Bonite Bottlers Ltd: Uwekezaji katika teknolojia za kisasa umetufanya tung’are katika PMAYA 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Fillip Mpango (kulia) akikabidhi cheti kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bonite Bottlers

Raman Anantha Narayanan wakati wa hafla ya ugawaji wa tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA).

Muktasari:

Novemba 18, 2022 Bonite Bottlers Ltd, wazalishaji wa bidhaa za Coca Cola na Maji ya kunywa ya Kilimanjaro, iliyopo Shirimatunda, Kilimanjaro walitunukiwa Tuzo ya Rais ya Mzalishaji bora wa mwaka katika kipengele cha vinywaji visivyo na kilevi.

Novemba 18, 2022 Bonite Bottlers Ltd, wazalishaji wa bidhaa za Coca Cola na Maji ya kunywa ya Kilimanjaro, iliyopo Shirimatunda, Kilimanjaro walitunukiwa Tuzo ya Rais ya Mzalishaji bora wa mwaka katika kipengele cha vinywaji visivyo na kilevi.

Hii ni mara ya pili kwa kampuni hii bora kupokea tuzo hiyo, 2021 ikiwa ya kwanza. Tuzo hiyo ilitolewa na Makamu wa Rais, Philip Mpango kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

PMAYA ni nini na jukumu lake ni lipi?

Tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA) ni hafla ya kila mwaka ambayo huandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) ili kutoa tuzo kwa kampuni zilizofanya vizuri katika mwaka uliotangulia.

Tuzo hizi zilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 2005 na zimefanyika kila mwaka tangu wakati huo. Tuzo hizo zinalenga; kutambua na kuthamini mchango muhimu wa sekta ya viwanda katika mchakato wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania, kuinua kiwango cha ufanyaji wa biashara na utawala bora wa mashirika nchini na kutambua na kutathmini maendeleo ya kiteknolojia katika sekta ya viwanda.

Kwa kipindi cha miaka 17 mfululizo (tangu 2005), CTI imekuwa ikiandaa tukio hili la kifahari zaidi la wanachama linalojumuisha sekta zote za uchumi.

Washindi wa shindano hilo hukabidhiwa tuzo wakati wa hafla ya chakula cha jioni ya kibiashara inayoandaliwa na CTI ambayo kwa kawaida huhuduriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mlezi wa CTI.

Mwakilishi wa Bonite azungumzia siri ya ushindi

Katika mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bonite Bottlers Raman Anantha Narayanan, alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na Uongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) kwa tuzo hiyo chini ya kipengele cha vinywaji visivyo na kilevi, ambavyo ni maji ya kunywa ya kilimanjaro na soda za Coca Cola.

Akibainisha baadhi ya mambo yaliyosababisha kutwaa tuzo hiyo, Narayanan aliishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa msaada wa mara kwa mara katika masuala ya sera na miundombinu ambayo inawawezesha wenye viwanda kote nchini kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya watu.

Sababu nyingine aliyoitaja ni uwekezaji katika teknolojia za kisasa zaidi za uzalishaji na uboreshaji wa chupa za bidhaa zao zote mbili Coca Cola na maji ya kunywa ya Kilimanjaro ambazo inazipa ubora wa hali ya juu kwa watumiaji wao.

Narayanan pia alitoa shukrani kwa bodi ya wakurugenzi, uongozi na wafanyakazi chini ya uenyekiti wa Abdiel Mengi kwa miongozo na msaada wanaoutoa katika kufikia malengo ya kampuni. Abdiel alichukua nafasi hiyo iliyoachwa na Hayati, Dk Reginald Mengi na ana ndoto kubwa za kuendeleza misingi na maadili mema iliyowekwa na Hayati Dk Mengi.

Kampuni ya Bonite Bottlers itaendelea kuheshimu dhamira yake kwa umma wa Watanzania kwa kuhakikisha wanaendelea kuzalisha bidhaa zao katika ubora wa hali ya juu kwa watumiaji wao.