Benki ya CRDB yasaini mkataba wa Dola 320 milioni na DFC, Citi kusaidia wajasiriamali Tanzania na Burundi
Benki ya CRDB imengia makubaliano ya mkopo wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 320 na Shirika la Fedha la Kimataifa la Marekani (DFC) na Citibank ili kuimarisha uwezo wake wa kutoa mikopo kwa ajili ya biashara ndogo, hususan zile zinazomilikiwa na kuongozwa na wanawake na vijana.
Utiaji saini wa makubaliano hayo ulifanyika kwenye Makao Makuu ya Citibank yaliyopo jijini New York, kando ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo, na ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema katika hafla hiyo, "Mkopo huu wa Dola za Marekani milioni 320 utaongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ufadhili wa biashara ndogo na za kati zinaozoongozwa na wanawake na vijana nchini Tanzania na Burundi, na kuwawezesha wajasiriamali kuwa wabunifu na hatimaye kuchochea ukuaji endelevu.
Tuna imani kwamba fedha hizi hazitachochea tu uwezeshaji wa wajasiriamali nchini lakini pia kukuza usawa wa kijinsia, zikiwapa wajasiriamali wanawake msaada wanaouhitaji ili kustawi na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi.”
Mbali na hayo, fedha kutoka DFC na Citibank zitaimarisha juhudi za Benki ya CRDB za kuchechemua ukuaji wa uchumi jumuishi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwa ni sehemu ya mpango mkakati wake wa miaka mitano unaolenga kusaidia kundi la wajasiriamali.
Nsekela alibainisha kuwa, pamoja na na kuwa na bidhaa za kifedha bunifu, benki hiyo kupitia taasisi yake tanzu ya CRDB Bank Foundation, imeweka msisitizo mkubwa katika kuwajengea uwezo wajasiriamali vijana na wanawake kupitia mafunzo ya elimu ya fedha na ujasiriamali. "Ushirikiano huu na DFC na Citibank utachochea zaidi juhudi hizi," Nsekela aliongeza.
Mradi huo utasaidia zaidi ya biashara ndogo 4,500 nchini, zikitajwa kuwa miongoni mwa masoko yenye nguvu barani Afrika. Dola za Marekani Milioni 60 zitasaidia biashara ndogo za Kitanzania zinazomilikiwa au kuoongozwa na wanawake ambazo zimekidhi masharti ya Mpango wa DFC wa 2X wa uwezeshaji wanawake, zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi ambazo wanawake wanakabiliana nazo duniani kote.
Inaelezwa pia kiasi cha Dola za Marekani Milioni 25 zitaenda kusaidia biashara ndogo ndogo nchini Burundi. Nsekela alitoa shukurani kwa wadau wote waliohusika, akipongeza kazi kubwa ililofanywa na Serikali za Tanzania na Burundi katika kuweka mazingira wezeshi kwa ushirikiano huo.
"Sera na mifumo wezeshi iliyowekwa na Serikali zetu imekuwa muhimu katika kuvutia uwekezaji wa kimataifa, ambao ni muhimu katika kuendeleza ajenda yetu ya maendeleo," Nsekela alibainisha.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa DFC, Nisha Biswal alisisitiza dhamira ya dhati ya shirika hilo, akisema, "DFC imejidhatiti kukuza uchumi wa Tanzania, kwa kuzingatia uwekezaji ambao unaleta athari chanya kwa jamii. Mkopo huu utasaidia maelfu ya wafanyabiashara wadogo ambao ni mhimili wa maendeleo ya kiuchumi."
Mkopo huo unaakisi dhamira ya DFC ya kupanua uhusiano wake nchini ili kuimarisha ushirikiano wake uliopo na kutafuta fursa mpya za ushirikiano, kuendeleza usalama wa kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kote barani Afrika.
Mkopo huu ni matunda ya kazi kubwa iliyowahi kufanyika hapo awali kati ya DFC, Benki ya CRDB pamoja na USAID/Tanzania kusaidia wafanyabiashara wadogo wa Kitanzania, ikijumuisha dhamana ya Dola za Marekani milioni 20 kusaidia utoaji mikopo kwa wafanyabiashara wadogo kwa lengo la kutoa huduma za elimu na kuzifikia sekta zisizo rasmi huku Dola za Marekani milioni 4 zikijikita kuongeza upatikanaji wa fedha kwa wanawake na vijana wanaokopa katika sekta ya afya.
Afrika ndiyo eneo la kipaumbele la uwekezaji wa DFC duniani kote. Kwa sasa shirika hilo lina zaidi ya Dola za Marekani bilioni 11 zilizoenda katika miradi ya uwezeshaji fedha kwa wajasiriamali barani Afrika, uwiano mkubwa zaidi wa fedha za uwekezaji duniani.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Citi Tanzania na Mkuu wa Huduma za Benki, Geofrey Mchangila alisema kuwa: "Kama Citi, tunaendelea kupambana kutekeleza ajenda yetu ya uwezeshaji fedha kwa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia ushirikiano wenye ubunifu kama huu.
Lengo letu ni kusaidia kujenga thamani halisi ya kiuchumi nchini Tanzania kusaidia malengo ya ujumuishi wa kifedha kupitia uwezeshaji wa wafanyabiashara wadogo kwa kukata kiu ya huduma za kifedha ambayo ilikuwa haijapatiwa ufumbuzi.
Makubaliano haya ni sehemu ya ahadi yetu ya uchangiaji Dola za Marekani trilioni 1 kwenye miradi endelevu ya kifedha ifikapo 2030, inayolenga kuongeza upatikanaji wa ajira, fedha, miundombinu ya msingi na huduma kwa jamii zenye kipato cha chini katika masoko yanayokua kwa kasi.
Kwa kutambua kuwa kesho iliyobora inategemea uwezeshaji wa wanawake na vijana, Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika uwezeshaji kundi hili nchini Tanzania, ikitengeneza fursa zinazochochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kama taasisi ya fedha inayoongoza nchini, imekuwa nguzo muhimu katika kuzishika mkono Biashara Ndogo Ndogo na za Kati, hususan zinazomilikiwa na wanawake na vijana, kuwezesha kustawi na kuwa vichocheo muhimu vya uimarishaji wa uchumi wa Tanzania.
Ikiwa na kampuni zake tanzu nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Benki hiyo pia inawaweka wafanyabiashara wadogo wadogo, wadogo na wa kati wa Kitanzania kutumia fursa mpya za kikanda kupitia Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA).
Kwa kuunganisha biashara za Kitanzania na soko la zaidi ya wateja bilioni 1.3 barani Afrika, Benki ya CRDB inafungua fursa kubwa za kiuchumi kwa wajasiriamali wa Tanzania, ili watimize ndoto zao za kutambulika kama wafanyabiashara wakubwa barani Afrika.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Benki ya CRDB imetoa zaidi ya Sh 4 trilioni kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo, wadogo na wa kati katika sekta mbalimbali, huku kipaumbele kikienda kwenye biashara zinazomilikiwa na wanawake kupitia huduma yake ya CRDB Malkia.
Hatua hii sio tu imeongeza upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali wanawake lakini pia imewawezesha kukuza biashara zao na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.