Franone Mining and Gems LTD (FMG) yasaidia jamii Simanjiro
Kampuni ya Franone Mining & Gem Ltd (FMG) inayochimba madini ya Tanzanite kwenye kitalu C na D, inamilikiwa na wawekezaji wazawa.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Onesmo Mbise anasema yeye na wenzake Francis Matunda na Vitus Ndakize wanamiliki asil-imia 84 na Serikali inamiliki asilimia 16 ya eneo la Kitalu C.
Kwa mujibu wa meneja mkuu wa kampuni ya FMG, Vitus Ndakize kampuni hiyo imetoa ajira rasmi 328 na ajira zisizo rasmi 1,000.
Ndakize anasema ajira zisizo rasmi zimejumuisha wauza bidhaa za chakula na huduma, mama lishe, wachekechaji na madereva wa pikipiki za kubebea abiria (bodaboda).
Kusaidia jamii
Kampuni ya Franone Mining LTD imelenga kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya thamani ya Sh38 milioni kwenye shule ya sekondari ya kidato cha sita ya Naisinyai.
Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD, Onesmo Mbise anataja changamoto zitakazotatuliwa na kampuni hiyo kwa gharama hizo ni kuchimba kisima cha maji, nishati ya umeme wa nyumba ya walimu, bweni la wasichana na bwalo na jiko la kudumu kwani lililopo lipo wazi linaingiza vumbi na kuchafua vyakula.
Mkuu wa shule ya sekondari ya kidato cha sita ya Naisinyai, William Ombay amemshukuru Mbise kwa kupitia kampuni yake kukamilisha baadhi ya changamoto zinazowakabili.
“Tunashukuru kwa kusaidia shule yetu kwani Serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kutimiza mahitaji ya shule ila wadau wa elimu kama ninyi siyo vibaya kusaidia pia,” anasema Mwalimu Ombay.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Laizer anasema watampa ushirikiano wa kutosha mwekezaji mzawa Onesmo Mbise kupitia kampuni ya Franone Mining LTD inayochimba madini ya Tanzanite.
“Hii ni hatua nzuri ya mahusiano mema ya uwekezaji kupitia kampuni yako ya Franone Mining LTD na jamii ya kata ya Naisinyai, tunatarajia tutashirikiana vyema,” anasema Taiko.
Wadau waipongeza kampuni ya Franone
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, hivi karibuni amewaongoza wajumbe 163 wa Baraza la Wawakilishi, Mawaziri watatu na manaibu mawaziri watano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutembelea mgodi wa kampuni ya Franone Mining LTD eneo la kitalu C.
Naibu Spika Mgeni, akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameongoza msafara huo kutembelea mgodi wa Kitalu C wa kampuni ya Franone Mining and Gems LTD uliopo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo ameipongeza kampuni ya Franone Mining and Gems LTD pamoja na uwekezaji wao pia kwa kutoa ajira 328 wakiwemo wanawake.
Anasema wamejifunza mengi ikiwemo uchimbaji wa madini ya Tanzanite unavyofanyika na kuona ukuta unaozunguka migodi ya madini hayo uliojengwa kipindi cha uongozi wa hayati John Magufuli.
"Kule Zanzibar tunazungumzia uchumi wa bluu kupitia bahari, tumekuja hapa Franone na kujifunza namna uchumi wa migodi unavyonufaisha Watanzania hasa wanawake," anasema Spika Mgeni.
Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, Onesmo Mbise amewakaribisha wageni hao na kusema kuwa wanaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwaamini wawekezaji wazawa hadi kuwakabidhi kitalu C.
Wakuu wa Wilaya za Ruangwa, Hassan Ngoma na Nachingwea Mohamed Moyo mkoani Lindi, nao hivi karibuni wamewaongoza baadhi ya viongozi wa Wilaya zao, kutembelea na kuingia ndani ya mgodi wa Franone Mining and Gems.
Ngoma, Moyo na baadhi ya viongozi hao wamezama chini ya mgodi wa mwekezaji mzawa, kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, eneo la kitalu C na kujionea shughuli za uchimbaji madini zinavyofanyika.
Akizungumza baada ya kuingia kwenye mgodi huo, Ngoma anasema lengo la ziara yao ni kujifunza namna shughuli za uchimbaji madini ya Tanzanite unavyofanyika ili nao waige mazuri.
"Tumeona shughuli za uchimbaji kwa mwekezaji mzawa kampuni ya Franone kwa kweli wanastahili pongezi kwa kufanya kazi kwa ufanisi," anasema Ngoma.
Anasema wilaya yao ya Ruangwa pia kuna uwekezaji mkubwa wa baadhi ya migodi hivyo kupitia uwekezaji wa kampuni ya Franone Mining wamejifunza kupitia madini ya Tanzanite.
"Uwekezaji uliopo hapa Franone, unapaswa kupongezwa kwani tumeshuka chini ya ardhi mgodini mita 700 kisha tukamaliza kilomita 1.2 tumeshuhudia kazi nzuri," anasema Ngoma.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo ambaye naye alizama kwenye mgodi huo ameipongeza kampuni ya Franone LTD kwa kuweka miundombinu thabiti ya uchimbaji madini ya Tanzanite.
"Watanzania wanaweza tumeona vijana wamepata ajira kwenye kampuni ya Franone na tunampongeza hayati John Magufuli kwa kujenga ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite," anasema Moyo.
Diwani wa viti maalum Tarafa ya Moipo, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Paulina Makaseni ameipongeza kampuni ya Franone Mining kwa kutoa kipaumbele kwa wanawake wanaochekecha kwa kuwapa mchanga.
Diwani huyo Paulina anasema wamiliki wa migodi, wachimbaji na wadau wa madini ya Tanzanite wanapaswa kuiga mfano wa kampuni ya Franone inavyowajali wanawake.
“Tunawashukuru viongozi wa kampuni ya Franone hususani Mkurugenzi wake Onesmo Mbise kwa kuwapa mchanga wanawake wachekechaji ili wajitafutie riziki zao,” anasema Diwani Paulina.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wanawake wachekechaji kupendana na kuwa na umoja katika shughuli zao ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na waepuke migogoro na migongano.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM (UWT) Kata ya Endiamtu, Claudia Dengesi anasema hatua ya kampuni ya Franone kuwapa mchanga wanawake hao inapaswa kupongezwa kwani inawanyanyua kiuchumi.
“Wanawake hivi sasa ndiyo wanalea familia zao hivyo tumpongeze Mkurugenzi wa Franone, Onesmo Mbise kwa kuwasaidia kina mama hao wachekechaji,” anasema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM (UWT) Kata ya Mirerani, Johari Mwaselela amewaomba wamiliki wa migodi ya Tanzanite waige mfano wa kampuni ya Franone kwa kutoa mchanga wenye mabaki mengi ya madini.
Mwaselela anasema wamiliki hao wakiwapa wanawake hao udongo uliotoka kwenye buti hawatakuwa wanafanya jambo sahihi hivyo waige mfano wa Mkurugenzi wa Franone Onesmo Mbise.
Kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd, pia imekipatia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Simanjiro Sh30 milioni kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa chama hicho.
Kutokana na hali hiyo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Ormemei Laizer ameipongeza kampuni ya Franone Mining LTD kwa kuwapatia kiasi hicho cha Sh30 milioni za ujenzi wa ukumbi huo wa chama hicho.
Kiria anasema kitendo cha kampuni hiyo kuchangia Sh30 milioni za ujenzi wa ukumbi wa chama hicho kinastahili pongezi kubwa kwani wameonyesha moyo wa upendo kwa CCM.
“Kwa niaba ya CCM Wilaya ya Simanjiro, pokea salamu za asante na ninakushukuru kwa kutuunga mkono katika ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa chama chetu na tutaipatia kampuni hiyo cheti cha shukrani,” anasema Kiria.
Anasema Mkurugenzi wa FMG Onesmo Mbise ameonyesha mfano mkubwa kwa wawekezaji waliopo kwenye Wilaya ya Simanjiro katika kukiunga mkono chama hicho hivyo anastahili pongezi.
Pia, Meneja wa FMG Vitus Ndakize anasema pia wapo kwenye mpango wa ujenzi wa korido ya njia ya kuingia na kutoka kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti (mochwari) ya kituo cha afya Mirerani ila wanasubiri orodha ya mahitaji ya manunuzi ya ujenzi (BOQ) kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.
“Katika miradi ambayo tunataka kuitekeleza tunasubiria Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, atupatie barua atuambie kipaumbele cha kusaidia jamii katika eneo lake,” anasema Ndakize.
Vilevile, Meneja wa FMG Vitus Ndakize anasema pia wametoa Sh47 milioni kwa ajili ya ujenzi wa korido ya njia ya kuingia na kutoka kwenye nyumba ya kuhifadhi maiti (mochwari) ya kituo cha afya Mirerani."Pia kampuni ya Franone tunatekeleza agizo la Waziri wa Madini Dk Dotto Biteko alilolitoa hivi karibuni mji mdogo wa Mirerani juu ya matengenezo ya barabara ya kuelekea mgodini tumetenga Sh171 milioni kwa ajili ya matengenezo tunasubiria mkandarasi wa ujenzi apatikane ili uanze," anasema.
Waziri wa Madini aipongeza Franone
Waziri wa Madini Dk Dotto Biteko ameipongeza kampuni ya wawekezaji wazawa Franone Mining and Gems Company LTD, inayochimba madini ya Tanzanite eneo la kitalu C Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa namna inavyofanya kazi kwenye eneo hilo.
Waziri Dk Biteko ameyasema hayo kwenye ziara yake mji mdogo wa Mirerani, hivi karibuni alipofika kuzungumza na wadau wa madini ya Tanzanite, kutembelea kitalu C na kukagua ujenzi wa jengo la soko la madini la Tanzanite City.
Anasema kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd, baada ya kushinda tenda na kukabidhiwa eneo la kitalu C, imefanya kazi kubwa kwa muda mfupi, kinyume cha matarajio ya watu wengi.
“Tumepata mwekezaji bora kabisa kwani aliahidi kuwa ataanza uzalishaji miezi 18 baada ya kupewa leseni ila ndani ya miezi sita ameweza kufanikisha uzalishaji tofauti na malengo ya awali,” anasema Dk Biteko.
Anasema kampuni ya Franone imeanza uzalishaji wa madini ya Tanzanite kwenye kipindi ambacho Serikali inahesabu kuwa wapo kwenye usafi na kutengeneza miundombinu ya uchimbaji.
“Kampuni ya Franone Mining ilipewa mgodi ukiwa umechakaa, wakati akifanya ukarabati wa miundombinu yake ya kazi, wao wameshaanza uzalishaji, wanastahili pongezi,” anasema Dk Biteko.
Anasema kampuni ya Franone imetoa ajira kwa watu 328 kwa muda mfupi na bado wapo kwenye ujenzi wa miundombinu na Serikali inakusanya kodi kwenye madini, inapata kodi kwenye ajira hivyo iungwe mkono.
“Ni kawaida yetu tunapomuona mwekezaji ni mweusi kama sisi tunadharau badala ya kumuunga mkono, mpeni ushirikiano Mtanzania mwenzetu na pia kuna mama wa kimasai anasema mngeleta mgeni nisingeweza kuzungumza naye kiingereza ila Onesmo Mbise hata kimasai anasikia kidogo,” anasema Biteko.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera ameipongeza kampuni ya Franone kwa namna inavyosaidia ajira kwenye maeneo yanayozunguka madini ya Tanzanite.
