Feed the Children na ndoto ya kuboresha maisha na ustawi wa mtoto Tanzania

Mkurugenzi wa Shirika la Feed the Children Tanzania, Dk Wilbald Lorri akiwa na wanafunzi wa moja ya shule za msingi ambazo shirika hilo linatekeleza miradi yake wilayani Kisarawe

Juni 16 kila mwaka Tanzania huungana na mataifa mengine ya Bara la Afrika huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.

Siku hii ilianzishwa na Umoja wa Afrika kama sehemu ya kuwakumbuka na kutambua mchango wa watoto waliopoteza maisha katika mauaji yaliyotokea Soweto, Afrika Kusini wakati watoto walipoandamana kudai haki zao za msingi.

Shirika la Feed the Children huungana na jamii ya kiafrika kuadhimisha siku hiyo maalumu katika kutambua mchango wa watoto katika jamii, sambamba na kuamsha uelewa wa jamii kwa ujumla katika kutimiza haki na malengo ya watoto.

Katika kulitimiza hilo, Shirika la Feed the Children linatekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo; kutoa huduma za chakula na lishe shuleni, afya na majisafi, uendelezaji wa miundombinu ya shule, mafunzo kwa kamati za shule, mafunzo juu ya ulinzi wa mtoto, uanzishaji na uendelezaji wa vikundi vya kuweka akiba na kukopa (VICOBA) na vikundi vya wakinamama wenye watoto wenye umri chini ya miaka mitano (Care groups), uhamasishaji wa klabu za afya shuleni na utekelezaji wa miradi ya uzalishaji mali shuleni.


Utoaji wa huduma za chakula na lishe shuleni

Elimu ni jambo muhimu kwa mtoto hivyo kwa kulitambua hilo, Feed the Children imeweza kuwafanya watoto kupenda shule kwa kuwapatia hitaji muhimu la chakula ili kuwafanya wasiwaze kitu kingine zaidi ya masomo pale wawapo shuleni.

Mradi huu unatekelezwa na Feed the Children kwenye shule za msingi 28 katika Wilaya ya Kisarawe kwa kushirikiana na kamati za shule,  erikali za vijiji, wazazi na walezi.

Mradi unahusisha utoaji wa unga wa dona ulioongezewa virutubisho pamoja na sukari.Ili kuufanya mradi huu kuwa endelevu Feed the Children imekuwa ikishirikiana na wazazi/walezi na kamati za shule ambapo kwa sasa shirika hilo linatoa chakula hicho siku tatu kwa wiki na siku mbili zinatolewa na wazazi na walezi tofauti na awali ambapo shirika lilitoa chakula kwa siku zote tano za juma.

Shirika limeamua kufanya hivyo ili kuwajengea uwezo wazazi/walezi kuendesha mradi huo baada ya wao kuondoka. Kutokana na mradi huu shirika limeweza kubadilisha mitazamo ya wazazi/walezi juu ya umuhimu wa watoto kula shuleni na sasa suala hilo linatekelezeka na limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya utoro mashuleni na kuongeza ufaulu kwa watoto.

Wanafunzi wa moja ya shule za msingi wilayani Kisarawe waki-saidi kupokea chakula kinachotolewa na Shirika la Feed the Children.

Afya na maji

Katika kusaidia afya na usafi kwa wanafunzi, mwaka wa fedha ujao shirika linatarajia kuwa na mradi mdogo wa kusaidia masuala ya hedhi salama kwa wanafunzi wa kike utakaotekelezwa kwenye Wilaya ya Morogoro vijijini ambapo wasichana zaidi ya 2000 wa shule za msingi watapatiwa taulo za kike zinazotumika zaidi ya mara moja (re-usable sanitary pads).

Pia shirika litaendesha mafunzo mbalimbali ya masuala ya hedhi yatakayoendashwa kwa kushirikiana na ofisi za afya ngazi ya wilaya na maafisa sayansikimu wa wilaya.

Feed the children imekuwa ikitekeleza miradi ya uboreshaji wa miundombinu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za maji kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na wakati mzuri wanapoingia kipindi cha hedhi pamoja na matumizi mengine kwa kujenga mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua.

Feed the Children pia inatekeleza mradi wa kuhamasisha unawaji mikono kwa wanafunzi ambapo wamefanikiwa kujenga vituo vya kunawia mikono vitatu kwenye kila shule katika shule za msingi 30 wiliyani Kisarawe.

Hii imesaidia sana hasa katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 ambapo watoto wamekuwa na muitikio mkubwa wa kusafisha mikono yao mara kwa mara.

