Benki ya CRDB, CRDB Bank Foundation na Proparco zashirikiana kupigia chapuo nishati safi za kupikia

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (wa kwanza kushoto)  akizungumza wakati wa mkutano na viongozi waandamizi wa Shirika la Proparco la nchini Ufaransa wakiongozwa na Mkuu wa Taasisi za Fedha wa shirika hilo, Gonzague Monreal wakati wa majadiliano juu ya ushirikiano wao katika nishati safi za kupikia. Kushoto kwake ni Mkurugnezi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, Joseph Maji, Mkuu wa Kitengo cha Hazina na Kenneth Kaisigila, Mkuu wa Kitengo cha Mipango na Sera ya Mabadilijo ya Tabianchi.

Paris, Ufaransa. Benki ya CRDB, CRDB Bank Foundation na kampuni ya Proparco yenye maskani yake jijini Paris, Ufaransa, zimefanya mazungumzo leo hii ya kuingia makubaliano ya kuwezesha wanawake na vijana wajasiriamali na kampuni changa zilizopo Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), maeneo ambayo benki hiyo inaendesha shughuli zake.

Katika kutekeleza azma ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya dunia nzima, taasisi hizo, kwa pamoja zilijadili uhitaji wa kujumuisha masuala ya uchangiaji fedha za uhimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi katika ushirikiano wao, wakijikita zaidi katika ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya nishati safi za kupikia.

Hii ni pamoja na uwekezaji katika uendelezaji wa kampuni kubwa na zile changa na kusambaza teknolojia za nishati safi za kupikia ili kuongeza ufanisi wa shughuli zao.

Inaelezwa kuwa pamoja na mambo mengine, jitihada za kuwawezesha wanawake wajasiriamali na majiko banifu na kuwajengea uwezo wa matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati safi za kupikia zilijadiliwa.

Mbali na hilo, ilionekana kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea uwezo wa matumizi yenye tija ya teknolojia za nishati safi na uendeshaji wa biashara endelevu, huku CRDB Bank Foundation ikiwa na jukumu mama la kusimamia jambo hili.

Mkuu wa Taasisi za Fedha wa Proparco, Gonzague Monreal (wa pili kushoto) akizugumza wakati wa majadiliano juu ya ushirikiano wao katika nishati safi za kupikia na ujumbe wa Benki ya CRDB na CRDB Bank Foundation.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameonyesha kufurahishwa na hatua hii ya ushirikiano na Proparco inayolenga kusaidia kundi la wajasiriamali barani Afrika.

“Mazungumzo yetu na Proparco yanaakisi utayari wetu wa kukuza ujasiriamali na maendeleo endelevu barani Afrika. Kwa kuunganisha nguvu, tunaweza kuacha alama katika maisha ya vijana na wanawake wajasiriamali wengi,” anadokeza Nsekela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesisitiza faida zilizopo za ushirikiano huo ambao ni msingi wa upanuzi wa shughuli zao katika maeneo mengine.

“Ushirikiano huu utatusaidia kupanua wigo wa programu yetu ya IMBEJU, tukilenga kufikia idadi ya vijana na wanawake wajasiriamali milioni 1.

Pia, tumefurahishwa na hatua ya kujumuisha masuala ya nishati safi za kupikia katika ushirikiano huu; kwa kuwa hii itakwenda kuleta matokeo bora ya afya zao na kuchangia katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi,” anasema.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, Programu ya IMBEJU imekuwa na matokeo makubwa ikiwamo kufikia zaidi ya biashara changa 300,000 za wanawake na vijana.

Mitaji wezeshi yenye thamani ya zaidi ya Sh7 bilioni imegawiwa kusaidia shughuli za ujasiriamali, Programu hiyo imekuwa na tija kubwa ikisaidia pia kukuza matumimizi ya nishati safi za kupikia.

Mkuu wa Taasisi za Fedha za Proparco, Gonzague Monreal ameipongeza Benki ya CRDB kama moja ya washirika wa thamani katika uwezeshaji kiuchumi hususan wanawake na vijana wajasiriamali.

Ujumbe wa Benki ya CRDB na CRDB Bank Foundation (kushoto) na ule wa Proparco (kulia) katika picha ya pamoja baada ya majadiliano juu ya ushirikiano wao katika nishati safi za kupikia.

“Tunajivunia kuingia katika ushirikiano huu mpya kupitia CRDB Bank Foundation, ambao utaimarisha msaada wa kiufundi kwa wajasiriamali.

Proparco imejipanga thabiti kusaidia jitihada zote zinazohusu ukuzaji ukuaji jumuishi,” anabainisha Monreal, akisisitiza utayari wao wa kutafuta masoko mapya na kuipongeza benki hiyo na upanuzi wake huko DRC.

Ushirikiano wa Benki ya CRDB na Proparco umekuwa wa mafanikio makubwa hususan katika ukuzaji wa ujasiriamali nchini.

Mwaka 2022, benki hiyo ilipata mkopo wa jumla ya Sh182 bilioni kutoka kwa Proparco, ikiwa ni sehemu ya kuimairisha uwezo wa kimsaada kwa wajasiriamali, hususan zile zinazoongozwa na wanawake na zile zilizoathiriwa na Uviko-19.

Hivi karibuni, taasisi hizo mbili zimesaini mkataba wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 125 wa mikopo ambayo itagawiwa mwaka huu.

Benki ya CRDB ni miongoni mwa wadau wakuu waliohudhuria Mkutano wa Nishati Safi za Kupikia kwa Afrika uliofanyika Paris, Ufaransa.

Mkutano huo ulioendeshwa kwa pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Støre.

Mkutano huo huwakutanisha pamoja viongozi wa dunia kujadili masuala ya nishati safi na maendeleo katika jitihada za kukabiliana na changamoto zilizopo barani Afrika na kutafuta masuluhisho endelevu.