ZA NDAANI KABISA: Panga la Vigogo linakuja Yanga

Monday August 01 2022
zandani pic
By Mwandishi Wetu

HUKO Jangwani mambo ni moto, kwani baada ya mabosi wapya wa klabu ya Yanga kuingia madarakani chini ya Rais Injinia Hersi Said, Za Ndaani Kabisa zinasema kwa sasa lipo panga la mabadiliko linalokuja kwenye nafasi mbalimbali katika idara za klabu hiyo.

Taarifa Za Ndaani Kabisa zinasema uongozi mpya unafanya tathimini kubwa ya wafanyakazi wa klabu hiyo kuanzia sekretarieti hadi kwenye maeneo mengine kabla ya kufyeka baadhi ya vigogo.

Usishtuke sana pale utakaposikia baadhi ya majina makubwa yakienda na maji katika kuunda sekretarieti hiyo na mabadiliko hayo yanaweza kuja kutokana na matakwa ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji ambao Yanga walishaupitisha.

Mbali na sekretarieti hiyo, pia kuna mabadiliko mengine yanaweza kufanyika katika benchi la ufundi la timu hiyo ambalo linaweza kutangazwa wakati wowote kuanzia leo Jumatatu.

Za Ndaani Kabisa zinasema wapo maofisa ambao tayari wameshapewa mkono wa kwaheri katika benchi hilo, huku wengine wakipandishwa madaraja kutokana na utumishi wao.

Mbali na wanaondolewa, ziko sura mpya nazo zitajumuishwa katika utawala huo katika benchi hilo katika kuongeza ufanisi mkubwa.

Advertisement

Yanga ilifanya uchaguzi mkuu Julai 9 mwaka huu na mbali na Injinia Hersi, pia Makamu Rais alichaguliwa Arafat Haji na wajumbe watano wa Kamati ya Utendaji ambao ni; Yanga Makaga, Munir Seleman, Alexander Ngai, Rodgers Gumbo na Seif Gulamali.

Advertisement