DMG na mkakati wa kuleta mapinduzi katika sekta ya bahari nchini
Bahari ni rasilimali muhimu katika kukuza uchumi, husasni kwa nchi zilizo na mwambao. Kuna sekta nyingi zinazotegemea bahari moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kama vile uvuvi, uchukuzi, utalii na nishati ya baharini.
Rasilimali hiyo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa dunia, hususani kwa nchi zenye mwambao. Eneo hili la maji lina fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinachangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kiwango kikubwa.
Uvuvi ni mojawapo ya sekta muhimu zaidi zinazotegemea bahari. Bahari hutoa samaki na viumbe wengine wa baharini ambao ni chanzo cha chakula kwa mamilioni ya watu duniani kote. Hii inachangia kupunguza njaa na kutoa ajira kwa watu wengi, hususani katika nchi zinazoendelea.
Bahari ni njia kuu ya usafirishaji wa bidhaa duniani. Karibu asilimia 90 ya biashara ya kimataifa inategemea bahari, ambapo meli zinatumika kusafirisha bidhaa mbalimbali kama mafuta, magari, vifaa vya umeme na bidhaa za kilimo.
Utalii wa baharini ni chanzo kingine kikubwa cha mapato kwa nchi nyingi. Miji ya kitalii inayopatikana kando ya bahari huvutia watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Vivutio kama fukwe nzuri, michezo ya maji, na maeneo ya kupiga mbizi huvutia watu na kuleta fedha za kigeni.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayojivunia kuwa na rasilimali hii muhimu ambayo imekuwa mhimili mkubwa katika kuchangia ukuaji wa uchumi. Hii ni kutokana na uwekezaji uliofanyika katika sekta ya bahari.
Dar es Salaam Merchant Group (DMG) ni miongoni mwa wadau muhimu katika sekta ya bahari ambapo wamejipambanua kama moja ya kampuni za kizawa zinazofanya vizuri katika sekta hiyo hususan kwenye maeneo ya uvuvi na shughuli za uchukuzi.
Ikiongozwa na misingi ya kuanzishwa kwake ambayo ni kuongeza thamani kwa jamii, kuweka malengo ya muda mrefu pamoja na kuwepo kwa manufaa ya pande mbili kwa kila eneo wanalofanya biashara.
Mkurugenzi Mtendaji wa DMG, Rayton Kwembe anasema kampuni hiyo ya kitanzania iliyoanzishwa miaka tisa iliyopita inajihusisha na ufanyaji biashara (kununua na kuuza bidhaa), ushauri elekezi katika sekta mbalimbali hususani sekta ya bahari (marine) pamoja na shughuli za bahari (marine activities).
Kwembe anasema katika utekelezaji wa majukumu haya wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali ambayo imekuwa mdau wake mkubwa.
“Tumefanya kazi na taasisi mbalimbali ikiwemo za Serikali kama vile; Ofisi ya Waziri Mkuu, Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Shirika la Huduma za Meli, Mamlaka ya Bandari, Wizara ya Uchumi wa Bluu Zanzibar na wadau wengine wa sekta binafsi “ anasema Kwembe.
Ubunifu, ujenzi na ukarabati wa meli
Kwembe anasema mwaka 2017 DMG ilianzisha kitengo cha shughuli za bahari (Marine section) ambacho kilipewa jukumu la kufanya ubunifu, kutengeneza pamoja na kufanya ukarabati wa meli.
“Sababu ya kuanzisha kitengo hichi ni kutokana na fursa tulizoziona katika sekta ya bahari kwani ni sekta yenye fursa nyingi za kusaidia ukuaji wa uchumi ambazo hazijaweza kutumiwa ipasavyo, lakini mkakati na juhudi za Serikali za kuamua kuipa jicho la kipekee sekta hii ikiwemo kufufua shirika la meli pamoja na kutekeleza miradi ya ujenzi wa meli ni sababu kuu zilizotushawishi kuingia katika sekta hii,” anasema Kwembe.
DMG ni kampuni ya pili ya kitanzania kupewa leseni ya kufanya shughuli za ukandarasi wa bahari (marine contractor) nchini. Kwembe anasema kuna mataifa makubwa duniani ambayo uchumi wake umekuwa kutokana na kuwekeza katika shughuli za bahari ikiwemo Korea Kusini.
Juhudi za Serikali katika kuhakikisha sekta hii inakua na kuongeza tija katika uchumi iliwasukuma DMG kutafuta wadau mbalimbali wa kufanya nao kazi wenye teknolojia za kisasa na utaalamu wa masuala ya meli na kuingia nao makubaliano ya ushirikiano jambo lililowawezesha kwenda na kasi ya Serikali.
Kwembe anasema hatua hiyo iliwawezesha kuwa kampuni ya kitanzania iliyoaminiwa na Serikali kwa kuweza kushiriki katika miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa meli.
“Mradi wa kwanza tulioahiriki ulikua wa ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi tu ambapo tulipewa kazi na Mkandarasi Mkuu kutoa huduma kwenye mradi ikiwepo kuajili wataalamu wa kizawa, kusimamia masuala ya kiutawala kwenye mradi hasa yanayohisisha maudhui ya ndani (local content). Huu ndio mradi ambao ulitifungulia njia na kuanza kufahamika na wadau wengine,” anasema Kwembe.
Anasema wakati wanaingia mwaka 2017 walijewekea lengo la kuhakikisha wanakuwa kampuni namba moja ya kitanzania katika sekta hiyo lakini pia kuliteka soko la Afrika lengo ambalo anaamini wameanza kulifikia kwa kiasi kikubwa.
“Katika kipindi cha miaka minne tumeweza kufanya kazi na taasisi zote za Serikali ambazo zinamiliki meli ikiwa ni pamoja na Kampuni ya Huduma za Meli ambayo kwa sasa ni wateja wetu wakubwa. Kampuni hiyo kwa sasa tunatekeleza nayo miradi mitatu ambayo ni; mradi wa kimkakati wa kufufua meli ya MV Liemba mradi huu ni wa kihistoria lakini Serikali imetuamini na kutukabidhi. Kwa sasa mradi umeshaanza na fedha za awali tushalipwa,” anasema Kwembe.
Anasema mradi mwengine ni ukarabati wa meli kubwa ya mafuta iliyopo jijini Mwanza pamoja na ukarabati wa tugboat moja kazi ambazo mikataba yake imeshasainiwa na malipo ya awali yameshalipwa hivyo kwa upande wa ukarabati tuna kazi tatu ambazo tunafanya na Kampuni hiyo.
Kwa upande wa kazi za usimamizi kampuni hiyo pia imetupa kazi mbili katika miradi ya ujenzi wa meli mbili za mizigo katika ziwa Victoria na Tanganyika ambayo inatekelezwa na Kampuni za Uturuki.
Kwembe anasema mbali na kampuni hiyo pia wamefanya kazi na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika utekelezaji wa miradi mitano.
“TPA tumetekeleza miradi ya ukarabati wa boti ndogo ya kubeba wafanyakazi wa meli (MV Aida Kondo) katika bandari ya Tanga pamoja na kuingia makubaliano ya kuuza boti za fiber, uuzaji wa vipuri vya boti za Mtwara na Tanga, pia tumefanya kazi ya ukarabati wa vivuko vya Temesa ikiwemo kivuko cha MV Tanga, MV Kitunda kilichopo Lindi, MV Kilambo kikichopo Mtwara pamoja na kuanza ujenzi wa meli mpya ya kwenda Mafia na Nyamisati,” anasema Kwembe.
Kuhusu uwekezaji katika teknolojia za kisasa za ujenzi wa meli anasema kwa sasa wanashirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) pamoja na Chuo cha Bahari (DMI) kwa ajili ya kuchukua wahitimu na kuwakutanisha na wataalamu kutoka Korea kwa ajili ya kupata uzoefu.
“Kwa sasa tuna wataalamu watano kutoka kwenye vyuo hivi ambao wanapata mafunzo kutoka kwa mtaalamu kutoka kwa washirika wetu wa Korea ili kuhakikisha tunakuwa na rasilimali yenye uwezo wa kutumia teknolojia hizo. Lakini pia kwa sasa tuna maeneo yetu wenyewe ya kufanyia kazi (facilities) ambayo moja iko Kimbiji na nyingine iko Zanzibar eneo la Mangapwani,” anasema Kwembe.
Uvuvi wa Bahari Kuu
DMG ni kampuni ambayo ilifanya utafiti kuhusu changamoto zinazowakabili wavuvi wengi nchini kwenda kuvua katika bahari kuu na kugundua kuwa sababu kubwa ni ukosefu wa vyombo ambavyo vinawawezesha kufika bahari kuu pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu bahari kuu.
Katika kuhakikisha inapunguza changamoto hiyo, DMG iliingia makubaliano na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambapo benki hiyo imetoa kiasi cha Sh 1 bilioni kwa DMG kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kisasa wa boti za kufanyia uvuvi wa bahari kuu.
“Baada ya kufanya utafiti na kugundua changamoto hizo tulienda kufanya mazungumzo na TADB ma wakakubali kutufadhili Sh 1 bilioni kwa ajili ya kujenga meli nne za uvuvi za kisasa ambapo kati ya hizo meli moja imekamilika na inatarajiwa kuanza kazi hivi karibuni, ya pili inatarajiwa kuanza kazi Desemba mwaka huu ya tatu Aprili mwaka 2025 na ya nne Oktoba, 2025 ,” anasema Kwembe. Tunaamini boti hizi zitaenda kuleta mageuzi makubwa katika uvuvi wa Bahari kuu.
Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani
Kama mdau muhimu wa sekta ya bahari, DMG wamejiandaa kuadhimisha siku ya bahari duniani mwaka huu kwa kufanya matukio mawili makubwa.
“Tunatarajia kufanya uzinduzi wa boti zetu za kisasa za uvuvi na kufanya safari ya kwanza kwenda bahari kuu lakini pia tutafanya usafi katika maeneo ya bahari tunayofanyia kazi,” anasema Kwembe.