Benki ya CRDB na miaka minne ya huduma bora za wakala wa benkibima nchini
Dar es Salaam. Benki ya CRDB, mwaka huu, inasherehekea miaka minne ya utoaji huduma za wakala benkibima tangu ilipopatiwa leseni na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) mwaka 2021.
Benki ya CRDB ni miongoni mwa benki chache za mwanzo kupata kibali cha kutoa huduma za wakala benkibima, ila ina historia ya kutoa huduma hii kama dalali wa bima kwa zaidi ya miaka 10.
Benki ilibadili mfumo wa kutoa huduma za bima kama dalali hadi kuwa na dawati maalumu la benki wakala bima kufuatia mabadiliko ya kisheria ya mwaka 2019 ambayo yalizaa huduma za wakala benkibima ikiwa na maudhui ya kuongeza wigo na upatikanaji wa huduma hizi kwa kila Mtanzania, kwa urahisi na uhakika.
Benki ya CRDB inajivunia kufanya kazi na kampuni za bima 11 nchini, kampuni 10 za bima zikiwa za Tanzania Bara na Februari mwaka huu, iliongeza huduma ya ‘Takaful’ kupitia kampuni Tanzu ya Shirika la Bima Zanzibar (ZIC Takaful) ambayo inaruhusu utoaji wa bidhaa za bima inayofata misingi ya dini ya Kiislamu, kukamilisha idadi ya taasisi 11.
Na hii ndiyo alama ambayo Benki ya CRDB imekuwa ikijitahidi kuiacha katika kila bidhaa inayoileta sokoni, thamani ya hali ya juu kwa wateja wake wa hali za maisha na imani tofauti.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, Mkuu wa Huduma za Uwakala wa BenkiBima wa CRDB, Linda Kamuzora amesema kuwa wanajivunia, kwa kushirikiana na kampuni wabia, kuleta ubunifu na upatikanaji wa huduma za benki wakala bima zenye kukidhi mahitaji yaliyopo ya huduma za bima ndani ya kipindi cha miaka minne. Hii ikiwemo na bima za afya, vikundi n.k.
“Tuna bima za maisha zenye manufaa ya kutoa mkono wa pole kwa ajili ya vikundi hadi mtu mmoja mmoja, huduma za bima za maafa ya biashara kubwa na ndogo, bima za ushafirishaji mizigo, majengo, magari, mali binafsi, majengo ya biashara, za kampuni na mashirika.
Kama hiyo haitoshi tunayo bima ya kilimo, kama mtakumbuka kwenye sikukuu za Nanenane Mkurugenzi wetu alisema kupitia kampuni yetu tanzu, yani CRDB Insurance Company tumejikita kuleta mabadiliko katika utambuzi wa mifugo kwa kutumia pua hivyo kuongeza ubunifu na ushindani katika kutoa huduma ya bima ya mifugo.
Pia tunazidi kuweka nia hii hii katika bima ya mazao ifahamikayo kama “Kijani Bima” inayotoa malipo endapo kuna maafa katika mazao yaliyosababishwa na mvua au ugonjwa, wadudu waangamizi n.k
Jukumu letu kuu halijaishia kwenye usambazaji wa bima bali tumepewa wajibu wa mamlaka wa kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuwa na bima, upatikanaji wake na kazi yake ni nini,” amesema Linda huku akitaja huduma za bima za afya za vikundi na watu binafsi kuwa aina nyingine ya bima ambayo inapatikana kupitia Benki ya CRDB.
Ukuaji wa kutoa huduma za wakala benkibima za Benki ya CRDB
Linda amebainisha kuwa kama unaweka katika asilimia za ukuaji wa sekta hiyo, basi wamekua kwa asilimia 15 ikichangiwa na mchango wa huduma za wakala benkibima katika mapato ya ujumla ya benki hiyo.
Kulingana na ripoti ya Tira ya mwaka 2023, Benki ya CRDB, kupitia wakala benkibima imeshika nafasi ya kwanza ikiongoza soko la huduma za bima za jumla, ikichangia kiasi cha Sh 45.03 bilioni sawa na asilimia 31.52 ya Jumla ya Michango ya Bima (GPW) huku ikisalia nafasi ya pili katika soko la huduma za bima za maisha kwa kuchangia Sh 60.75 bilioni, sawa na asilimia 31.79 ya Jumla ya Michango ya Bima (GPW).
Amesema kuwapo katika soko la huduma za wakala benkibima kwa muda mrefu kumewahakikishia nafasi yao ya uongozi, ila pia kupitia matawi yetu wateja wanapata nafasi ya kuhudumiwa na kupata maelezo kuhusu huduma zetu za Bima.
Hata hivyo amesema kuwa benki hiyo kwa miaka mitatu mfululizo imeendelea kuwa kinara wa huduma za uwakala wa bima katika bima za maisha na za ujumla.
Linda amefafanua kuwa uwakala wa huduma za bima kwa benki, pamoja na sababu nyingine za kibiashara, zimekuja kubadili mitazamo na dhana kuhusu bima, ambapo asilimia kubwa ya watu walikuwa na imani ya kuwa bima ni wizi.
“Hii ilichangiwa na kukosekana kwa uaminifu kwa madalali wa bima ambao hapo nyuma walikuwa wanapokea michango ya wateja na kukaa nayo wenyewe bila kuwasilisha kwa kampuni za bima na kutengeneza migogoro baina ya wateja na kampuni hizo,” amesema zaidi.
Amesema kuwa uwepo wa huduma za bima kupitia benki umechangia kuongeza idadi ya benki nyingine kuanza kuchukua leseni na kufanya biashara hiyo na uelewa wa watu wengi kuhusu bima na faida zake.
