Habaki mtu nyuma: mikakati minne ya uboreshaji mifumo ya chakula nchini

Mwakilishi wa FAO Tanzania, Dk Nyabenyi Tipo

Muktasari:

  • Uzalishaji bora, mazingira bora, lishe bora na maisha bora kwa wote

Dk Nyabenyi Tipo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mataifa mengine duniani kwa mara nyingine wameadhimisha siku ya chakula duniani Oktoba 16. Sherehe hizo kitaifa zinafanyika mkoani Simiyu Tanzania bara huku kwa Zanzibar zinafanyika kisiwani Pemba.

Kwa kuzingatia msukumo uliowekwa na Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula mwaka jana, kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Chakula Duniani inasema, “Habaki mtu nyuma: uzalishaji bora, mazingira bora, lishe bora na maisha bora kwa wote,” ilitoa wito wa mabadiliko ya mifumo bora zaidi, jumuishi, thabiti na endelevu ya kilimo cha chakula kwa ajili ya kuboresha uzalishaji, lishe, mazingira, na maisha bora kwa wote, bila kuacha mtu nyuma.

Mwaka 2021, Mkutano wa Mifumo ya Chakula uliweka msingi wa mabadiliko ya mifumo ya chakula duniani na kuharakisha hatua ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu. Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia, na wasomi wote wana jukumu la kutekeleza, lakini vivyo hivyo na matendo yetu binafsi.

Mifumo ya chakula huchangia hadi theluthi moja ya uzalishaji wa gesi chafuzi duniani huku pia ikichagizwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Mabadiliko makubwa yanahitajika ili kulisha watu bilioni 10 duniani kote kufikia 2050, bila kuacha mtu yeyote nyuma.

Wizara za Kilimo (Bara na Zanzibar) pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na wadau wengine, waliandaa shughuli mbalimbali kwa wiki moja mfululizo za kuwafikia watu ili kuongeza uelewa na kuchukua hatua za kuondoa njaa, uhaba wa chakula na utapiamlo.

Ilijumuisha maonyesho katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi ya teknolojia mbalimbali za mifumo ya chakula cha kilimo (kutoka shambani hadi mezani); kampeni ya upandaji miti; maonyesho ya chakula cha jadi; Siku ya afya na Lishe kijijini (SALIKI) na shughuli za Siku ya Chakula Duniani kwa vijana kama vile urushaji wa vibonzo jongevu (animation) kuhusu lishe bora, na Jitihada zinazofanywa na Wasichana katika Kilimo kinachozingatia lishe kwa ajili ya kutengeneza “Mabalozi wa Chakula Bora” ili kuendeleza ajenda 2030 na uzinduzi wa mikakati/miongozo/vifaa mbalimbali ili kusaidia mabadiliko ya mfumo wa kilimo cha chakula.

“Njia nne bora” zinawakilisha mbinu mpya ya kufanya kazi na wito mpya kwa wadau wote ili kusaidia kufanya mifumo yetu ya chakula kuwa bora zaidi, jumuishi, thabiti na endelevu kupitia uzalishaji bora, mazingira bora, lishe bora na maisha bora kwa wote, bila kuacha mtu nyuma.

Kwa ajili hiyo, Siku ya Chakula Duniani mwaka huu inatoa fursa ya kipekee kwetu kutafakari, kuangazia, kutumia, na kukuza kasi inayotokana na mchakato wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula ya kubadilisha mifumo yetu ya kilimo cha chakula kwa kutekeleza mabadiliko ya kimuundo ambayo hayakufikiriwa hapo awali.

*Mwakilishi mkazi wa Shirika La Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Tanzania