DUWASA na mikakati kabambe ya uboreshaji huduma ya maji Dodoma

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (wa kwanza kushoto) akizungumza jambo wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji Ihumwa-Njedengwa jijini Dodoma. Wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph na maofisa wengine.

Muktasari:

Maji ni rasilimali muhimu kwa mustakabali wa Taifa lolote duniani. Bila maji, hakuna maisha na maji yamechukua takriban robo tatu ya sehemu ya dunia.

Maji ni rasilimali muhimu kwa mustakabali wa Taifa lolote duniani. Bila maji, hakuna maisha na maji yamechukua takriban robo tatu ya sehemu ya dunia.

Upatikanaji wa maji umekuwa jambo muhimu katika historia ya utamaduni wa binadamu tangu mwanzo lakini rasilimali yenye faida lukuki endapo tu itatumika vyema.

Rasilimali hii ipo hatarini kutokana na kutokutumika na kulindwa vyema. Serikali nyingi duniani zimekuwa zikichukua hatua za kusimamia vyema rasilimali hii ili isipotee kwa kuja na mikakati mbalimbali ya kuihifadhi na kuilinda.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi akieleza jambo katika moja ya mikutano yake

Hapa nchini jukumu hilo lipo chini ya Ofisi za Mabonde Tisa ambayo ndiyo yenye majukumu ya Kisheria kuhakikisha kuna matumizi sahihi ya maji kwa maslahi ya Taifa.

Na kwa upande wa Dodoma, chanzo kikubwa cha maji kinapatikana katika Bonde la Makutupora ambalo linasimamiwa na Ofisi ya Bonde la Wami-Ruvu.

Jukumu la msingi la DUWASA ni kutoa huduma endelevu ya usambazaji majisafi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa maeneo yanayohudumiwa ambayo ni Jiji la Dodoma na miji ya Bahi, Chamwino na Kongwa.

Pia, mamlaka hiyo imepewa jukumu la kusimamia Mamlaka za maji za Kibaigwa na Mpwapwa kwa lengo la kuhakikisha zinajengewa uwezo ili zijitegemee. Hivi karibuni DUWASA iliendesha semina ya elimu kwa Wahe.

Madiwani wa Jiji la Dodoma kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Mipango Vijijini (IRDP) ambapo masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na huduma za maji na majitaka kwenye Kata mbalimbali za Jiji la Dodoma, changamoto sambamba na mipango mbalimbali ya maboresho katika jiji hilo.

Hali ya Usambazaji Majisafi

Hadi mwezi Septemba 2021, DUWASA ilikuwa na mtandao wa majisafi wenye urefu wa kilomita 728.07 na imeweza kuunganisha huduma ya majisafi kwa wateja 61,410 kupitia uunganishaji huu, DUWASA imeweza kuhudumia asilimia 62.7 ya wakazi wote kwa sasa.

Mafanikio ya Duwasa, Dodoma Mjini

Mamlaka hiyo imefanikiwa kutekeleza yafuatayo:-

• DUWASA imefanikiwa kuondoa mgao mkali wa maji ulikuwepo kabla ya kuanzishwa kwake mwezi Julai, 1998;

• Kuongeza idadi ya wateja kutoka 4,800 waliokuwepo mwaka 1998 hadi kufikia 61,410 mwezi Septemba, 2021;

• Kuongeza mapato ya Mamlaka kutoka wastani wa shilingi milioni 14 kwa mwezi mwaka 1998 hadi kufikia shilingi bilioni 2 mwezi Septemba, 2021;

• Kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha huduma ya maji ikiwemo mradi ulioongeza uwezo wa uzalishaji maji Mzakwe kutoka lita milioni 30 kwa siku hadi lita milioni 61 kwa siku uliokamilika mwaka 2015;

• Kuongeza mtandao wa majitaka kutoka kilomita 42.2 mwaka 2010 hadi 117.9 mwaka 2021;

• Kupunguza upotevu wa maji kutoka wastani wa asilimia 40 mwaka 2010 hadi asilimia 34.9 mwezi Septemba, 2021;

• Kurahisisha mifumo ya utoaji na upokeaji wa taarifa kutoka kwa wateja.

Changamoto

• Mahitaji makubwa ya maji ambayo ni mita za ujazo 103, 000 kwa siku ikilinganishwa na uzalishaji wa mita za ujazo 66,000 kwa siku.

• Ufinyu wa mitandao ya majisafi na majitaka kuweza kuwafikia Wananchi wote wanaoishi ndani ya eneo la utendaji kazi la DUWASA;

• Mabwawa ya majitaka ya Swaswa kuzidiwa kiasi cha kutokidhi viwango vinavyotakiwa;

• Kuchakaa kwa mfumo wa majitaka wa area C na D na kusababisha kuziba mara kwa mara. Baadhi ya wananchi wasio waaminifu wanaoiba maji kwa njia mbalimbali na ili kukomesha tatizo hili, DUWASA imeweka mkakati wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani wanaobainika Mamlaka hiyo inakamata wastani wa wezi watano hdi sita kila mwezi), kutoa motisha kwa watoa taarifa kiasi cha Sh100,000 kila taarifa sahihi inayotolewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph anatoa wito kwa wadau wote kushirikiana na Mamlaka hiyo katika kuhakikisha huduma ya maji inakuwa endelevu katika maeneo yote ambayo inahudumia.

