GBT imeleta mapinduzi kwenye tasnia ya michezo ya kubahatisha, kuchangia uchumi na maendeleo

Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (2017 hadi sasa ), James Mbalwe.

Muktasari:

Michezo ya kubahatisha ni moja ya tasnia zinazokua kwa kasi duniani hususani katika nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.

Michezo ya kubahatisha ni moja ya tasnia zinazokua kwa kasi duniani hususani katika nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.

Kwa sehemu kubwa, michezo hii ni burudani maridhawa kwa jamii lakini pia ni chanzo cha mapato ya Serikali. Kama ilivyo katika nchi nyingine duniani, sambamba na ukuaji wa tasnia hiyo, Tanzania imeshuhudia pia mchango mkubwa wa tasnia ya michezo ya kubahatisha katika uchumi na maendeleo ya jamii.

Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, tasnia hiyo imekuwa moja ya maeneo yanayochangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Serikali kwa njia ya kodi pamoja na kutoa ajira.

Mkurugenzi Mkuu, Bahati Nasibu ya Taifa (1995 - 2003), Muasisi na Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (2003 - 2017), Tarimba Abbas.

Ukuaji wa tasnia hii, pamoja na mambo mengine, umechangiwa zaidi na uwepo wa chombo mahsusi cha kusimamia tasnia hiyo ambacho ni Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).

Ikiwa na miaka 18 ya kusimamia tasnia hiyo tokea kuanzishwa kwake baada ya kufutwa kwa lililokuwa shirika la Bahati Nasibu ya Taifa (BNT), GBT imeleta mapinduzi makubwa na kuifanya tasnia ya michezo ya kubahatisha kuwa moja ya maeneo muhimu katika kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu na maendeleo ya jamii. Gazeti hili lilipata nafasi ya kufanya mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa GBT, James Mbalwe ambaye alieleza safari ya GBT katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru na namna ilivyojipanga kuhakikisha kuwa tasnia ya michezo ya kubahatisha inaendelea kuwa imara na yenye kuaminika.

Tueleze safari ya Michezo ya Kubahatisha nchini katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru

Michezo ya kubahatisha nchini ilikuwepo tangu enzi za mkoloni, kwenye miaka ya 1950. Wakati huo, michezo hii ilitumika kama njia ya kukusanya pesa kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii kama vile ujenzi wa zahanati na shule.

Baada ya ukoloni michezo hii iliendelea kuwepo hususan Bahati Nasibu ya Taifa ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa Sheria ya Pools and Lotteries Act ya mwaka 1967 na baadae Sheria ya Taifa ya Bahati Nasibu ya Mwaka 1974.

Pamoja na kuendesha biashara ya michezo ya bahati nasibu, Shirika la Bahati Nasibu ya Taifa lilipewa pia jukumu la kusimamia na kudhibiti waendeshaji wa michezo mingine ya kubahatisha.

Hali hii ilisababisha mgongano wa kimaslahi kwa kuwa shirika lenyewe pia lilikuwa likifanya biashara hiyo iliyopewa jukumu la kuidhibiti.

Mkurugenzi Mkuu Bahati Nasibu ya Taifa (1974 - 1995), Muhammed Mussa Dassu (marehemu).

Sekta ya michezo ya kubahatisha haikuachwa nyuma na mageuzi ya kiuchumi nchini yaliyoanza kwenye miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Kufuatia mageuzi hayo, tasnia ilipitia katika mabadiliko makubwa ambapo katika mwaka wa 2003, Sera ya Taifa ya Michezo ya Kubahatisha ilitungwa ikifuatiwa na Sheria ya Bunge Sura Na. 4 ya Mwaka 2003 (Gaming Act No. 4 of 2003).

Sheria hii ilifuta lililokuwa Shirika la Bahati Nasibu ya Taifa (BNT) na kuunda Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (Gaming Board of Tanzania; (GBT).

Tofauti na BNT ambayo ilikuwa ikifanya kazi ya udhibiti na wakati huo huo ikiendesha michezo ya Bahati Nasibu, GBT yenyewe imepewa jukumu la kusimamia, kuratibu na kudhibiti uendeshaji wa tasnia ya Michezo ya Kubahatisha nchini na haijihusishi na uendeshaji wa michezo hiyo.

Mabadiliko haya yaliwezesha sekta kuratibiwa vizuri zaidi na hivyo kuweza kuchangia vema katika uchumi wa nchi.

GBT ina Majukumu gani?

GBT ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi zake chini ya Wizara ya Fedha na Mipango. Majukumu ya GBT yameainishwa katika kifungu cha 7 cha Sheria ya Michezo ya Kubahatisha ambapo jukumu kubwa na la msingi ni kusimamia na kuratibu uendeshaji wa tasnia ya michezo ya kubahatisha nchini. Jukumu hili la GBT linahusisha kazi kubwa zifuatazo:

• Kutoa leseni za kuendesha michezo ya kubahatisha nchini. GBT ndiyo chombo pekee kilichopewa jukumu la kisheria la kutoa leseni za kuendesha michezo ya kubahatisha zinazowafanya waendeshaji kufanya shughuli zao kihalali hapa nchini.

• Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa waendeshaji wa shughuli za michezo ya kubahatisha nchini ili kuhakikisha kuwa wanafuata sheria za uendeshaji wa michezo hiyo.

• Kushauri Serikali kuhusiana na masuala ya kodi zitokanazo na michezo ya kubahatisha na namna bora ya ukusanyaji wake. Kimsingi, GBT ndiyo mshauri mkuu wa Serikali kuhusiana na mambo ya kodi, ada na tozo mbalimbali zitokanazo na michezo ya kubahatisha.

• Kazi nyingine zimejumuisha kuweka viwango vya kiufundi katika uendeshaji wa michezo ya kubahatisha (Technical Standards), kusimamia ushindani wa haki na kutatua migogoro inayotokea kati ya waendeshaji na wachezaji wa michezo hii.

• Kufanya mambo mengine mbalimbali yanayowezesha sekta kukua na kudhibitiwa ipasavyo ili kuwezesha kuchangia katika mapato ya Serikali huku ikilinda maslahi ya jamii kwa mapana yake; kwa mfano kuzuia ushiriki wa watoto, kuhakikisha hakuna udanganyifu katika uendeshaji, kuhakikisha michezo inaendeshwa katika maeneo maalum yanayoruhusiwa kisheria na kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na uwepo wa michezo hii kama uraibu.

Ni nini hasa dhana ya Michezo ya Kubahatisha?

Dhana kuu ya michezo ya kubahatisha ni ‘burudani’ kama zilivyo aina nyingine za burudani ambapo watu hucheza ili kujifurahisha.

Jamii inapaswa kufahamu kwamba michezo ya kubahatisha sio njia ya kumuondolea mtu matatizo yake ya kifedha au kiuchumi na kwamba sio moja ya vyanzo vya fedha vya kuaminika katika kukidhi mahitaji ya kila siku.

Kwa wanaofahamu dhana ya bahati nasibu, hucheza huku wakijua fika kuwa, michezo hii ni burudani, hivyo hawatumii fedha za ziada kwa ajili ya michezo hiyo na hivyo kutokutoa nafasi ya madhara kujitokeza kama vile kuzisahau au kushindwa kuzihudumia familia zao, kuingia katika madeni au kusababisha uzembe kazini.

Totauti kubwa ya michezo ya kubahatisha na burudani nyingine ni suala la matumaini ya kupatikana kwa zawadi kwa washiriki wake. Hata hivyo, ni lazima jamii na hasa wachezaji waelewe kuwa, kushinda zawadi katika mchezo wowote ule wa bahati nasibu unatokana na ‘bahati’ na si vinginevyo.

Kwa maana hiyo, ingawa uwezekano wa kupata zawadi upo, watu hawatakiwi kushiriki kwa minajili ya kukimbiza bahati bali kujaribu kupata bahati hiyo. Hivyo basi, endapo mtu atashinda anatakiwa atumie pesa au aina yoyote ya zawadi aliyopata vizuri ili kujiletea maendeleo na kuboresha hali ya maisha, na endapo hatoshinda basi aridhike na ajaribu bahati yake wakati mwingine.

Kuna msemo kwenye tasnia hii usemao ‘mabingwa wanajua wakati wa kuacha kucheza’. Hivyo watu wacheze kwa kiasi kulingana na uwezo wao wa kifedha na bila kusahau majukumu na mahitaji yao ya msingi, kwa kuwa michezo hii ni burudani na haipaswi kuleta madhara ya aina yoyote ile.

Michezo ya bahati nasibu pia huweza kutumika kwa malengo maalum ikiwa ni pamoja na kuhamasisha biashara, kukusanya fedha kwa ajili ya malengo maalum ya kijamii kama kujenga shule, zahanati au miradi mingine ya kijamii.

Aina hii ya bahati nasibu huendeshwa na makampuni au vikundi tofauti katika jamii ili kuweza kufikia malengo yao.

Kuna aina ngapi za michezo ya kubahatisha hapa Tanzania ambayo inasimamiwa na GBT?

Sheria imeainisha michezo tofauti tofauti ambayo imegawanyika katika makundi makuu mawili yaani kundi la michezo ya kibiashara na ile isiyo ya kibiashara.

Kundi la michezo ya kibiashara linajumuisha michezo ya Kasino (za kwenye majengo maalum na za mtandaoni (Landbased and Online Casino), michezo ya kubashiri matokeo (sports betting), ambayo nayo inachezwa kupitia mfumo wa kawaida na mtandaoni, michezo ya kwenye Mashine za sloti kwenye maduka maalum (slots mashines shops) ama kwenye baa. Pia kundi hili la michezo ya kibiashara linajumuisha pia Bahati Nasibu ya jumbe fupi za simu za mkononi (SMS Lottery), Bahati Nasibu za kuchagua namba (Number Game) pamoja na Michezo ya Vikaragosi (virtual games).

Kundi la pili ni lile la michezo isiyokuwa ya kibiashara ambayo ni pamoja na bahati nasibu ya kuhamasisha biashara (promotional lottery) ambayo huendeshwa na makampuni mbalimbali kwa lengo la kutangaza huduma au bishara zao.

Vilevile, kuna bahati nasibu za kijamii (public lottery) ambapo vikundi mbalimbali katika jamii wanaweza kuanzisha kwa lengo la kupata fedha ya kufadhili kazi/mradi maalum. Bahati nasibu za kundi hili huwa ni za muda maalum na siyo za kudumu kwa muda mrefu kama zile za kibiashara.

Kati ya aina hizo za michezo ya kubahatisha, zinazolipa kodi ni zile za kibiashara pekee kama zilivyoainishwa hapo awali.

Utaratibu wa kutoa leseni za uendeshaji wa michezo ya kubahatisha uko vipi?

Kimsingi, kazi kubwa ya GBT ni kutoa leseni za michezo ya kubahatisha kwa mujibu wa Sheria. Kwa kiasi kikubwa utoaji wa leseni za michezo ya kubahatisha unatofautiana sana na utoaji wa aina nyingine za leseni kama vile za udereva ama biashara zingine. Hii ni kutokana na upekee wa tasnia yenyewe.

Hatua ya kwanza, baada ya kupokea maombi ya leseni, kabla hatujatoa uamuzi wa aidha kutoa au kutotoa leseni, ni kufanya upekuzi wa kina (background check) ili kufahamu historia ya muombaji, kujua anapotoka na kama ana historia yoyote ya kujihusisha na makosa ya jinai.

Baada ya hapo tunakagua chanzo cha fedha zake, ili kusiwe na uwezekano wa matumizi ya fedha haramu na pia tunaangalia fedha alizonazo (mtaji) kama zinatosha kufanya biashara anayoombea leseni.

Kitu kingine tunachokiangalia ni kama mwombaji ana teknolojia ya kisasa ya kuendesha biashara anayoombea leseni pamoja na uzoefu na ujuzi wa biashara ya michezo ya kubahatisha na pia watu anaoshirikiana nao.

Vile vile, upekuzi huu unajumuisha kupata taarifa za polisi (criminal record) ya muombaji pamoja na nyaraka za usajili wa kampuni ya muombaji/waombaji kutoka mamlaka husika.Baada ya kufanyika kwa upekuzi huu na endapo GBT ikijiridhisha kuwa muombaji yuko safi, ndipo atapatiwa leseni na kinyume chake hatopatiwa leseni.