“Pamoja na hayo, wanawake mnaopatiwa udongo wekeni utaratibu wenu vizuri ili msiwe mnagombania huo mchanga na pia vijana mnaowasumbua kina mama wanapokuwa na udongo acheni mara moja,” anasema Dk Serera.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka ameipongeza kampuni ya Franone kwa kushinda zabuni ya kuchimba madini ya Tanzanite, eneo la kitalu C.
“Ni kampuni iliyoshinda kwa sifa stahiki na wanastahili kupewa ushirikiano katika kutimiza malengo yao ya uwekezaji wa machimbo ya madini ya Tanzanite,” anasema Ole Sendeka.
Mmoja kati ya wanawake wanaosuka kamba za manila kwenye kampuni hiyo, Nai Leyani amemshukuru mkurugenzi wa kampuni hiyo Onesmo Mbise kwa kuwapa ajira.
“Kwa kweli tunamshukuru Mungu kwa kupata ajira kwani hivi sasa, tunasaidiana na wanaume zetu, katika kuhudumia na kutunza familia zetu majumbani kutokana na ajira ya Franone,” anasema Nai.
Mwenyekiti wa wanawake wachekechaji Nadoiwoki Julius, anasema kampuni ya Franone Mining imewasaidia makundi manne ya wanawake, walemavu, wazee na vijana wanaochekecha udongo.
“Tuna imani kubwa na wewe Onesmo Mbise, ila tunaomba tuongezewe udongo, kwani tupo wengi na udongo ni mchache na pia nafasi za ajira zikitokea wanawake tusisahaulike,” anasema Nadoiwoki.
Franone wamshukuru na kupongeza Rais Samia
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, Onesmo Mbise amemshukuru na kuipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna walivyokuwa na imani kubwa na wachimbaji wazawa hadi kukubaliwa wao kuwekeza.
“Imani huzaa imani, kutokana na imani kubwa tuliyopewa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan nasi tunatoa ahadi kuwa tutatekeleza wajibu wetu ipasavyo ili kulinda heshima tuliyopewa,” anasema Mbise.
Franone yazawadiwa
Kutokana na kampuni ya FMG kutoa udongo wa kuchekecha kwa makundi maalum ya wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Onesmo Mbise amepatiwa zawadi ya mbuzi, rungu ya heshima ya kiongozi wa kimila (mshili) na blanketi na shuka.
Diwani wa viti maalum wa tarafa ya Moipo, Paulina Makeseni anasema zawadi hizo ni upendo kwa wanawake wanaofanya kazi ya kuchekecha mchanga wenye mabaki ya madini ya Tanzanite, yanayotolewa na kampuni ya Franone.
“Hivi sasa uchumi wa wanawake hawa ni mzuri hivyo wakaona wanunue zawadi hizi ndogo ili iwe shukurani kwao na wewe utambue furaha yao kutokana na msaada mkubwa uliowapatia,” anasema Makeseni.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer akimkabidhi Onesmo Mbise rungu ya heshima ya kiongozi wa kimila (mshili) anasema wanawake hao wamemshirikisha jambo lao naye kwa nia ya dhati akashiriki kutokanana tukio hilo kubwa kwani kampuni hiyo imewawezesha kiuchumi wanawake hao.
“Nilikuwa na majukumu mengine ya kikazi ila nilipomaliza na kupata taarifa ya jambo hili nikaamua nije tushiriki pamoja, kwani mtu anaposema asante nasi tunapaswa kushukuru,” anasema Taiko.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) Kata ya Mirerani Claudia Dengesi (Mama Sonjoo) anasema wanawake hao wametoa shukrani zao kutokana na kampuni ya FMG kuwajali wakina mama.
“Tunapaswa kumshukuru mno Mkurugenzi wetu Onesmo Mbise kwani ni mtu ambaye ana utu na kuwajali wanawake, pamoja na wazee na watu wenye ulemavu,” anasema Claudia.