Sherehe kila kona, Nyerere akienda Yugoslavia

Sherehe kila kona, Nyerere akienda Yugoslavia

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanganyika aliwasili mji mkuu wa Yugoslavia, Belgrade kwa ajili ya ziara ya siku tano, ambayo ilihusisha kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa nchi hiyo Josip Broz Tito pamoja na viongozi wengine wa taifa hilo.

Waziri Mkuu wa Tanganyika aliwasili mji mkuu wa Yugoslavia, Belgrade kwa ajili ya ziara ya siku tano, ambayo ilihusisha kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa nchi hiyo Josip Broz Tito pamoja na viongozi wengine wa taifa hilo.

Pamoja na mambo mengine, ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujadili mustakabali wa uhusiano wa mataifa hayo katika nyanja za kiuchumi na utamaduni.

Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Radolijub Calakovic aliongoza viongozi wa serikali, mawaziri na balozi wa Uingereza, Sir Michael Creswell kumpokea Nyerere kwenye uwanja wa ndege wa Zemun.

Kikundi cha wanafunzi 16 wa Tanganyika wanaoishi Belgrade wakiwa wamevaa nembo zenye picha ya Jomo Kenyatta, walipiga kelele kwa kutaja neno “Uhuru” walipata nafasi ya kupeana mkono na Nyerere.

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard


Moshi waandaa maonyesho ya mavazi

Maonyesho kwa ajili ya kuonyesha mavazi yatakayofaa kuvaliwa kwenye sherehe za uhuru yaliyoandaliwa na tawi la baraza la wanawake Tanganyika, yalifanyika mjini Moshi.

Wanachama 94 walihudhuria kwenye mashindano hayo ambayo yaliandaliwa na Bi Reder akisaidiana na Bi Steel pamoja na mweka hazina wa tawi hilo, Bi. Kassamali Hirji.

Mavazi mazuri yaliyotengenezwa kwa kutumia nyuzi, pamba na kunakshiwa vyema yalivaliwa na kuvutia watu wengi waliohudhuria kwenye mashindano hayo.

Pia vazi jipya la Tanganyika lilionekana kugusa hisia za watu wengi jambo lililofanya kupigiwa makofi kwa wingi.

Mavazi aina ya Saris na ya usiku yalionyeshwa kwenye mashindano hayo na kuvutia sana. Pia kulikuwa na nguo fupi kwa ajili ya hafla za usiku.

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard


Moshi yaandaa vilipuzi kwa ajili ya huru

Serikali wilayani Moshi ilitangaza kwamba sherehe za uhuru kwenye wilaya hiyo, zingeambatana na kazi ya kulipua vilipuzi vilivyonunuliwa kutoka Marekani maalumu kwa ajili ya shamrashamra hizo.

Huduma za ibada za madhehebu yote zilitakiwa kufanyika kabla ya saa tano katika siku ya mkesha wa uhuru na itakapofika saa tano kamili usiku, maandamano yaliyoandaliwa na TANU yangefanyika katika maeneo ya mijini wilayani humo na kuwasili katika eneo la Boma, kabla ya usiku wa manane kwa ajili ya sherehe ya kupeperusha bendera.

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard

Iringa mashindano ya urembo, matamasha ya vijana

Uwashaji wa vilipuzi, mashindano ya urembo, maonyesho ya vijana ni miongoni mwa mambo yaliyopendekezwa na kamati ya maandalizi ya uhuru kufanyika kwenye sherehe za uhuru Iringa.

Kwenye kikao, Mkuu wa wilaya alitoa ufafanuzi kuhusu sherehe ya kupandisha bendera ambayo ingefanyika usiku wa manane wa Desemba 8.

Ilipendekezwa kuwa uwashaji wa taa wakati bendera za Union Jack na Umoja wa Mataifa zinaposhushwa na kupandishwa ile ya Tanganyika.

Baada ya tukio hilo kutakuwa na tukio la kuwashwa kwa vilipuzi na fataki karibu na mlima, ambao bendera hiyo ingewekwa kwenye wilaya hiyo.

Ratiba ya siku nne pia ilitangazwa ambapo ilihusisha mchezo wa mpira wa miguu Desemba 8 ambayo ingekuwa fainali ya kombe la uhuru iliyoandaliwa na Jamii ya Ismaili.

Maonyesho ya vijana yalipangwa kufanyika kwenye uwanja wa wazi na kikombe kwa ajili ya mshindi wa maonyesho hayo kingekabidhiwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Iringa, Bi Z. Reeves.

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard