Chuo cha Maji kinaandaa wataalamu wa maji kwa ajili ya ustawi wa Taifa


CHUO PICS

Maji ni kimiminika muhimu na kiini cha uhai wa viumbe hai wote duniani. Hakuna kiumbe hai anayeweza kuishi bila maji, hata miili ya wanyama na mimea pia kwa kiasi kikubwa ni maji. Katika dunia...

Maji ni kimiminika muhimu na kiini cha uhai wa viumbe hai wote duniani. Hakuna kiumbe hai anayeweza kuishi bila maji, hata miili ya wanyama na mimea pia kwa kiasi kikubwa ni maji. Katika dunia, maji yamechukua karibu robo tatu ya eneo lake lote, kwa hiyo maji ni kitu cha msingi sana.

Mbali na umuhimu huu wa maji kwa viumbe hai walioko juu ya uso wa dunia, maji pia hutumika katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kama vile shughuli za viwanda. Ni sahihi kwamba maji yana umuhimu mkubwa kwa viumbe hai duniani lakini pia maji ni taaluma pana na muhimu ambayo mtu hukaa darasani na kwa miaka kadhaa ili kuipata.

Wengi tunafahamu kwamba utoaji wa huduma za maji unaishia tu kwenye ufungaji wa mabomba, uchimbaji wa visima na usomaji wa mita za maji, lakini uhalisia sio huo bali utoaji wa huduma za maji unasimamiwa na taaluma pana ambayo inahusisha mambo mengi yanayosaidia upatikanaji wa rasilimali maji yenye ubora na inayozingatia afya za viumbe hai.

Hapa nchini taaluma hiyo inatolewa na Chuo cha Maji. hii ni Taasisi ambayo inaten-geneza na kutoa wataalamu wanaotumika katika sekta ya maji. Mkuu wa Chuo cha Maji, Dkt. Adam Karia anasema Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1974 ikiitwa “Water Resources Institute” na ikiwa na jukumu la kuzalisha wataalam wa kada ya kati (middle level) kwa ajili ya kwenda kufanya kazi katika sekta ya maji.

“Mwaka 1980, Chuo kilibadilishwa jina kutoka Water Resources Institute na kuwa Chuo cha Maji Rwegarulila kwa ajili ya kuenzi mchango wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Fredrick Rwegarulila katika uanzishwaji wa chuo hicho,” anasema Dkt. Karia.

Dkt. Karia anasema, mwaka 2008 katika maboresho ya sekta ya umma ambayo yalikuwa yanaratibiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Chuo kilibadilishwa na kuwa Wakala wa Serikali kwa Sheria ya Wakala na kupewa jina la Chuo cha Maendeleo na Usimamizi wa Maji (WDMI), “Baada ya kuwa wakala Chuo kiliongezewa majukumu mapya mawili, nayo ni kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam na kufanya Chuo hiki kuwa na majukumu makuu matatu (mafunzo, tafiti na ushauri wa kitaalamu),” anasema Dkt. Karia.

Hata hivyo mnamo mwaka 2016, Chuo kilibadilishwa tena jina na kuitwa Chuo cha Maji, huku majukumu yake ya Wakala wa Serikali yakibakia kama awali. Dkt. Karia anasema, Chuo cha Maji kipo chini ya Wizara ya Maji na porogramu zake za mafunzo zimepewa ithibati na Baraza la Taifa la Ufundi (NACTE) na Tume ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Chuo kilipandishwa hadhi kuwa moja ya Taasisi za elimu ya juu mwaka 2012 na kuanza kutoa mafunzo katika ngazi ya shahada ya kwanza mwaka 2013.

“Tangu kipindi hicho Chuo cha Maji kimeendelea kutoa mafunzo bora kwa kuanzia ngazi ya Astashahada, Stasha-hada mpaka Shahada ya kwanza. Chuo kinatoa elimu inayozingatia ubora kwa mhitimu ili baada ya kuhitimu mafunzo hayo awe ameiva na mwenye uwezo unaolingana na kozi aliyoisomea,” Dkt. Karia anasema kwa sasa Chuo cha Maji kinatoa mafunzo, ushauri wa kitaalam na utafiti na programu zitolewazo na chuo ni Stashahada za Uhandisi wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira (Water Supply and Sanitation Engineering) na Haidrojiolojia na Uchimbaji wa Visima (Hydrogeology and Water Well Drilling).

“Kozi nyingine ni Haidrolojia na Hali ya Hewa (Hydrology and Meteorology), Teknolojia ya Maabara ya Ubora wa Maji (Water Quality Laboratory Technology) na Uhandisi wa Umwagiliaji (Irrigation Engineering).” Pia Shahada ya Kwanza katika Uhandisi wa Rasilimali za Maji na Umwagiliaji (Bachelor Degree in Water Resources and Irrigation Engineering), Chuo kinatarajia hivi karibuni kuanza kutoa mafunzo katika ngazi ya Shahada ya pili. Anasema, kadhalika Chuo kinatoa kozi za muda mfupi ili kuwawezesha wafanyakazi kujiendeleza wawapo kazini kwa ufanisi zaidi na weledi.

Kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi

Dkt. Karia anasema, Chuo baada ya kubadilishwa kuwa wakala mwaka 2008 kimekuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha udahili wa wanafunzi. Mwaka 2008 chuo kilikuwa na wanafunzi wasiozidi 300 na sasa udahili umeongezeka na chuo kina wanafunzi wapatao takribani 2,300. “Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano kuna maendeleo makubwa katika Chuo ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya maabara za Chuo. Jambo hili limefanya wahitimu kuongezeka kwa sababu mwaka uliopita chuo kilifanikiwa kutoa wahitimu zaidi ya 680 idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na miaka iliyopita,” anasema Dkt. Karia.

Nafasi ya chuo kusaidia utekelezaji miradi ya maji

Serikali ya Awamu ya Tano tangu iingie madarakani imekuwa ikitekeleza miradi mingi ya maji kwa lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa maji safi na salama nchini. Kutokana na jambo hilo, Chuo cha Maji kimekuwa kikizalisha wataalamu ambao wanasaidia katika utekelezaji wa miradi hiyo. Anasema, kutokana na hitaji hilo, kwa sasa Chuo cha Maji kinatoa wataalamu wa sekta ya maji katika kada ya ufundi sanifu na uhandisi wa maji.

“Ili kuhakikisha kwamba Chuo cha Maji kinaendelea kuwa na uwezo wa kuzalisha wataalamu wakaosaidia kuboresha sekta ya maji, Serikali ya Awamu ya Tano imetoa fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa majengo yote ya Chuo ukiondoa mabweni tu. Ukarabati huo utafanya majengo yote ya chuo kuwa ya ghorofa moja,” huu ni ukarabati wa kihistoria ambao haujawahi kufanyika kwa kiwango hicho tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mnamo mwaka 1974. Hivyo shukrani kubwa zimuendee Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli bila kuwasahau viongozi wakuu wa Wizara ya Maji nikianza na Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Katibu Mkuu, Prof. Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga,” anasema Dkt. Karia.

Utendaji wa Chuo katika maeneo matatu ya kimkakati (mafunzo, tafiti na ushauri) Mafunzo

Dkt. Karia anasema, “Katika kutoa mafunzo, chuo kwa kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano kumefanyika uwekezaji mkubwa katika uboreshaji wa Karakana, Madarasa na maabara jambo lililosababisha kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa pamoja na wanaohitimu, ambapo katika kipindi cha miaka mitano chuo kimekuwa na ongezeko la asilimia 75 ya wanafunzi wanaodahiliwa kwa mwaka hadi kufikia mwaka 2019.”

Anasema, miongoni mwa uwekezaji huo ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya maabara zote za Chuo ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa mafunzo ya vitendo. Pia maboresho makubwa ya majengo ya chuo ambayo wanatarajia kuyafanya hivi karibuni na kutoa kozi fupi zaidi ya 47 ambazo zinasaidia kutoa mafunzo kwa watu zaidi ya 1,500. Chuo pia kimeongeza idadi ya walimu kutoka walimu 30 na sasa chuo kina walimu zaidi ya 62.

Utafiti

Dkt. Karia anaeleza kuwa, kwa upande wa utafiti, Chuo cha Maji kimefanikiwa kufanya tafiti nyingi na moja ya tafiti hizo ni ile tuliyofanya hivi karibuni kuhusu upungufu wa maji kwenye mto Ruaha. “Tafiti nyingine kubwa tuliyoifanya ni ile ya kuangalia maendeleo ya mamlaka za maji ili mamlaka hizo ziweze kuwa endelevu na kutoa huduma zinazotakiwa. Tafiti hizi na nyingine tulizofanya machapisho yake yako tayari na yanapatikana katika majarida ya kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kujifunza,” anasema Dkt. Karia.

Ushauri wa kitaalamu

Dkt. Karia anasema, chuo kimefanya huduma nyingi za ushauri wa kitaalamu kwenye mambo ya maji na sasa chuo kimechukua miradi mitatu katika Kanda ya Mashariki na Pwani, ambapo mradi mmoja uko Pangani (Tanga) na miwili iko Pwani ili kusaidia kutoa ushauri wa kuifanikisha miradi hiyo ambayo hapo awali haikuweza kufanya kazi vizuri kama ilivyotarajiwa.

Umuhimu wa Chuo katika kufikia Mapinduzi ya Kiuchumi

“Taaluma ya maji ina umuhimu mkubwa katika ustawi wa taifa hili kwa saba-bu wataalamu wa maji ndiyo nguzo katika upatikanaji wa huduma bora za maji. Bila taaluma ya maji, upatikanaji wa huduma bora za maji safi ni ndoto ya mchana,” anasema Dkt. Karia.

Dkt. Karia anasema, ili kufikia malengo ya kiuchumi na hususan uchumi wa viwanda ambao ni ndoto ya Serikali ya Awamu ya Tano, upatikanaji wa huduma bora za maji ni jambo lisiloepukika na upatikanaji wa huduma hizi unatokana na uwepo wa wataalamu wa kutosha.

“Hivyo, nadiriki kutamka kwamba, Chuo cha Maji kina umuhimu mkubwa katika kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa viwanda kwa sababu bila maji hakuna viwanda na bila wataalamu wa maji hakuna maji yatakayofika viwandani. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia zaidi ya 75 ya wataalamu waliopo kwenye sekta ya maji hapa nchini wametoka kwenye chuo hiki,” anasema Dkt. Karia. “Kutokana na hilo, niwasihi vijana kutumia fursa ya Chuo cha Maji ili kupata taaluma ya maji kwa sababu kwa sasa Sekta ya Maji ina upungufu wa wataalamu wa maji takribani 2,020” anasema Dkt. Karia.

Namna Chuo cha Maji kinavyoadhimisha siku ya Maji Duniani

“Katika kuadhimisha siku ya maji mwaka huu, Chuo kinatarajia kuwa na program maalumu ya kutembelea baadhi ya shule katika jiji la Dar es Salaam kuzungumza na wanafunzi wa kike kuhusu umuhimu wa masomo ya sayansi ili wanapomaliza shule za sekondari waweze kujiunga na Chuo cha Maji ili kuwa na wataalamu wa kike katika sekta ya maji,” anasema Dkt. Karia.

Anasema, “Tutakuwa na maonyesho mbalimbali ya huduma zetu, tutashiriki katika uwasilishaji wa mada mbalimbali, tutafanya uzinduzi wa matawi mapya ya Chuo ambayo tunatarajia kuyazindua kwenye mikoa ya Mwanza na Singida na tutazindua jarida jipya linalohusu masuala mbalimbali ya maji ambalo limeandaliwa na wasomi na wataalamu waliobobea katika taaluma ya maji.”

Mambo ambayo Chuo kinajivunia

“Tunajivunia kuendelea kuwepo na kutoa wataalamu wanaosaidia kuboresha sekta ya maji. Pia tunajivunia kukua kwa sekta ya maji pamoja na kuboreka kwa huduma za maji,” anasema Dkt. Karia. Anasema, “Tunajivunia ushirikiano tunaoupata kutoka serikalini hususan kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa Wizara ya Maji na wafanyakazi wote wa Chuo cha Maji ambao kwa pamoja wamehakikisha kuwa chuo kinazalisha wataalamu wa kutosha ili kuboresha sek-ta ya maji nchini.”

Chuo cha Maji katika kuisaidia jamii

“Katika juhudi za kuisaidia jamii, Chuo cha Maji kwa kushirikiana na Wizara na wadau mbalimbali pamoja na Shirika la Kijerumani (GiZ) kulianzishwa Mfuko wa Mafundi Sanifu wa Maji. Mfuko huu ulianzishwa kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu, wakiwamo yatima ili waweze kumudu gharama za mafunzo,” anasema Dkt. Karia.

Na kuongeza kuwa, “Kipaumbele katika mfuko huo hutolewa kwa wanafunzi wa kike wanaotoka katika mazingira magumu kwa sababu kada ya mafundi sanifu haipo katika orodha ya program zinazowezesha wanafunzi kuomba mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.” Maji ni muhimu lakini taaluma ya maji ni muhimu zaidi kwa sababu hii ndiyo inafan-ya nchi iendelee au isiendelee na maji huonekana mazuri pale yanapopata utunzaji na usimamizi mzuri, maji yasiposimamiwa na kutunzwa vizuri husababisha madhara makubwa kwa afya za viumbe hai ikiwemo binadamu hivyo kufanya taifa kukosa nguvu kazi iliyo na afya bora. Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi na za aina mbalimbali za maji iki-wemo mito, maziwa, maeneo chepechepe na chemchemi zinazozalisha maji, hivyo ili rasilimali hizi ziweze kutumika vizuri zinahitaji wataalamu wa kuzisimamia na wataalamu hawa wanapatikana Chuo cha Maji.