Faida za huduma za wakala benkibima kupitia Benki ya CRDB
Linda ametaja faida za bima kupitia benki hiyo ni pamoja na urahisi wa upatikanaji wa bidhaa za bima kupitia mtandao wake wa CRDB wakala nchi nzima, matawi 250 yaliyotapakaa na jukwaa lake la SimBanking, kupitia njia hizi wateja wanaweza kukata bima mahali popote na wakati wowote.
Mkopo wa bima ni faida nyingine anayoipata mteja anayekata bima na CRDB. Kutokana na sheria kutaka mteja wa bima kulipa michango yake kwa mkupuo mmoja, kupitia benki ya CRDB, mteja anakopeshwa kulipiwa ada yake ya bima ya mwaka mzima huku akitakiwa kurejesha kidogo kidogo ndani ya miezi 10.
“Sokoni hakuna utaratibu huo kwa kampuni nyingi kwani utatakiwa kulipa kiwango kamili cha mwaka mzima au asilimia 70 ndani ya miezi sita, jambo linaloongeza makali ya gharama za bima kwa wateja ndicho kilichotupelekea kuja na mkopo wa bima ili kuwasaidia wateja wetu waweze kumudu kupata huduma za bima kwa unafuu.
Uzoefu wa uendeshaji wa madai ya bima kwa benki yetu unampa mteja amani ya moyo juu ya uhakika wa kupata stahiki zake bila kuingia katika migogoro. Linda amesema ushirikiano wao na kampuni kumi na moja za bima unawapa ujasiri na nguvu ya kuhudumia wateja wake,” amesema na kuongeza:
“Tunapozindua bidhaa sokoni tayari tunakuwa tumeshafanya utafiti na kuhakikisha hatua zote za kisheria zimefuatwa kuanzia underwriting, madai ya bima na namna gani ya kuelewa uendeshaji wake,” ameongeza zaidi.
Amesema ubunifu ni eneo lingine la kujivunia kwa benki hiyo ambapo bidhaa za bima hubuniwa kukidhi mahitaji mahsusi ya wateja wao.
Amesema kipengele cha bima kimeongezwa kwenye baadhi ya bidhaa za benki kama faida jumuishi na kuongeza thamani ya bidhaa za benki.
Wateja wanaoishi nje ya nchi
Kwa wale wanaomiliki akaunti za benki hiyo kutokea ughaibuni, wananufaika kwa bima katika akaunti zao ambapo mteja anapofariki hulipiwa gharama za usafirishaji mwili na rambirambi za Sh5 milioni kwa familia ya marehemu, ameeleza zaidi.
Kwenye bima za vikundi, licha ya wateja wa kifurushi cha juu zaidi kulipia kiasi cha Sh 6000 kwa mwezi lakini anaweza kupata rambirambi ya hadi Sh10 milioni pale mwanachama au mwenzi anapofariki huku pia wakiwa na fursa ya kuongeza wanakikundi wengine. Faida zingine ikiwepo na fao la Maisha kwa kufiwa mtoto hadi wanne, fao la ulemavu wa kudumu utokanao na ajali, fao la Maisha wazazi pamoja na wakwe n.k.
Bima kidijitali na ubunifu
Katika kufanikisha mkakati wa benki kutoa huduma zake kidijitali, Linda amesema Benki ya CRDB inaendelea kuimarisha kuuza bidhaa za bima kupitia mfumo wa SimBanking.
“Tumeunganisha mifumo yetu ya benki na ile ya Mamlaka yaani TIRA na TRA na hivi sasa wateja wetu wanaweza kununua huduma za bima, kwa mfano bima za magari kupitia SimBanking. Mteja anapolipia muamala wake unakwenda kuonekana katika mfumo wa Taifa wa kuhakiki bima.”
Linda ameweka wazi matamanio yao kama benki ni kuendelea kufungamanisha huduma za upatikanaji wa bima kimtandao (dijitali) zaidi kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya kila siku huku akigusia ushindani kutoka kwenye kampuni za mitandao ya simu.
“Tumeona hivi sasa mitandao ya simu imekuja na huduma tofauti zikiwemo huduma za bima ambazo wateja wanaweza kuzipata mahala popote, hivyo kama benki tunajaribu kutengeneza bidhaa zitakazozingatia urahisi wa upatikanaji wake na usasa kuhimili ushindani huo na kubakia kiongozi wa huduma hizi sokoni,” amesema Linda ambaye amekiri uwezekano wa hilo kupitia mtandao wao mpana wa mawakala na SimBanking.
Matarajio
Benki inaendelea na hatua ya mwisho ya kuleta bidhaa mpya ya bima sokoni ambayo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni. Hata hivyo, amesema bidhaa hiyo itakwenda kuleta masuluhisho ya mahitaji yote ya huduma za bima kwa watu na tasisi.
Linda amesema wanatarajia kuendelea na mageuzi ya kidijitali kwa kutumia bidhaa zile zile huku mtazamo wao ukiwekwa zaidi katika bidhaa za bima ndogo ndogo kwa watu wa kipato cha chini. Hii ni pamoja na kuhakikisha muendelezo wa kutoa taarifa na kuelimisha umma juu ya faida ya Bima.
“Mwaka jana tulianzisha bima ya buku, lengo likiwa kuongeza ukataji bima kwa watu wa maisha ya kawaida kabisa na kulifikia kundi hilo ambalo hukosa fursa ya kupata huduma za kifedha mara nyingi, tupo kwenye zoezi la kuiboresha huduma hii kuongezea wigo zaidi na kuwafikia Watanzania wengi ili kuendelea kuchagia upatikanaji wa bima.”