Mbali na ujenzi wa vituo vya kunawia mikono, katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa huu shirika liliweza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari na namna ya kujikinga na ugonjwa huo wa corona. Wanajamii waliopatiwa elimu waliwezeshwa vifaa vya kujikingia ili waweze kwenda kutoa elimu kwa wengine; vifaa hivyo ni pamoja na; barakoa (mask) na glovu.


Mafunzo kwa kamati za shule

Kamati za shule ndiyo msingi wa maendeleo ya shule hivyo  ikiwezeshwa na kupewa mafunzo zinasaidia kuboresha mwenendo wa shule kwa kuzingatia kuwa kwenye kamati hizi kuna wawakilishi wa  wazazi/walezi hivyo ni rahisi sana ujumbe kuwafikia na kutekelezwa.

Mafunzo haya yamefanyika katika shule zote 30 kwa kushirikiana na idara ya elimu Wilaya ya Kisarawe na yalihusu kutambua urasimu na umuhimu wa kamati hizi katika maendeleo ya shule na mapokeo yake

yalikuwa mazuri. Ulinzi wa mtoto Kutokana na maadili ya jamii na nyakati tulizopo sasa, ulinzi wa mtoto umekuwa changamoto kubwa, hivyo Feed the children imekuwa ikishirikiana na taaaisi ya C-Sema ambayo inaratibu namba ya bure ya huduma kwa mtoto yaani 116.

Namba hii inatumika kutoa taarifa ili kupata usaidizi wa changamoto yoyote inayohusiana na ulinzi wa mtoto kwa sababu taasisi hii inafanya kazi na Serikali kupitia dawati la jinsia na watoto lililopo katika vituo vya polisi nchi nzima.

Pia, shirika limeshirikiana na C-Sema kwenye mradi wa masanduku ya maoni (happy and sad boxes). Haya ni masanduku yenye sehemu mbili (kitu kinachofurahisha na kinachochukiza) ambayo watoto wanaweka maoni yao kuhusu vitendo ambavyo wanakutana navyo kila siku.

Katika utekelezaji wa programu hii shirika lilipita kwenye shule za msingi na kukutana na wanafunzi, wazazi na walezi na kuwapa elimu ya vitendo vya ukatili na njia za kuripoti vitendo hivyo ili kupatiwa msaada.


Miradi ya uzalishaji mali shuleni

Shirika limeweza kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji mali kama ufugaji wa nyuki, ufugaji wa ng’ombe katika shule za msingi. Lengo la miradi hii ni kuzisaidia shule hizi kutengeneza kipato na kuweza kuendesha mradi wa chakula peke yao kwa kushirikiana na  wazazi/walezi.

Mradi mwingine ni pamoja na kilimo cha maembe ya kisasa. Miradi hii imesaidia kwa kiasi kikubwa shule hizo kuongeza mapato kwa kutumia  elimu ya kujitegemea.


VICOBA na Care groups

Kila jambo linalofanywa na Feed the children linamlenga mtoto hivyo kuboresha uchumi wa familia na jamii ni sehemu ya kuboresha ustawi wa mtoto.

Kutokana na hilo shirika lina ushirikiano na wanajamii katika kata za Wilaya ya Kisarawe na limetengeneza vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA), kutoa mafunzo kwa maofisa wa shirika ambao wanakwenda

kwenye maeneo haya kukutana na wanajamii kwa ajili ya kuwapa elimu ya namna ya kunufaika na vikundi hivi.Care groups ni mradi unahusisha kuhamasisha na kuhimiza mabadiliko ya tabia kwa wazazi/walezi

Wafanyakazi wa Shirika la Feed the Children wakitoa mafunzo ya namna ya kuendesha VICOBA kwa wakazi wa Wilaya ya Kisarawe ikiwa ni juhudi za shirika hilo kuboresha maisha ya wanajamii hao.

katika malezi ya mtoto ili kuboresha afya na ustawi wake, hii inahusisha wazazi/walezi wenye watoto kuanzia mtoto akiwa tumboni mpaka akifikisha miaka mitano, na lengo ni kuweka msingi bora wa afya ya mtoto unaosaidia sana katika maendeleo ya mtoto kwa jumla.

Wito wa Feed the children katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika Jamii inatakiwa kuwa na jumuku la kumlea mtoto.

Tunatakiwa kutambua kwamba mtoto ana haki ya kulindwa na jukumu hili linatakiwa kutekelezwa na jamii nzima. Jamii inatakiwa ueleweshwa kumuona “mtoto kama mtoto” (let a child, be a child). Kukiwa na uelewa mkubwa kuhusu jambo hili itasaidia kupunguza changamoto wanazokutana nazo watoto.Wazazi/walezi wanatakiwa kuwa makini na  matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto maana kwa sehemu kubwa imechangia mmomonyoko mkubwa wa maadili japo kuna faida pia.

Imeandikwa na Jafari Juma, Mwananchi