, Joyce Lomalisa kutokea upande wa kushoto.

Dakika 55, Mayele aliwatoka mabeki wa Ruvu Shooting na kufyatua shuti kali lakini kipa Hussein Masalanga akalipangua. Mwamnyeto alifunga bao la pili dakika ya 71 kwa kuunganisha kwa kichwa kona ya Dickson Ambundo aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Farid Mussa.

Bao la Ruvu lilifungwa na Msonjo katika dakika 86 akiunganisha wavuni mpira wa kichwa aliodondoshewa miguu na beki Lomalisa aliyekuwa akijaribu kuokoa mpira wa kona na kumuacha Diarra akiwa hana la kufanya. Matokeo ya jana yaliwaacha Ruvu na pointi zao 9.

Ruvu Shooting: Hussein Msalanga, Michael Aidan, Mpoki Mwakinyuke, Tariq Abed/Chanongo, Frank Nchimbi, Rolland Msonjo, Ally Kombo, Shaban Msala, Samson Joseph, Rashid Juma/Bilal na Abalkasim Suleiman.

Yanga: Djigui Diarra, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Yanick Bangala, Salum Abubakary/Aucho, Farid Mussa/Ambundo, Fiston Mayele/Makambo, Feisal Salum na Tuisila Kisinda/Nkane.


IBENGE APANIKI

KOCHA wa Al Hilal ya Sudan, Mkongomani Florent Ibenge ameangukiwa na kitu kizito jijini hapa na kujikuta akipaniki na kung’aka. Ameikosa TP Mazembe na kuambulia kipigo kikali.

Hilal iko Lubumbashi kwa siku kadhaa sasa ikicheza mechi za kirafiki kujiandaa na mechi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga inayochezwa Dar es Salaam Jumamosi ijayo.

Iko hivi; Hilal walianza kutangaza tangu wiki iliyopita kwamba wanacheza na Mazembe huku pande zote mbili zikiwa hazijaafikiana. Hilal walipotua Kocha wa Mazembe akaikataa mechi hiyo kwa madai kwamba haikuwa kwenye programu zake. Juzi Jumapili Saa 9 Alasiri, Hilal wakaenda Uwanjani wakijua bado wanakwenda kucheza na Mazembe lakini badala yake wakakutana na Don Bosco Fc ambayo inashiriki Ligi Kuu na ni kama tawi la Mazembe kwani inamilikiwa na mtoto wa Moise Katumbi.

Kilichowashangaza wengi ni kwamba Don Bosco hawakuvaa jezi zao, walivalishwa uzi wa Mazembe na wakashinda mabao 3-1. Ibenge baada ya kushtukia kwamba si Mazembe akaamua kuendelea tu kucheza mechi hiyo ingawa walizidiwa pia kimchezo.

Baada ya mchezo huo, Ibenge alipoulizwa akang’aka; “Haijalishi tumecheza na nani, cha msingi ni kwamba tumenufaika na huu mchezo.”

Ibenge ameonekana kutofurahishwa na kilichotokea kwani Mazembe waliikwepa mechi hiyo kuhofia majeruhi ingawa yeye alidhani kwamba itakuwa rahisi kutokana na umaarufu wake nchini humo.