Sanaa na burudani katika miaka 60 ya Uhuru

Muktasari:

  • Imebaki miezi kama miwili kabla ya Watanzania kusherehekea miaka 60 ya Uhuru.

Imebaki miezi kama miwili kabla ya Watanzania kusherehekea miaka 60 ya Uhuru.

Tanganyika ilipata Uhuru Desemba 9, 1961 kabla ya kuwa Jamhuri 1962 na miaka miwili baadaye, Aprili 26, 1964, ikaungana na Zanzibar.

Katika umri wa miaka 60 Tanzania Bara inasherehekea mafanikio katika sekta mbalimbali ikiwamo kisiasa, kiafya, kiuchumi na kimaendeleo kwa ujumla huku michezo na burudani nayo haikubaki nyuma.

Hakuna siri sanaa na utamaduni hususan ile ya muziki, maigizo na ngoma asilia zimechangia katika kuhamasisha harakati za Uhuru na hata maendeleo ndani ya jamii hata baada ya kupatikana kwa Uhuru.

Miongoni mwa safari ndefu ya mafanikio ni katika nyanja ya sanaa ya urembo. Mashindano ya urembo yalianzishwa 1967, ikiwa ni miaka sita tangu nchi ipate Uhuru na mshindi wa kwanza alikuwa Theresa Shayo ambaye hata hivyo hakupata nafasi ya kuiwakilisha nchini katika shindano la kimataifa. Mwaka mmoja tu baadaye mashindano hayo yalipigwa marufuku.

Shindano hilo maarufu kwa sasa kama ‘Miss Tanzania’ lilirudi wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili baada ya kuruhusiwa tena 1994 na Aina Maeda akatwaa taji na kufuatiwa na mfululizo wa mashindano kuanzia ndani ya kitongoji. Mara baada ya kurejeshwa, mashindano hayo yalisimamiwa na Rhino International chini ya uongozi wa Hashim Lundenga ambaye aliyaendesha kwa miaka karibu 25 hadi waliponyang’anywa kutokana na mgogoro wa zawadi ya Diana Edward aliyekuwa Miss Tanzania 2016.

Wakati Theresa anashiriki shindano hilo halikuwa na mwonekano wa kitaifa kwani yalifanyika maeneo machache na fainali zake zilifanyika Hoteli ya Kilimanjaro (sasa ikifahamika kama Hyatt Regency). Katika kipindi chote cha kufanyika kwa shindano hilo, warembo 28 walipatikana baadhi yao wakijipatia umaarufu uliowawezesha kupata mikataba minono ya matangazo.

Baadhi ya warembo waliobeba taji la Miss Tanzania baada ya kurejea 1994 ni Aina Maeda (1994), Emily Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basila Mwanukuzi (1998), Hoyce Temu (1999) na Jacqueline Ntuyabaliwe (2000). Wengine ni Happiness Magese, Angela Damas, Sylvia Bahame, Faraja Kotta, Nancy Sumari, Wema Sepetu, Richa Adhia, Nasreen Karim, Miriam Gerald, Genevieve Emmanuel, Salha Israel, Lisa Jensen, Brigitte Alfred, Happiness Watimanywa, Lilian Kamazima, Diana Edward, Julitha Kabete, Queen Elizabeth Makune, Sylvia Sebastaian na Rose Manfere ambaye hivi karibuni alitangazwa kuvuliwa taji.

Mbali na Miss Tanzania pia sanaa ya urembo iliyochangia ajira za wasichana kadhaa nchini kulikuwa na Miss Utalii, Miss Universe, Face of Africa na mengine yaliyowaibua kina Miriam Odemba, Flavian Matata na wengine waliotamba kimataifa na kupata dili zilizowapa fedha.

Kwa sasa mashindano ya urembo yamepoteza mvuto wake ikilinganishwa na miaka ya nyuma. “Mwanzoni tulipata ugumu kwa vile jamii ilikuwa haikubali, lakini nashukuru ukiacha kuwa na viongozi waelewa, kwa kipaji cha kuchangamana na watu nilichojaliwa walinishika mkono,” anasema.

Lundenga anasema wakati akiwa ofisa katika Kiwanda cha Nguo cha Kilitex alijuana na watu mbalimbali ambao ndio walimsaidia.

Juu ya kilichotokea 2016 cha kushindwa kutoa zawadi hadi mshindi kushindwa kumkabidhi zawadi yake, ni kutokana na kupeleka mashindano hayo mjini Mwanza huku waliyempa kazi ya kukusanya kiingilio hakuwa mwaminifu na hivyo kujikuta wanakosa fedha ambazo walitegemea zingewawezesha kununua zawadi.

Akizungumzia mashindano ya sasa, anasema ni kama yamekosa hamasa na kuishauri serikali kumuunga mkono mwandaaji yarudi kama zamani.


Kutoka Dar Jazz hadi Twanga Pepeta

Mbali na sanaa ya urembo, sanaa ya muziki nayo ina historia kubwa katika Uhuru wa nchi kwani ulitumika katika kuhamasisha harakati za kuudai.

Historia inaonyesha kuwa muziki wa dansi ulianza miaka ya 1930, hasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, ikitajwa bendi ya Dar es Salaam Jazz iliyoanzishwa 1932 kisha kuibuka Cuban Marimba ya Salum Abdallah ‘SAY’ 1948 mjini Morogoro, halafu nyingine kama Morogoro Jazz, Tabora Jazz na nyinginezo zilizotamba.

Baada ya Uhuru zikaibuka bendi nyingine zilizoibua vipaji vilivyoibeba Tanzania kimataifa na kuchangia kuhamasisha shughuli za kisiasa, kijamii na nyanja nyingine kama Nuta Jazz ‘Msondo Ngoma’ iliyoanzishwa 1964, Vijana Jazz iliyoasisiwa 1971, DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ ya 1978 na nyinginezo.

Bendi hizo kongwe hadi sasa bado zipo zikiendelea na shughuli zao kama kawaida, ingawa sio kama ilivyokuwa zamani. Nuta Jazz ambayo imepitia majina kadhaa yakiwamo Juwata Jazz, OTTU Jazz kwa sasa ndio Msondo Ngoma Music Band wakati DDC Mlimani Park imeachana na neno DDC na kuwa Mlimani Park, huku Vijana ikibaki kama ilivyo.

Mbali na bendi hizo kongwe za muziki wa dansi, lakini Tanzania imeshuhudia mabadiliko makubwa katika miondoko hiyo, ikiwamo kuibuka bendi za dansi la kisasa lililoongeza uhamasishaji na ajira kwa vijana wengi wenye vipaji vya fani ya muziki.

African Stars ‘Twanga Pepeta’, FM Academia, Chuchu Sound, Pamo Sound, Akudo Impact, Diamond Musica, TOT Plus, Mchinga Sound, Double Sound, Extra Bongo na makundi mengine yaliendeleza muziki huo.

Kwa wanaokumbuka miaka ya 1970-2000, kumbi mbalimbali zilijipatia umaarufu kwa kutambulika kwa bendi zilizokuwa zikipiga kwenye kumbi hizo kama Lang’ata Social Hall, Vijana Hall, Safari Resort, White House Hall, Wapiwapi Bar Chang’ombe, Bahama Mama Club, DDC Magomeni Kondoa, DDC Kariakoo, DDC Keko, DDC Mlimani, Amana Social Hall, Max Bar, Lango la Jiji na nyinginezo kwa jijini Dar.

Kwa sasa dansi limezimika na halina nguvu kutokana na kuibuka kwa Bongo fleva, Singeli, Taarabu na mingine inayotamba kwa sasa.