Kwa mujibu wa Sheria, gharama zote za zoezi la upekuzi hulipwa na muombaji wa leseni husika na hazirudishwi hata kama muombaji hatopewa leseni.

Lengo la kufanya upekuzi na kuweka vigezo hivi ni kuhakikisha kuwa, ni watu safi tu (suitable) ndiyo wanaoingia katika tasnia ya michezo ya kubahatisha, ili kudhibiti na kuzuia vitendo vya udanganyifu ambavyo vinaweza kuikosesha Serikali mapato pamoja na kupotea kwa haki za wachezaji na kusababisha migogoro ya mara kwa mara na hivyo kuharibu taswira ya tasnia ya michezo hii nchini.

Dira ya GBT ni kuwa Mdhibiti wa kiwango cha kimataifa wa michezo ya kubahatisha ili kuchangia ukuaji wa uchumi, je ni kwa kiasi gani GB metimiza dira yake hii?

Kupitia utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria, GBT imeweza kutimiza dira yake kwa kuweza kuchangia katika ukuaji wa tasnia ya michezo ya kubahatisha nchini ambayo imekuwa chachu ya kuongezeka kwa kodi na mapato mengine ya Serikali pamoja na kutengeneza ajira.

Mwaka 2003 wakati GBT inaanzishwa kulikuwa na waendeshaji wa michezo ya kubahatisha wasiozidi sita (6) na aina mbili (2) tu za michezo ya kubahatisha ambayo ni Kasino na Mashine za Sloti, lakini mpaka sasa kuna waendeshaji wa kibiashara ambao wanalipa kodi wapatao sitini na nne (64) na zaidi ya aina tano za michezo ya kibishara.

Ongezeko hili la waendeshaji, limechangia katika utoaji ajira, ambapo kwa sasa tasnia imetengeneza ajira za moja kwa moja kwa Watanzania zaidi ya 20,000, huku ikitegemewa na watu wengi kama sehemu ya kuendesha maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wa mapato, GBT imewezesha tasnia hii kuongeza ulipaji wa kodi serikalini ambapo mapato yamekuwa yakiongezeka kwa kiwango kikubwa mwaka hadi mwaka.

Mathalan, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kuanzia Julai 2016 hadi Juni 2021, jumla ya kodi iliyolipwa serikalini kutokana na uendeshaji wa michezo ya kubahatisha nchini ilifikia Sh. bilioni 428.9.

Katika mwaka 2016/17 mapato yalikuwa Sh. bilioni 33.6, mwaka 2017/18 yalikuwa Sh. bilioni 78.7 na mwa-ka 2018/19 yalikua Sh bilioni 95.1. Mapato yalishuka kidogo katika mwaka 2019/20 kutokana na mlipuko wa janga la Uviko-19 ambao ulichangia kudorora kwa biashara na michezo na mapato yalikuwa Sh bilioni 89.5.

Katika mwaka 2020/21 mapato yaliongezeka na kufikia Sh bilioni 132. GBT imedhamiria kuendelea kuisimamia vema tasnia hii ili, pamoja na faida nyingine, Serikali iendelee kupata mapato makubwa zaidi kila mwaka.

Pamoja na ongezeko la makusanyo ya kodi, GBT pia imeweza kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa kutoa gawio kwa Serikali kutokana na faida inayopatikana.

Maendeleo yote haya ya tasnia hii yametokana na ubunifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu ya GBT pamoja na kukumbatia teknolojia ya kisasa katika uendeshaji wa michezo ya kubahatisha nchini.

Ili kuhakikisha tasnia inaendelea kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi, GBT imehakikisha inatoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa tasnia hiyo katika kusaidia juhudi za kukuza uchumi na maendeleo ya jamii katika nyanja mbalimbali kama vile michezo n.k.

Tunaamini kwamba wadau wakiwa na uwelewa sahihi kuhusu tasnia hii wataifanya kuwa endelevu na hivyo kuiwezesha kuchangia zaidi kwenye kukuza uchumi huku wakiepuka madhara ya kijamii yanayoweza kutokea kutokana na uwepo wake.

GBT pia imehakikisha inaweka mazingira mazuri ya kibiashara kwa waendeshaji na wachezaji wa michezo ya kubahatisha ili kuondoa vikwazo na kuhakikisha kila upande unapata inachostahili.

Mazingira mazuri yamewawezesha waendeshaji kupata faida kutokana na biashara zao na hivyo kuendelea kulipa kodi na pia wachezaji wanapata burudani pamoja na kipato kinachotokana na kucheza kwao, pale inapotokea.

Vile vile uwepo wa mazingira mazuri ya biashara na udhibiti wa sekta, umeendelea kuisaidia Serikali kupata kodi inayotokana na tasnia hiyo ipasavyo.

Ni kwa kiasi gani GBT inatumia teknolojia katika kazi zake? Kama nilivyosema awali kwamba moja ya mambo yaliyoleta mafanikio makubwa kwa GBT na tasnia kwa ujumla ni kukumbatia teknolojia ya kisasa katika uendeshaji na udhibiti wa michezo ya kubahatisha.

Matumizi ya teknolojia yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mapinduzi ya tasnia ya michezo ya kubahatisha nchini na GBT tumedhamiria na tunatarajia kwa siku za usoni, tufikie asilimia 100 ya matumizi ya teknolojia katika uendeshaji na usimamizi wa shughuli zote za michezo ya kubahatisha nchini.

Kwa sasa tumeweza kuweka mifumo mbalimbali ya kielektroniki kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa majukumu yetu.

Katika kutekeleza jukumu mama la kutoa leseni za uendeshaji wa michezo ya kubahatisha, tunatumia mfumo unaojulikana kama Gaming Licensing Inspections and Compliance Application (GLICA) ambapo kazi na taratibu zote za leseni, ukaguzi na usikilizaji wa malalamiko zinafanyika kwa njia ya kielektroniki kupitia mfumo huu.

Kupitia mfumo huu, muombaji anaweza kuomba leseni mahali popote alipo duniani hivyo kurahisisha muda na gharama za maombi na mchakato wa leseni.

Mfumo mwingine ambao uko kwenye hatua za mwisho za kukamilika unaitwa Gaming Regulatory Monitoring System (GReMS). Mfumo huu utakapokamilika utasaidia kusimamia shughuli zote za michezo ya kubahatisha kwa kuunganishwa na waendeshaji popote walipo nchini. Mfumo huu utatumika katika kuratibu miamala inayofanyika katika biashara ya michezo ya kubahatisha.

GBT pia ina mifumo ya ndani kama vile mfumo wa utunzaji taarifa na nyaraka ambao unatusaidia kwenye shughuli zetu za kila siku.

Tunaamini kwamba kwa kutumia teknolojia za kisasa tutaweza kuongeza ufanisi katika usimamizi wa tasnia hii ya michezo ya kubahatisha na kuweza kufikia Dira yetu na pia kuongeza mchango wa tasnia katika kukuza uchumi wa nchi yetu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Mafanikio ya GBT

Tangu kuanzishwa kwake miaka 18 iliyopita GBT imeweza kupata mafanikio makubwa yafuatayo: -

• kuifanya tasnia kuwa tulivu na salama, hivyo kuvutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi.

• Kukua kwa mchango wa tasnia katika ukuzaji wa uchumi kwa kuchangia mapato ya Serikali yatokanayo na kodi,

• Kuzalisha ajira; zilizo rasmi na zisizo rasmi.

• Imesaidia kuleta uwekezaji kutoka nje (foreign direct investment).

• Imechangia katika kuleta fedha za kigeni nchini.

• Imechangia katika kuletwa kwa teknolojia mpya.

• Imekuwa chachu ya ukuaji wa biashara nyingine kwa njia ya promosheni,

• Imesaidia kuongeza mzunguko wa rasilimali fedha,

• Imekuza tasnia ya michezo kutokana na udhamini wa timu mbalimbali na kuongeza hamasa ya watu kufuatilia mashindano mbalimbali duniani, na pia,

• Imesaidia kukuza tasnia nyingine za kiuchumi kama sekta ya utalii.GBT tutaendelea kuunga mko-no juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kujenga uchumi wa nchi yetu na kuleta maendeleo kwa watu wake.

Tanzania Salama, Kazi Iendelee.