Uhaba wa maji unaendelea kupungua siku hadi siku

Muktasari:

  • Miongo miwili iliyopita, katika barabara za Jiji la Dar es Salaam kulikuwa na mambo ya kushangaza. Miongoni mwa mambo hayo ni barabara kujaa magari yanayobeba maji yakienda kasi kupeleka kwa wateja mithili ya magari ya wagonjwa yanayowakimbiza hospitalini.

Haikuwa jambo la kushangaza katika maeneo mengi jijini Dar es Salaam, kukutana na magari, maarufu ‘bowsers’, yakiwa yamebeba madumu makubwa ya pembe nne yaliyojaa maji kwa ajili ya kusambaza kwa wateja.

Miaka 20 baadaye katika maeneo mengi hali imebadilika. Katika barabara ya Morogoro kuelekea Kimara ambako kulikuwa miongoni mwa maeneo ambayo yalikuwa na wingi wa magari ya kusambaza maji, sasa kuna mabadiliko makubwa si tu mabasi ya mwendo kasi yakisafiri kupita kwenye barabara zake maalumu, pia magari ya ‘bowsers’ ya wauza maji yameadimika.

Hata wakosoaji wakubwa wa hali ile hawakuwahi kufikiria kwamba kuna siku itafika ambapo shida za kudumu za upatikanaji wa maji jijini Dar es Salaam zitakuwa ni historia.

Matatizo ya usambazaji wa maji yanaweza kuchukua muda mrefu kushughulikiwa. Ukweli ni kwamba jiji halijafikia asilimia 100 ya upatikanaji maji. Yaani hayajaanza kupatikana saa 24, kwa siku saba za wiki mwaka mzima, maeneo kama ya viwanda, hospitali bado wanalalamika kuwa usambazaji wa maji kwa mgawo unaathiri shughuli zao.

Lakini jiji la Dar es Salaam linapofikisha umri wa miaka 60 mwaka huu, ni vyema kutafakari juu ya safari ndefu na ngumu ambayo viongozi wa jiji wamesafiri ili kufanikisha usambazaji maji kwenye wakazi wake wanaokadiriwa kuzidi milioni tano. Dar es Salaam ilipata hadhi ya jiji Desemba 9, 1961.

Ugavi wa maji kabla ya uhuru

Mfumo rasmi wa kwanza wa usambazaji maji jijini Dar es Salaam ulianzishwa na Serikali ya kikoloni kwa mara ya kwanza mwaka 1951, ikiwa ni miaka kumi kabla ya Uhuru. Kiwanda cha kutibu maji cha Mtoni (The Mtoni Water) kilipewa kazi ya kusambaza maji sehemu za kusini mashariki mwa jiji kama vile Chang’ombe na Kurasini pamoja na maeneo ya kibiashara ya Dar es Salaam. Mtambo wa Mtoni ulikuwa ukipata maji kutoka mito ya Bonde la Kizinga na Mzinga.

Kulingana na masimulizi tofauti ya kihistoria, mtandao wa mabomba ya maji ulikuwa umeandaliwa katikati mwa jiji tangu miaka ya 1920 na 1930 kuchukua maji kutoka mtambo wa kutibu maji wa Gerezani. Hii baadaye ilitelekezwa kwa sababu ya chumvi nyingi iliyokuwa kwenye maji hayo. Nyongeza ilifanyika katika miaka ya 1950 baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa usambazaji maji wa Mtoni.

Miaka minane baadaye, mwaka 1959, mtambo wa kutibu maji wa Ruvu Juu wenye uwezo wa kusukuma mita za ujazo 18,000 kwa siku ulianza kufanya kazi. Mwaka 1975 mtambo wa Ruvu Chini ulipewa uwezo kusukuma mita za ujazo 180,000 kwa siku.

Mamlaka ya usambazaji maji

Baada ya uhuru, usambazaji maji Dar es Salaam ulisimamiwa moja kwa moja na Serikali Kuu kupitia idara ya Ugavi wa Maji Dar es Salaam. Mwaka 1977 idara hiyo ikawa shirika la Serikali na likapewa jina la ‘Dar es Salaam Water Supply Cooperation Sole’.

