Halmashauri ya Mwanga inavyosimamia uhifadhi wa mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu

Muktasari:

Mazingira ni jumla ya mambo yanayomzunguka binadamu ikiwa ni pamoja na hewa, ardhi, maji, tabianchi, sauti, mwanga, harufu, ladha, vijiumbe, hali za kibaolojia za wanyama na mimea, rasilimali za kitamaduni na masuala ya uchumi jamii.

Mazingira ni jumla ya mambo yanayomzunguka binadamu ikiwa ni pamoja na hewa, ardhi, maji, tabianchi, sauti, mwanga, harufu, ladha, vijiumbe, hali za kibaolojia za wanyama na mimea, rasilimali za kitamaduni na masuala ya uchumi jamii.

Aidha mazingira yanagusa maisha ya wanadamu, majengo, mashine na nyenzo zilizotengenezwa na wanadamu. Miaka kadhaa iliyopita suala la mazingira halikupewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya uchumi na kuondoa umaskini.

Hivi sasa uelewa wa jamii umeongezeka na masuala ya mazingira yanapewa kipaumbele katika kuandaa mipango ya maendeleo. Halmashauri ya wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa halmashauri za kupigwa mfano nchini katika usimamizi wa mazingira kwa kulifanya jambo hilo kuwa ajenda rasmi ya kimaendeleo wilayani humo.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Zefrin Lubuva anaeleza namna Wilaya hiyo ilivyofanikiwa katika usimamizi wa mazingira.

“Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ina ukubwa kilomita za mraba 2,641 kati ya hizo kilometa za mraba 2,558 ni nchi kavu, 82.4 ni maji ambapo kilometa za mraba 56 ni Bwawa la Nyumba ya Mungu na 26.4 ni Ziwa Jipe,” anaeleza Lubuva.

Anasema, Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ina ya watu 131,442 kati ya hao wanaume ni 63,199 na wamawake ni 68,243 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Mwelekeo wa Halmashauri katika kusimamia mazingira

“Dira ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ni kuwa Halmashauri yenye mazingira safi na maendeleo. Pamoja na kuwa na uwezo wa kuratibu na kusimamia shughuli kuu zilizopo na kuwezesha wananchi kupata huduma za msingi kwa kuongeza tija ili kuboresha maisha yao,” alisema Lubuva.

Anaongeza kuwa, “Mwelekeo wa Halmashauri ya Wilaya ni kuwahamasisha, kuwashirikisha wadau wote wa mazingira na kuwajibika katika suala la uhifadhi wa mazingira wa kufuata misingi ya Sheria ya usimamizi wa mazingira namba 20, ya mwaka 2004.”

Sababu za kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira

“Uchafuzi wa Mazingira katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mwanga unasababishwa na shughuli za kilimo kwa kutumia viatirifu kinyume cha taratibu, uanzishwa wa gereji kwe-nye maeneo mbalimbali yasiyo rasmi, utiririshaji wa maji taka kwenye baadhi ya maeneo yenye shughuli za viwanda na utupaji wa taka hovyo katika maeneo mbalimbali,” alisema Lubu-va.

Jitihada za kuzuia athari za uharibifu wa mazingira

Lubuva anasema kuwa, kuna mpango bora wa matumizi ya ardhi, kkatika vijiji viwili ambavyo ni Kileo na Kivulini vina mpango wa matumizi bora ya ardhi na zoezi linaendelea kwa maeneo mengine.

“Halmashuri ya Wilaya ya Mwanga inaweka jitihada katika suala la upandaji miti katika maeneo mbalimbali kwa kuweka Sheria ndogo kwa mfano katika maeneo ya makazi na viwanja vinavyopimwa kupanda miti isiyopungua 8 pia itatege-mea ukubwa wa eneo. kwa mwaka 2018/2019 jumla ya miti 839,091 ilipandwa katika maeneo mbalimbali,” alieleza Lubuva.

“Kufanya ufuatiliaji wa maandalizi mapitio na vibali vya Tathmini ya athari kwa Mazingira (TAM) kwa wawekezaji wa ndani kwa miradi mbalimbali inayoanzishwa katika Wilaya ya Mwanga ili shughuli hizo zisilete athari mbaya kwa mazingira,” alisema.

Hali ya utunzaji wa mazingira Wilaya ya Mwanga ukilin-ganisha na miaka iliyopita

“Usafi katika maeneo ya wazi yaliyopo katika Mamlaka ya Mji Mdogo Mwanga kwa uondoaji wa vichaka na mapori yaliyokuwepo awali umeimarishwa, na maeneo hayo kwasasa yameboreshwa na kuweka mandhari nzuri ya Mji wa Mwanga hasa eneo la barabara ya kuingilia Mji wa Mwanga kuanzia darajani mpaka Ofisi za CCM Wilaya eneo linalokadiriwa ukubwa wa ekari 1. Kwa sasa eneo hilo limeanzishwa bustani,” alisema Lubuva.

Anasema, katika udhibiti wa taka ngumu na utupaji wa taka hovyo Halmashauri ya Mwanga pamoja na wadau imefanikiwa kuweka mapipa 4 na “dustbins” 5 za kuhifadhia taka ngumu katika maeneo ya wazi yenye mikusanyiko ya watu.

“Katika kuboresha na kupendezesha mandhari za Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga na Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Mwanga jengo la Ofisi hizo limefanyiwa ukarabati mkubwa pamoja na kupakwa rangi,” alieleza mkurugenzi huyo.

Ushirikishwaji wa wadau wa mazingira katika kuhakiki-sha athari za kimazingira zinapungua ndani ya Wilaya

“Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga inashirikisha wadau mbalimbali waliopo ndani na nje ya Wilaya ambao ni Taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali katika suala zima la uhifadhi wa mazingira,” alisema.

Anasema, kwa sasa kuna jumla ya vikundi 13 ambavyo vimesajiliwa na vinajihusisha katika masuala ya mazingira. Taasisi za Jeshi la Magereza Kiruru, Jeshi la Polisi, Benki ya NMB, CRDB na Benki ya Wananchi wa Mwanga ni wadau wakubwa wanaoshirikiana na Halmashauri ya Mwanga katika suala la mazingira.

Anaongeza kuwa, aidha tunawakaribisha wadau mbalimbali wa mazin-gira kuwekeza katika Halmashauri ya Mwanga kwenye masuala ya mazingira kutokana na fursa zilizopo hasa Ardhi nzuri, miun-dombinu na rasilimali kama milima, Ziwa na Bwawa la nyumba ya Mungu.

Mipango iliyowekwa katika kukabiliana na changamoto za kimazingira zitokanazo na shughuli za viwandani

Lubuva anaeleza kuwa, ili kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya 5 nchi kuelekea kwenye uchumi wa viwanda, Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imeshatenga eneo katika Kitongoji cha Kisangiro kwa ajili ya uwekezaji wa shughuli za viwanda.

 “Kuwepo kwa eneo maalumu kwa ajili ya viwanda utarahisisha utekelezaji wa Tathimini ya mazingira kimkakati ya shughuli na mipango ya miradi mikubwa itakayofanyika katika Halmashauri ya Mwanga,” alisema Lubuva.

Mikakati ya kuboresha usimamizi na utunzaji wa mazingira

“Kuwepo na kuimarisha usimamizi wa sheria ndogo za uhifadhi na usafi wa mazingira katika ngazi ya Halmashauri na vijiji vyote vya Wilaya ya Mwanga, kuongeza uwezo wa kusafisha, kukusanya na kudhibiti taka maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na barabara kuu, maeneo ya wazi, masoko, mifereji na makazi kwa kuunda vikundi vya ukusanyaji taka majumbani,” alisema Lubuva.

Lubuva aliitaja mikakati mingine kuwa ni kuimarisha kamati za mazingira, kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Kijiji, Kamati hizo zinawajibika kuratibu na kutoa ushauri kuhusu vikwazo kwenye utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na programu za mazingira, kuongeza mwamko au utambuzi kuhusu mazingira, utoaji habari, ukusanyaji na utawanyaji habari zin-azohusu mazingira katika wilaya, kata au vijiji.

Changamoto za usimamizi na utunzaji wa mazingira

Lubuva anasema, katika shughuli za usimamizi na utunzaji wa mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

Ukame ni tatizo kubwa katika Wilaya yetu hasa maeneo ya tambarare. Pamoja na jitihada za kukabiliana na tatizo hilo pia mabadiliko ya tabia nchi yanadhoofisha jitihada hizo.

Mmomonyoko wa udongo nao unapunguza uwezo wa ardhi kuzalisha mazao katika sehemu mbalimbali ndani ya wilaya yetu. Uharibifu wa makazi ya viumbe wa majini, viumbe hai wa majini hasa mazalia ya samaki kwenye Ziwa Jipe, Bwawa la Nyumba ya Mungu na mito vinaathirika kutokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu kandokando ya maeneo hayo pamoja na uvuvi haramu.

Uharibifu wa misitu rasilimali za misitu na nyika zinapungua kila mwaka kutokana na ukataji miti hovyo kwa ajili ya kuni, mkaa, mbao na kuvamiwa kwa maeneo hayo kwa ajili ya kilimo na malisho.

Uharibifu wa vyanzo vya maji Shughuli mbalimbali za kibinadamu hasa kilimo zinazofanywa ndani na kandokando ya maeneo haya zinatishia kutoweka kwa vyanzo vya maji mfano ziwa Jipe kuathirika na magugu maji.