Ujenzi wa karavati ya kupitisha bomba chini ya reli ya kisasa (SGR).

Hii ni pamoja na kulipa ankara ya huduma kwa wakati, kutoa taarifa zozote za hujuma dhidi ya DUWASA au wizi wa maji kupitia namba ya huduma kwa wateja bila malipo (Toll free 0800110078) au namba ya WhatsApp 0738 100333.

Pia, wadau na wananchi wanaaswa kutoa taarifa za uvujaji wa maji au ukosefu wa maji kwenye maeneo yao kupitia namba zilizotajwa. Kama hiyo haitoshi, DUWASA kupitia Mtendaji wake, inasisitiza wananchi kusambaza taarifa zinazotolewa na DUWASA kupitia makundi ya WhatsApp kwenda kwa wananchi, hasa kuhusu katizo la maji kwa sababu mbalimbali ikiwemo matengenezo ya miundombinu au kukatika kwa umeme n.k.

Mikakati ya DUWASA ya kuboresha huduma ya majisafi na uondoshaji wa majitaka

Katika jitihada za kuimarisha zaidi huduma ya majisafi na uondoshaji wa majitaka, DUWASA chini ya Wizara ya maji, inatekeleza miradi mbalimbali ya muda ikiwa ni pamoja nakujikita katika mwelekeo wa miradi ya muda wa kati na muda mrefu kama ifuatavyo:

Mipango ya muda mfupia

Kukamilisha miradi yote ya muda mfupi kwa asilimia 100 ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji bila ya kikwazo chochote.b) Kufanya utafiti wa vyanzo vya maji katika maeneo ya NALA, ZUZU na KONGWA kwa kutumia mitambo ya kisasa ya kubaini maji chini ya ardhi na kazi hii imekamilika na uchimbaji wa visima unaendelea.

Mipango ya muda wa kati na mrefua

Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Farkwa. Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) imeonyesha nia ya sehemu ya ujenzi wa Bwawa hilo na miundombinu yake kwa njia ya mkopo wenye masharti nafuu. Awamu ya kwaza ni ujenzi wa Bwawa (Dam Structure) na treatment plant, awamu itakayofuata ni ujenzi wa Bomba lakusafirishia maji maji (transmission main) kwa umbali wa 117Km kutoka Chemba mpaka Tenki la Kilimani.b) Mradi wa Maji kutoka Ziwa Viktoria hadi Dodoma.

Mpango wa muda mrefu ni ujenzi wa mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria hadi Dodoma. Upembuzi wa awali (Pre- Feasibility Study) umefanyika. Wizara ya Maji imetenga fedha kwa ajili Upemuzi yakinifu usanifu wa kina wa mradi huo katika mwaka wa fedha 2021/2022, na taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri (Consultant) zinaendelea chini ya Wizara ya maji.


Mradi wa Ihumwa-Njedengwa kuimarisha huduma ya maji Dodoma

Ile kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya “Kazi Iendelee” imepokelewa kwa mikono miwili na inafanyiwa kazi na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).

Mamlaka hiyo haitaki kusinzia linapokuja suala la huduma za majisafi na majitaka kwa jiji la Dodoma kama ambavyo Mhe. Waziri mwenye dhamana ya maji, Jumaa Aweso naye amekuwa akisisitiza.

Katika moja ya azma zake, DUWASA ikishirikiana na Wizara ya Maji, inaendelea kutekeleza mradi wa maji wa Ihumwa-Njedengwa kupitia mipango ya muda mfupi, ili kuongeza uzalishaji wa maji, na kuboresha usambazaji maji katika Jiji la Dodoma.

Mradi huu unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 2.7 na unatekelezwa na DUWASA kwa mfumo wa Force Account.

Maelezo ya mradi

Mradi huu umehusisha ununuzi na usimikaji wa pampu kubwa mbili (2) za kusukuma maji, ulazaji wa mabomba ya kupeleka maji kwenye tenki yenye urefu wa 11.6 km, ulazaji wa mabomba ya kusambazia maji yenye urefu wa 5.6km kwenda maeneo ya Iyumbu, Njedengwa na Mwangaza, nyumba 300, FFU, stendi kuu ya mabasi, soko la Job Ndugai na eneo la Nzuguni.

Pia umehusisha uendelezaji wa visima, ujenzi wa vibanda vya kuendeshea visima, ujenzi wa kibanda cha mlinzi na Chemba kwenye viungio muhimu vya mabomba.

Maendeleo ya utekelezaji wa mradi

Mradi umekamilika kwa asilimia 99 kwa kuhudumia wakazi wa maeneo ya Njedengwa, sehemu ya Iyumbu, soko la Job Ndugai, stendi mpya, nyumba 300, nyumba za kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) na Nzuguni. Kinachofanyika sasa ni marekebisho madogo madogo ili huduma iendelee kutolewa.