Jambo kuu lilikuwa kulifanya shirika lijitegemee kifedha na kiutawala. Shirika hili halikufanya vyema katika utendaji wake na mwaka 1984 taasisi mpya, National Urban Water Authority (Nuwa) ilianza shughuli zake.

Hapo awali Nuwa ilikusudiwa kuwa mamlaka moja kubwa ya maji yenye jukumu la kusimamia usambazaji wa maji katika vituo vyote vya miji Tanzania Bara. Hiyo ikawa kazi ngumu na Nuwa ikaendelea kubaki kusimamia usambazaji maji Dar es Salaam pekee.

Wakati mji ulipoanza kupanuka hadi kuelekea mwishoni mwa miaka ya 1980, kidogo kidogo usambazaji wa maji ulianza kuwa mgogoro.

Huu pia ulikuwa ndio wakati ambao Tanzania ilikuwa ikikumbwa na hali mbaya ya kiuchumi ya muda mrefu iliyoanza mwishoni mwa miaka ya 1970, iliyochochewa na vita ya Kagera na kuendelea hadi miaka ya 1980.

Mgogoro huo, ukichochewa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni na ukosefu wa bidhaa muhimu, Serikali ilishindwa kupata vipuri vya kutengeneza mitambo ya mfumo wa maji, achilia mbali kupanua mfumo uliokuwapo.

Kupanuka kwa kasi kwa jiji la Dar es Salaam na shida ya uchumi vilifuta mafanikio yaliyokuwa yamepatikana kutokana na mfumo wa usambazaji maji katika Tanzania ya miaka ya 1970.


Dawasa yaanzishwa

Mwaka 1997 Serikali iliipanga upya Nuwa na kuiongeza kazi za maji taka na usafi zilizokuwa zikitekelezwa na Tume ya Jiji na kuunda Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa).

Mamlaka ya Dawasa iliongezwa kwenye miji ya pembeni kama Kibaha na Bagamoyo mwaka 2001. Mabadiliko ya Nuwa kuwa Dawasa hayakuboresha sana hali iliyokuwapo awali. Uhaba wa fedha uliifanya Dawasa ishindwe kurekebisha miundombinu na kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya watu wa jiji. Wakazi wa jiji waliendelea kutumia muda mwingi na fedha kununua maji kutoka kwa wachuuzi wa huduma hiyo.

Mwaka 2003, katikati ya wimbi la ubinafsishaji nchini, usambazaji wa maji jijini ulibinafsishwa. Jumuiya ya wawekezaji kutoka Uingereza, Ujerumani na Tanzania iliingia kandarasi ya kusambaza maji.

Hata hivyo, miaka miwili baadaye baada ya biashara hii kuthibitika kuwa haikufaulu, kampuni mpya iliyoitwa City Water Services (CWS) iliundwa na kuanza kufanya kazi Agosti 2003.

Katika mpangilio huo Dawasa alibaki kama mmiliki wa miundombinu na City Water kama mpangaji ambaye alipaswa kulipa ada ya pango. Mei 2005 Serikali ilisitisha mkataba wa City Water kutokana na mwekezaji kushindwa kuboresha huduma na kwa kuvunja sheria na masharti ya mkataba. Julai 2005, kampuni mpya, Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) ilianzishwa na ikapewa mkataba wa miaka kumi na Serikali kusambaza maji. Dawasco ilitakiwa kulipa ada kwa Dawasa. Licha ya gharama kubwa za kiutendaji, uhaba wa fedha za kutosha kurekebisha miundombinu ya maji iliyochakaa, Dawasco ilileta maendeleo makubwa katika kuboresha na kupanua usambazaji wa maji Dar es Salaam.

Mwaka 2015 mkataba wa Dawasco uliongezwa kwa miaka mitatu hadi 2018 kuiruhusu Serikali kuunganisha huduma hizo mbili. Septemba 2018, Dawasa na Dawasco waliungana na kuendelea kufanya kazi na majukumu yake chini ya Sheria ya Dawasa namba 20 ya 2001. Mwaka 2019 chombo hiki kilichounganishwa kikaitwa Dawasa na kilianza kufanya kazi chini ya Sheria ya Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira namba 5 ya 2019. Tangazo la Serikali namba 660/2019 lilipanua mamlaka ya Dawasa hadi wilayani Kisarawe na Mkuranga mkoani Pwani na mamlaka zilizokuwa katika miji hiyo zilifutwa.