Sherehe za Uhuru zaanza kupamba moto, Taifa laombewa

Muktasari:

  • Katika kufanikisha maandalizi ya uhuru, manispaa mbalimbali zilianza kuwasilisha michango yao kwenye kamati ya maandalizi ya sherehe hizo, huku Moshi ikitoa Paundi 250 na Tanga Paundi 233.

Katika kufanikisha maandalizi ya uhuru, manispaa mbalimbali zilianza kuwasilisha michango yao kwenye kamati ya maandalizi ya sherehe hizo, huku Moshi ikitoa Paundi 250 na Tanga Paundi 233.

Manispaa ya Moshi iliwasilisha mchango huo kwenye kamati ya fedha, iliyoundwa kwa ajili ya sherehe hizo. Kamati iliundwa na wajumbe wanne; Lukamoyo, Leshabari, Bennet na Bundeali.

Kwa upande wa Tanga, fedha walizochanga zilitokana na michango kutoka kwa watu binafsi, taasisi na kampuni mbalimbali.

Kampuni na taasisi hizo ni; Dalgety&Co (Paundi 100), Salim Aman (Paundi 20), European Bakery (Paundi 50), wafanyakazi wa Karimjee Jivanjee (Paundi 121), R.E.D Cluer (Paundi 100), Park Hotel (Paundi 50), Taibali Essajee Sachak Co Ltd (Paundi 50), Ralli Estate Ltd (Paundi 2,000), Karimjee Jivanjee Estates Ltd (Paundi 1,000), Chief Officers Tanga mjini (Paundi 400), Lehann’s (EA) Ltd (Paundi 100) na Saifee Ice & Aerated Water Factory (Paundi 21).

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard


Kanga, mashati na tai vyawasili

Katika kuelekea sherehe za uhuru, Chama cha Tanu kiliagiza kanga, tai na mashati kutoka Japan kwa ajili kugawa kwa wananchi ili vitumike kwenye sherehe za uhuru.

Vitu hivyo vilivyoagizwa kutoka Japan viliwasili Tanganyika na Tanu ikatangaza kwamba vitauzwa kwa wananchi, kupitia ofisi za matawi ya chama hicho yaliyopo maeneo mbalimbali nchini.

Taarifa iliyotolewa na Tanu ilisema: “Kanga, tai na mashati yaliyoagizwa kutoka Japan yamewasili Tanganyika mwishoni mwa Oktoba na yatauzwa kupitia ofisi za matawi ya chama kote nchini.”

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard


Nyerere, Kaunda na Kenyatta wafanya mkutano

Mkutano wa amani na umoja miongoni mwa Waafrika ulifanyika na viongozi watatu wenye ushawishi mkubwa, Julius Nyerere (Tanganyika), Jomo Kenyatta (Kenya) na Kenneth Kaunda (Northern Rhodesia) walihutubia umati wa watu wapatao 40,000 kwenye uwanja wa Kisumu, Kenya.

Nyerere aliuambia umati huo kuwa japokuwa Kenya iko mbele ya Tanganyika kwa mambo mengi, lakini nchi hiyo imezidiwa kwenye masuala ya kisiasa kutokana na kukosa umoja.

“Kama hakuna umoja utaendelea kupeperusha bendera ya wakoloni katika ardhi yako kwa muda mrefu,” alisema Nyerere.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Kenyatta alivionya vyama vya Kanu na Kadu na kuviambia kwamba mpaka vikiamua kuungana kwa amani, ndipo atatoa idhini ya kuanzisha chama cha tatu.

“Kama vyama hivi vikiweza kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja, kuna muda utafika nitafikiria kuanzisha chama kipya cha siasa,” alisema Kenyatta.

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard


Shinyanga yatangaza kuliombea Taifa

Ratiba ya maandalizi ya sherehe za uhuru Shinyanga iliyokuwa na matukio mbalimbali ya kuburudisha na maombi ilitangazwa kupitia kamati ya wilaya.

Ratiba hiyo ilionyesha kwamba siku ya mkesha wa uhuru kutakuwa na maombi ya umma, ambayo yangeongozwa na viongozi wa imani mbalimbali, yakifuatiwa na ngoma zitakazopigwa kwenye eneo la Aerodrome (uwanja wa ndege wa zamani uliopo nje ya mji).

Ngoma hizo zitasimama kwa muda kupigwa usiku sana, bendera ya ‘Union Jack’ na Umoja wa Mataifa zitashushwa na kupandishwa bendera mpya ya Taifa la Tanganyika, baada ya hapo ngoma zitachezwa mpaka asubuhi.

Siku yenyewe ya uhuru kutakuwa na mashindano ya michezo ya kikabila, michezo ya shule, maonyesho ya watoto pamoja na mashindano ya urembo. Iliaminika kwamba ifikapo jioni ya siku hiyo, bendi ya polisi kutoka Mwadui ingeburudisha.

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard.