Tanzania miaka 60: Julius Nyerere ahutubia Baraza la UN

Julius Nyerere ahutubia Baraza la UN

Muktasari:

  • Julai 1961, Waziri Mkuu wa Tanganyika, Julius Nyerere alikwenda nchini Marekani katika ziara ya kikazi akiambatana na viongozi mbalimbali wa Tanganyika.



Julai 1961, Waziri Mkuu wa Tanganyika, Julius Nyerere alikwenda nchini Marekani katika ziara ya kikazi akiambatana na viongozi mbalimbali wa Tanganyika.

Akiwa nchini humo, Julai 17 Nyerere alipata nafasi ya kulihutubia Baraza la Wadhamini la Umoja wa Mataifa.

Kwenye ziara hiyo Nyerere aliambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Nsilo Swai, Rais wa Umoja wa wafanyakazi wa Kiasia walioajiriwa kwenye Serikali ya Tanganyika, M.C Zachariah na Rais wa Chama cha Wafanyakazi wa Umma wa Kiasia nchini Tanganyika, P.K.G Nayar.

Viongozi hao wawili wa vyama vya wafanyakazi walipitisha pendekezo la kulitaka baraza hilo kuwahakikishia wafanyakazi wote wa Kiasia mafao kama wanayopewa wafanyakazi wa kutoka Ulaya, ambao walitarajiwa kupoteza ajira zao mara baada ya Tanganyika kuwa huru.


Nyerere akutana na Rais Kennedy

Mchana wa Julai 18, 1961 Nyerere alitembelea Ikulu ya Marekani iliyopo Washington kwa ajili kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais John Kennedy.

Mkutano huo ambao ulichukua zaidi ya saa moja, pamoja na mambo mengine ulihusisha majadiliano kuhusu Marekani kuisaidia Tanganyika fedha za kutekeleza mpango wake wa maendeleo wa miaka mitatu.

Baada ya mkutano huo taarifa zilitoka kwamba Rais Kennedy alikubali kuisaidia Tanganyika kufanikisha suala hilo na kuahidi kuwa nchi hiyo itatoa fedha ili kuongezea katika zile zilizotolewa na Uingereza kuiwezesha Tanganyika kutekeleza mpango wake wa maendeleo.

Baada ya mkutano huo, Nyerere aliwaambia waandishi wa habari kuwa ameridhishwa na kufurahishwa na majadiliano hayo na safari yake nzima ya kufika Ikulu ya Washington.

Nyerere aliondoka Marekani usiku wa Julai 18 kurudi Tanganyika kwa ajili ya kuendelea na harakati za uhuru.


Lwegarulila atetea heshima

Mwenyekiti wa Chama cha wanafunzi wa Tanganyika wanaosoma Uingereza, Fredrick Lwegarulila aliwataka Watanganyika waliopo kwenye nchi hiyo kufanya mambo yatakayoipa heshima Tanganyika wakati ikielekea kupata uhuru wake.

Lwegarulila aliyasema hayo wakati akitoa hotuba kwenye mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika jijini London Julai, 1961 na kuongeza kuwa kinachotazamwa zaidi ni tabia zao na si elimu yao.

“Katika muda mtakaokuwepo hapa, watu wengine watawatazama sana kwa mambo yenu mnayotenda kwa ajili ya Tanganyika na kwa namna mnavyoshika heshima ya nchi yenu,” alisema Lwegarulila.

Aliendelea kusema kuwa watu wa Tanganyika wanatega masikio ili kusikia kila kitu kinachofanywa na wanafunzi waliopo Uingereza.

“Baada ya Desemba 9, 1961 Watanganyika watakuwa raia wa Serikali mpya na kuwa wananchi wa Taifa jipya kabisa, hivyo wanafunzi mna wajibu wa kuunda msingi imara wa baadaye kwa kulinda heshima ya nchi yetu mbele ya macho ya ulimwengu,” alihitimisha Lwegarulila.


Wabunge Uingereza washinikiza msaada kifedha

Julai 27 kwenye Bunge la Uingereza kulizuka mabishano makali ambapo pande zote za Bunge ziliingia kwenye malumbano kuhusu Afrika ambapo Serikali ya nchi hiyo ilitangaza kwamba haingeongeza fedha za kuisaidia Tanganyika kutekeleza mpango wake wa kimaendeleo wa miaka mitatu.

Kiongozi wa zamani wa Tanganyika ambaye alikuwa moja ya wabunge wa Bunge hilo, Henry Clark alisema suala la Serikali ya Uingereza kukataa kuongeza fedha kwa ajili ya kumpatia Nyerere kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka mitatu wa Tanganyika utapunguza imani iliyonayo Tanganyika kwa Uingereza.

Clark alisema katibu wa makoloni ya Uingereza nchini Tanganyika, Ian Macleod atakasirishwa sana na kitendo hicho cha Serikali yake.

Clark alisema fedha hizo zinatakiwa kupatikana katika tarehe za mwanzo baada ya Tanganyika kujipatia uhuru wake ili iwe rahisi kwao kutekeleza mpango huo.

Msemaji wa wafanyakazi kwenye makoloni ya Uingereza, Mr Callaghan alisema kutoa fedha hizo kwa Tanganyika si kuifanyia fadhila bali inastahili kwa sababu fedha ilizovuna Uingereza kutokana na kilimo cha Katani na Kahawa ziliisaidia nchi hiyo kwenye kipindi kigumu, hivyo ni zamu yao kuipatia Tanganyika fedha.