GGML yatoa Sh200 milioni kudhamini Maonyesho ya Saba ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita
Geita Gold Mining Limited (GGML), kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti, imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania kwa mara nyingine tena, kwa kudhamini Maonyesho ya Saba ya Teknolojia ya Madini Geita kwa kutoa mchango wa Sh 200 milioni.
Maonyesho haya yanatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 2 hadi 13, 2024, na yatatoa fursa kwa GGML kuonyesha uvumbuzi wake wa kiteknolojia, uzingatiaji wa maudhui ya ndani, na uwekezaji wake wa kijamii kupitia miradi mbalimbali ya Uwajibikaji kwa Jamii wa Kampuni (CSR).
Aidha, maonyesho haya yatafunguliwa rasmi Oktoba 5, 2024 na Dk Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambaye ameonyesha uongozi imara katika sekta ya madini nchini. Hafla ya kufunga maonyesho hayo itafanyika Oktoba 13, 2024, ambapo Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Maonyesho haya ya kila mwaka yanayoandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), yanatazamiwa kuwa jukwaa muhimu la kibiashara linalokutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini na sekta nyingine zinazohusiana.
Washiriki wa maonyesho haya wanapata fursa ya kujadili changamoto, uvumbuzi, na fursa za kiuchumi zinazojitokeza, huku pia wakishuhudia jinsi kampuni kama GGML inavyochangia maendeleo endelevu ya Taifa kupitia teknolojia na uwekezaji wa ndani.
Gilbert Mworia, Meneja Mwandamizi wa Uendelevu wa GGML, alisema, "GGML imekuwa mdau muhimu katika maonyesho haya ya Teknolojia ya Madini kwa miaka saba mfululizo, na tuna furaha kubwa kushiriki tena mwaka huu.
Mchango wetu kwenye maonyesho haya sio tu msaada wa kifedha, bali pia tunalenga kuimarisha mahusiano yetu na wadau wakuu kama vile Serikali za mitaa, wachimbaji wadogo, na biashara za ndani. Tunaamini kuwa teknolojia bora na ushirikiano wa kweli vinaweza kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya madini."
Kupitia mpango wake wa urudishaji kwa jamii, GGML inatekeleza miradi mbalimbali inayoimarisha jamii za Geita na maeneo jirani. Mradi wa ujenzi wa viwanja vya Maonyesho ya EPZA huko Geita ni mojawapo ya miradi mikubwa iliyofadhiliwa na GGML ambao unalenga kubuni miundombinu inayochochea ukuaji wa kiuchumi katika sekta mbalimbali. Maeneo hayo yatatumika kwa shughuli za kibiashara na teknolojia kwa miaka mingi ijayo, huku yakifungua milango kwa wawekezaji na wabunifu wapya.
Kwa mujibu wa dira yake ya muda mrefu, GGML inaunga mkono kikamilifu jitihada za Serikali ya Tanzania za kukuza uchumi wa madini. Hii ni sambamba na lengo la Serikali la kuhakikisha sekta ya madini inachangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.
Ushiriki wa GGML katika maonesho haya ni ishara ya wazi ya azma yake ya kusaidia kufanikisha lengo hili kwa kutumia teknolojia za kisasa na kutoa fursa za ajira na mafunzo kwa Watanzania.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, GGML imeendelea kuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya jamii inayozunguka mgodi wa Geita.
Kupitia miradi mbalimbali ya CSR, GGML imewekeza katika sekta za afya, elimu, miundombinu, na ujasiriamali, huku ikilenga kuboresha maisha ya Watanzania na kuleta mabadiliko endelevu. Hii inaonyesha kuwa kampuni hiyo inabaki kuwa kielelezo bora cha uwajibikaji wa kampuni na mshirika wa kweli wa maendeleo kwa Tanzania.