Uhitaji wataalamu wa sekta ya utalii

Muktasari:

  • Habari za maendeleo ya rasilimali watu katika sekta ya utalii nchini Tanzania, zinaenda sambamba na mwelekeo wa sera za utalii tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi.

Habari za maendeleo ya rasilimali watu katika sekta ya utalii nchini Tanzania, zinaenda sambamba na mwelekeo wa sera za utalii tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi.

Baada ya uhuru Serikali haikutilia mkazo sana utalii kama shughuli ya biashara ambayo ingesaidia kuijazia hazina ya Serikali, kutengeneza ajira na kupunguza umaskini.

Ingawa watalii waliruhusiwa kuingia nchini na hoteli nyingine zilijengwa katika mbuga za kitaifa, hakukuwa na juhudi zozote za makusudi za kuitangaza Tanzania kama mahali pa kuchagua kwenda.

Utalii wa kutia moyo ulionekana kuwa unategemea wageni kukuza uchumi, jambo ambalo lilikuwa kinyume cha sera ya Ujamaa na Kujitegemea.

Kwa sababu ya sera hii, hakuna juhudi zilizofanywa kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu. Matokeo yake uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi likawa ni suala kubwa ambalo bado linasumbua sekta ya utalii hata wakati huu ambao Tanzania inatimiza miaka 60 tangu ipate uhuru.

Ripoti ya hivi karibuni ya utafiti inaonyesha kuwa asilimia 28 ya wafanyakazi wote katika nafasi za usimamizi kwenye sekta ya utalii ni wageni.

“Idadi ya wafanyakazi wa kigeni ni sawa na asilimia 28 ya wafanyakazi wote kwenye ngazi ya usimamizi, jambo linaloashiria kuwa kukosekana kwa ujuzi na uzoefu unaohitajika kwa wafanyakazi wa ndani ndiko kunawazuia kupewa majukumu ya juu katika taasisi,” inasema sehemu ya ripoti yenye kichwa ‘ Demand and Supply of Skills in the Tourism and Hospitality Sector in Tanzania’ iliyotolewa na Profesa Wineaster Anderson wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuchapishwa mwaka 2016.

“Utalii ni kazi ngumu na kubwa na inaajiri idadi kubwa ya wanawake na vijana,” anaongeza Profesa Anderson katika ripoti hiyo.

Uwezo wa sekta ya utalii kutengeneza ajira kwa watu wengi na kumaliza umaskini hauna kikomo. Mwaka 2014 takriban watu milioni 1.2 waliajiriwa katika sekta ya utalii, na 500,000 kati yao kwa ajira za moja kwa moja. Hiyo ni kulingana na hotuba ya bajeti ya mwaka 2015/16 ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kufikia mwaka 2019, ajira za moja kwa moja ziliongezeka na kufikia 850,000. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia iliyoitwa ‘Transforming Tourism: Towards a Sustainable, Resilient and Inclusive Sector’ iliyotolewa Julai 2021. Lakini ajira hizo hatimaye zilianguka kutokana na janga la Uviko-19.

Licha ya uwezekano wa waajiri kuajiri zaidi, bado hawawezi kupata wafanyakazi wenye ujuzi sahihi wa kujaza maelfu ya nafasi zilizopo.

Ikumbukwe kwamba taasisi za mafunzo nchini Tanzania hazijatoa mipango yoyote ya usimamizi iliyowekwa kwa ajili ya utalii. Hii inadokeza ni kwa nini kampuni nyingi za utalii zimechagua kuajiri watu kutoka nje ya nchi katika nafasi za usimamizi.

Taasisi za elimu ya juu zilianza kutoa shahada katika kozi zinazohusiana na utalii mwaka 2000, hiyo ikiwa ni karibu miaka 40 baada ya uhuru.

Kulingana na Profesa Anderson, Chuo Kikuu cha Tumaini (TU) kilianzisha programu ya shahada katika ‘anthropolojia’ (elimu ya binadamu, hasa elimu ya habari zinazohusu asili na maendeleo yake ya awali).

Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ilianzisha kozi za Shahada ya Biashara katika Utalii na Usimamizi mwaka 2008. Baadaye Kitivo cha Jiografia cha UDSM pia kilianzisha kozi ya Stashahada katika Utalii wa Kitamaduni.

Kulingana na Dk Florian George Mtey, Mkurugenzi wa Mafunzo na Shughuli za Kitaaluma katika Chuo cha Kitaifa cha Utalii (NCT), leo kuna chuo kinachotoa kozi ya shahada katika Usimamizi wa Hoteli.

Anasema NCT tayari imeunda mtalaa wa kozi za shahada ya usimamizi wa hoteli kujaza pengo lililopo.

Nchini Tanzania mafunzo ya ustadi wa utalii yanasimamiwa na mamlaka tatu; Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ambayo ina jukumu la kuratibu na kudhibiti elimu ya vyuo vikuu; Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), ambayo ina jukumu la kuratibu, kudhibiti, kufadhili, kutoa na kukuza elimu ya ufundi; Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), ambalo lina jukumu la kuratibu, kudhibiti na kuidhinisha taasisi za kiufundi.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa kuna taasisi 116 zilizosajiliwa zinazotoa mafunzo ya utalii nchini Tanzania kuanzia cheti hadi shahada ya uzamili, na vina uwezo wa kuandikisha wanafunzi 12,659 kila mwaka. Asilimia 11 ni vyuo vikuu, asilimia 29 ni vyuo vya ufundi na asilimia 60 ni taasisi za ufundi.

“Ni muhimu pia kutambua kuwa nyingi (karibu asilimia 75) za taasisi za mafunzo ya kiwango cha chini cha utalii nchini zinamilikiwa na watu binafsi.

Kwa bahati mbaya, wengi wao hawana vifaa vyote kulingana na vifaa vya mafunzo, mikataba ya mafunzo, mikataba na wafanyakazi kiasi kwamba wanashindwa kuzalisha wahitimu walio na ujuzi unaohitajiwa sana na sekta ya utalii,” Profesa Anderson anaandika katika utafiti wake.

Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Allan Kijazi anakiri kuwa uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi katika sekta ya utalii bado ni tatizo kubwa, lakini anasema juhudi zinafanywa na maendeleo mengi yamepatikana kutatua tatizo hilo. Anasema kuanzishwa kwa Chuo cha Taifa cha Utalii na vyuo vyake vya Arusha na Mwanza ni sehemu ya juhudi hizo.

“Tunashughulikia mipango ya kuongeza ushirikiano na taasisi kutoka ng’ambo nchini Italia na Uswizi ili kukuza ujuzi wa utalii,” Dk Kijazi anasema.

Profesa Anderson, ambaye amefanya utafiti wa kina juu ya ukuzaji wa ujuzi katika sekta ya utalii, anasema juhudi za kuboresha mafunzo katika sekta hiyo zinapaswa kwenda sambamba na kuongeza mishahara.

“Utafiti uliofanyiwa waajiri unaonyesha kwa mapana kwamba sekta ya utalii inajulikana sana kwa kuwalipa wafanyakazi mishahara midogo ... hii inaweza kuwavunja watu moyo,’’ anaeleza.

Mafunzo ya utalii nchini Tanzania yalianza miaka ya 1960 wakati ‘Hallmark Hotels Ltd’ inayomilikiwa na Waingereza ilipoanzisha kituo cha mafunzo ya hoteli kilichoitwa ‘Tanzania Hotel School’ kutoa ujuzi wa kimsingi katika shughuli za ofisi, kutunza nyumba na usafi, mapishi ya chakula na mbinu za uandaaji vinywaji.

Mwaka 1969 kituo hicho cha mafunzo kilitaifishwa na Serikali na jina lake likabadilishwa na kuitwa Taasisi ya Mafunzo ya Hoteli na Utalii (HTTI--Hotel & Tourism Training Institute) na kukabidhiwa kwa Shirika la Utalii Tanzania (TTC).

Mwaka 1977 taasisi hiyo ilikabidhiwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii. Mwaka 2003 kituo hicho kilipewa jina Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT).