DSE na utoaji fursa za uwekezaji katika dhamana, kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na utoaji mitaji
Uwekezaji ni njia mojawapo ya kuongeza thamani ya mali zako kwa kuzifanya zitoe mapato zaidi. Moja ya aina za uwekezaji zinazojulikana ni uwekezaji katika dhamana na hatifungani.
Dhamana ni vipande vya umiliki katika kampuni fulani. Unaponunua dhamana, unakuwa sehemu ya wamiliki wa kampuni hiyo na una haki ya kushiriki faida zake kupitia gawio na ongezeko la thamani ya dhamana. Dhamana ni maarufu kwa wawekezaji wanaotafuta ukuaji wa mtaji kwa muda mrefu.
Hatifungani ni aina ya uwekezaji ambapo mwekezaji anakopesha fedha kwa shirika au Serikali kwa riba. Kwa kawaida, hatifungani zina muda maalumu wa malipo, ambapo mwekezaji atapata malipo ya riba mara kwa mara hadi muda huo utakapomalizika na kisha kurejeshewa mtaji wake wa awali.
Uwekezaji katika dhamana na hatifungani hutoa fursa nyingi za kifedha kwa wawekezaji. Wakati dhamana zinatoa uwezekano wa faida kubwa kupitia ukuaji wa mtaji na gawio, hatifungani hutoa usalama wa mtaji na mapato ya mara kwa mara.
Kwa kuchanganya aina hizi mbili za uwekezaji, wawekezaji wanaweza kufaidika kutokana na urari wa hatari na faida na hivyo kuwa na uwekezaji habiti na wenye faida.
Ili uwekezaji huu uweze kuleta tija kwa wananchi na Taifa, lazima kuwepo na jukwaa la uwazi na linalodhibitiwa vizuri ambapo wawekezaji wanaweza kununua na kuuza dhamana na hatifungani jukumu ambalo linafanywa na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
DSE ni jukwaa ambalo kampuni na Serikali zinaweza kutoa dhamana na hatifungani kwa wawekezaji ili kupata mtaji wa kukuza biashara na miradi ya maendeleo.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela anaeleza mambo mbalimbali kuhusu taasisi hiyo na namna ilivyoleta mapinduzi katika uchumi wa Tanzania. mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo;
Je, ni mchango gani mkubwa ambao Soko la Hisa la Dar es Salaam limekuwa nao katika kukuza uchumi wa Tanzania tangu kuanzishwa kwake?
Soko la Hisa la Dar es Salaam limekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania kupitia:
Kuwezesha ubinafsishaji wa mashirika ya umma kama vile TBL, TCC, TOL, TPCC, n.k. Ubinafsishaji huu umesaidia kuongeza ufanisi na kusaidia mashirika kutoa gawio na kodi kwa Serikali na pia kuchangia katika Pato la Taifa.
Kuziwezesha kampuni kukuza mitaji yake kwa mfumo wa kuuza hisa na hatifungani kupitia Soko la Hisa.
Kuwezesha uuzwaji wa hatifungani za Serikali na taasisi za Umma na za kiserikali (mfano, Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka ya Jiji la Tanga; Tanga UWASA).
Kutoa fursa kwa Watanzania kuwekeza katika dhamana zilizoorodheshwa sokoni na kutoa elimu na mafunzo juu ya uwekezaji na faida zake kwa Watanzania.
Je, DSE inachangiaje katika kuongeza uwekezaji wa ndani na wa nje katika sekta mbalimbali za uchumi?
Kwa kushirikiana na Serikali, mashirika ya umma, taasisi binafsi na wadau wengine wa maendeleo, DSE inatoa fursa za uwekezaji katika dhamana zilizoorodheshwa kwa kutoa gawio na riba shindani, kufanya biashara katika mazingira yenye uwazi, kuweka sheria na kanuni nzuri zinazoweka mazingira mazuri ya uwekezaji na utoaji mitaji.
DSE inachangiaje katika kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa makampuni yaliyoorodheshwa?
Soko lina sheria na kanuni ambazo zinatoa muongozo wa uwazi katika ufanyikaji wa biashara na wakati huo huo ikiwalinda wawekezaji na watafuta mitaji kwa ujumla.
Ni fursa zipi ambazo DSE inatoa kwa wananchi wa kawaida na wawekezaji wadogo katika kujenga utajiri na kuongeza kipato?
DSE ina bidhaa kuu mbili nazo ni Hisa na Hatifungani. DSE kwa kushirikiana na Mawakala wa soko, inatoa mafunzo na ushauri kwa wananchi wa kawaida kupitia vyombo vya habari, semina, makongamano, warsha na mikutano mbalimbali, juu ya namna ya kuwekeza na kupata faida kupitia dhamana zilizoorodheshwa.
DSE imeenda mbali zaidi kwa kushauri pia makampuni yanayouza hisa zake katika Soko, kuweka bei ambazo Mtanzania wa hali yoyote anaweza kumudu na kushiriki katika kujiongezea kipato.
Faida za uwekezaji hupatikana kupitia gawio litokanalo na faida ambayo makampuni iliyoorodheshwa kufanya biashara imefanikiwa kupata; pia faida huweza kupatikana kutokana na uongezekaji wa thamani za hisa husika pale kampuni zinapofanya vizuri na kuvutia wawekezaji zaidi ambao hufanya bei yah isa kupanda kutokana na kupanda uhitaji wa hisa hizo.
DSE ina mipango gani ya kuhakikisha kuwa uwekezaji wa hisa unakuwa endelevu na unachangia ukuaji wa uchumi wa muda mrefu?
Baadhi ya mipango ya DSE katika kuhakikisha kuwa uwekezaji wa hisa unakuwa endelevu na unachangia ukuaji wa uchumi wa muda mrefu ni pamoja na;
Uwepo wa mazingira mazuri na wezeshi ambayo yanavutia makampuni na taasisi binafsi kuja sokoni kuuza hisa na hatifungani kwa bei shindani ambayo inahakikisha uendelevu wa kufanya biashara, kulipa kodi, kuajiri Watanzania na kutoa huduma katika jamii.
Kutoa elimu na ushauri endelevu kwa umma katika namna ambavyo muwekezaji anaweza kunufaika na uwekezaji katika dhamana zilizoorodheshwa katika soko.
Kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha elimu ya fedha na uwekezaji inaanza kufundishwa mashuleni kuanzia ngazi za awali
Uwepo wa bidhaa mpya zenye mrengo wa kutoa faida nzuri kwa wawekezaji na kusimamia sheria na kanuni ambazo zinawalinda watafuta mitaji na wawekezaji kiujumla.
Ni changamoto zipi DSE inakutana nazo katika juhudi zake za kuchangia ukuaji wa uchumi endelevu, na ni hatua gani zinafanywa kuzitatua?
Changamoto kubwa haswa na utayari wa watanzania katika masuala mazima ya masoko ya mitaji na dhamana. Hii inaenda kwa pande zote mbili za wadau wa soko ambao ni watafuta mitaji na wawekezaji.
Watafuta mitaji: Wamiliki wengi wa makampuni ambayo yangeweza kuja sokoni kutafuta mtaji kwa kuuza hisa (sehemu ya kampuni hizo) kidogo wamekuwa na ugumu wa kufanya hivyo kwa sababu ya kutotaka kupunguza umiliki wa kampuni kwa kufikiria juhudi walizoweka katika kuyajenga lakini pia sharti la kampuni hizo kuweka taarifa za utendaji wa biashara zao wazi kwa umma umeonekana kuweka ugumu kuyavutia makampuni kuja sokoni.
Wawekezaji: Watanzania wengi wamekua nyuma katika shughuli za uwekezaji rasmi na hivyo kuweka nguvu nyingi sana katika uwekezaji usio rasmi kisheria kama vile vikoba na vikundi vya mtaani kutokana na kutokidhi au kutokuwa na nyaraka zitakazowawezesha kufanya uwekezaji rasmi mfano Vitambulisho vya Taifa. Wengi pia wamekuwa wakiamini katika uwekezaji wa kupata faida ya haraka ambayo katika soko la hisa uvumilivu ni nguzo ya muhimu sana.
Je, DSE imechukuwa hatua gani kuhakikisha kuwa makampuni yanayoorodheshwa yanafuata sera za mazingira, kijamii, na utawala bora (ESG) ili kukuza uchumi endelevu?
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limetekeleza hatua kadhaa ili kuhakikisha kuwa makampuni yaliyoorodheshwa yanazingatia sera za Mazingira, Kijamii na Utawala (ESG) ili kukuza uchumi endelevu. Hatua hizi ni pamoja na:
Inajumuisha Mahitaji ya Kuripoti ya ESG: DSE inahitaji kampuni zilizoorodheshwa kufichua matumizi ya ESG kama sehemu ya ripoti zao za kawaida. Hii inahakikisha uwazi na uwajibikaji, na kuhimiza makampuni kupitisha mazoea endelevu.
Sheria na Kanuni za Kuorodhesha: DSE imeunganisha vigezo vya ESG katika sheria zake za uorodheshaji, na kuifanya hitaji la makampuni kutii viwango mahususi vya ESG. Hii husaidia katika kuoanisha shughuli za shirika na malengo endelevu.
Ukuzaji wa Fahirisi za ESG: DSE imefanya kazi katika kutengeneza fahirisi za ESG zinazofuatilia utendakazi wa kampuni zinazofuata viwango vya juu vya ESG. Hili halitoi motisha kwa kampuni tu kuboresha utendakazi wao wa ESG lakini pia huwapa wawekezaji kipimo cha kutathmini uendelevu.
Uhamasishaji na Kujenga Uwezo: DSE huendesha warsha, semina, na vipindi vya mafunzo kwa makampuni yaliyoorodheshwa ili kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa mazoea ya ESG. Mipango hii husaidia makampuni kuelewa manufaa ya kujumuisha ESG katika shughuli zao na kuripoti.
Ushirikiano na Mashirika ya Udhibiti: DSE inashirikiana na mashirika ya udhibiti kama vile Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ili kuhakikisha kwamba utiifu wa ESG unatekelezwa. Ushirikiano huu husaidia katika kufuatilia na kutathmini utendaji wa ESG wa makampuni yaliyoorodheshwa.
Kuhimiza Dhamana za Kijani na Ufadhili Endelevu: DSE inakuza utoaji wa hati fungani za kijani na vyombo vingine endelevu vya kifedha. Kwa kutoa jukwaa la vyombo hivyo, DSE inahimiza makampuni kufadhili miradi ambayo ina athari chanya kwa mazingira na kijamii.
Ufichuzi wa Umma na Uwajibikaji: Makampuni yaliyoorodheshwa kwenye DSE yanahimizwa kuweka hadharani mikakati na utendakazi wao wa ESG. Uwazi huu unaruhusu washikadau, ikiwa ni pamoja na wawekezaji, kufanya maamuzi sahihi kulingana na kujitolea kwa kampuni kwa uendelevu.
Kukuza Uelewa wa Wawekezaji: DSE inashirikiana na wawekezaji ili kuangazia umuhimu wa mambo ya ESG katika maamuzi ya uwekezaji. Kwa kukuza uwekezaji unaowajibika, DSE husaidia kuongeza mahitaji ya makampuni ambayo yanatanguliza ESG, na kuwatia moyo zaidi kufuata mazoea endelevu.
DSE inashirikiana vipi na wadau katika kuboresha uelewa na matumizi ya masoko ya mitaji katika kukuza uchumi?
DSE imekua moja ya wadau wakubwa katika mpango mkakakati wa Serikali wa Elimu ya huduma za kifedha “Financial Literacy” na ushirikishwaji “Inclusion” ambao unasimamiwa na Wizara ya Fedha. Katika mpango huu, DSE imetoa mchango wake kwa namna gani umma unaweza kunufaika na uwekezaji katika Soko lakini pia tumekua tukishiriki katika wiki ya elimu za huduma za kifedha chini ya Wizara ya Fedha, makongamano, warsha, semina, mikutano, midahalo ambayo imelenga kutoka uelewa wa masuala ya huduma za kifedha.
Lakini soko pia linaendesha shindano “DSE Scholar Investment Challenge” la kujifunza uwekezaji kwa vitendo kupitia App ambalo limelenga wanafunzi wa vyuo vikuu kwa ajili ya kuwapa elimu na uelewa wa jinsi ya kuwekeza na kunufaika na bidhaa zilizopo katika Soko.
Je, kuna mikakati gani inayowekwa na DSE ili kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika masoko ya mitaji?
Tangu kuanzishwa kwa Soko la hisa mwaka 1998, limekuwa likiweka kipaumbele kwa kada zote za jamii ambazo ndani yake kuna wanawake na vijana. Elimu ndiyo imekuwa nguzo kubwa lakini pia uwepo wa bidhaa zenye bei ambazo kila kada inaweza kumudu kwa urahisi mfano hisa za makampuni yaliyoorodheshwa katika soko.
Kupitia Soko la Hisa, baadhi ya watafuta mitaji wameweza kutoa hatifungani ambazo zimelenga kusaidia makundi haya maalum kwa kuuza hatifungani ya jinsia “Gender Bond” ambayo ilifuatiliwa na hatifungani ya kijamii “Social Bond”.
DSE inachangiaje katika kuwawezesha wawekezaji kuwekeza kwenye sekta ambazo zina athari kubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kama vile kilimo, elimu, na afya?
Kwa kutoa elimu ya uwekezaji kwa umma, kwa kuweka mazingira mazuri ya sekta hizo kuweza kupata mitaji ya kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia hatifungani za kijamii mfano zile za benki ya CRDB, NMB, NBC, KCB na hivi karibuni kumekuwa na hatifungani ya Tanga UWASA Water Bond.
Makampuni yanapokuja kutafuta mitaji kwa kuuza hisa zake maana yake yanaenda kupata mitaji ambayo inaenda kuyaongezea nguvu ya kulipa kodi na pia kuajiri watanzania ambao pia watalipa kodi na kuchangia katika shughuli nyingine za kimaendeleo.