IMELIPIWA: MCHANGO WA UVUMBUZI NA UBORESHAJI TEKNOLOJIA (UUT) KATIKA USHINDANI WA VIWANDA NA MAUZO YA BIDHAA NJE YA TANZANIA

Muktasari:

Kwa tafiti zaidi zinazolenga kutoa mapendekezo ya kisera kwa maendeleo jumuishi, tembelea: www.repoa.or.tz

REPOA. Andiko hili la kisera linawasilisha muhtasari wa matokeo muhimu na mapendekezo kutoka katika utafiti wa REPOA kuhusu mchango wa UUT katika ushindani wa sekta ya viwanda na mauzo ya bidhaa nje ya Tanzania.

Ili kufikia lengo lake, utafiti ulifanywa katika vipengele vitatu. Kipengele cha kwanza kiliangalia uchanganuzi wa hali halisi ya mambo ambapo tulitathmini hali ya sasa na mwelekeo wa teknolojia na uvumbuzi miongoni mwa sekta za viwanda vya Tanzania.

Kutokana na upungufu wa ushahidi wa kutosha wa kisayansi wa kuchagiza majadiliano ya kisera kuhusu ajenda ya UUT nchini Tanzania, kipengele cha pili kilijikita katika uchambuzi wa kitaalamu, kwa kutumia takwimu zilizopo za Utafiti wa Mwaka wa Uzalishaji Viwandani (ASIP) ili kubaini vichochezi vya UUT katika ngazi ya kampuni na kupima athari zake katika ushindani wa makampuni.

Ili kuonyesha jinsi kampuni zinavyoweza kufanyia kazi UUT kwa vitendo, kipengele cha tatu na cha mwisho kiliwasilisha mfano halisi kulingana na uzoefu wa kampuni chache zilizochaguliwa ili kutambua na kufafanua vipengele vya mafanikio na mazingira halisi ambapo UUT imefanya kazi na kuimarisha kwa kiasi kikubwa utendaji wa kampuni na ushindani.

Mbinu ya utumiaji mifano halisia ilisaidia kukabiliana na vikwazo vya upatikanaji wa taarifa za utafiti wa ASIP ambao haukuwa ukitoa taarifa za kutosha za uzoefu wa kampuni katika masuala ya UUT, changamoto na matarajio.

Muhtasari muhimu wa matokeo ya utafiti umefupishwa hapa chini na kupangwa kulingana na maswali muhimu ya utafiti wa kisera.

Matokeo muhimu ya utafiti

Mwelekeo na hali ya sasa ya UUT katika sekta ya viwanda nchini ikoje?

Kwa kutumia fahirisi tofauti hususan Fahirisi ya Uvumbuzi wa Kimataifa, Utendaji wa Biashara na Viashirio vya Msingi vya Utafiti, matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa:

  • Tanzania imefanya vyema katika viwango vya Fahirisi ya Uvumbuzi wa Kimataifa katika mapato yatokanayo na uwekezaji katika uvumbuzi ikilinganishwa na nchi za kipato cha chini zinazolinganishwa barani Afrika. Tanzania ilishika nafasi ya 88 kwenye fahirisi ya mwaka 2020 hivyo kuongoza kundi la watu wa kipato cha chini kwa mwaka huo.
  • Hata hivyo, bidhaa nyingi zinazouzwa nje ya nchi ni zile zenye teknolojia duni, hususan zitokanazo na rasilimali (madini/dhahabu), huku bidhaa zenye teknolojia ya hali ya juu zikiwa ni zile zinazoingizwa nchini. Hata hivyo, kulingana na uboreshaji wa jumla wa utendaji kazi wa kipengele cha uvumbuzi, muundo wa mauzo ya nje umekuwa ukibadilika kwa ajili ya kuongezeka kwa sehemu ya bidhaa za teknolojia ya juu katika mauzo ya bidhaa nje.
  • Sekta nyingi zinazotumia teknolojia duni nchini zinachangia 75% ya jumla ya viwanda vya uzalishaji, zile zinazotumia teknolojia za kati na juu zikichangia kwa 25%.
  • Vile vile, juhudi zaidi za UUT huwekewa mkazo zaidi miongoni mwa kampuni zinazotumia teknolojia za kati na juu kuliko kampuni zinazotumia teknolojia duni jambo ambalo halishangazi kwani kampuni nyingi za aina hii zina uwezo mdogo wa kuwekeza katika masuala ya uvumbuzi.


Je ushahidi wa kisayansi unaendana na lengo la sera ya ukuzaji mchango na athari za UUT katika ushindani wa kampuni? Vipi ni vichochezi vikuu vya UUT na kwa namna gani uvumbuzi na uboreshaji teknolojia unaathiri moja kwa moja ushindani wa kampuni?

Kulingana na kanzidata ya ASIP kuhusu viwango vya kampuni, utafiti unakadiria viambatisho vya UUT na baadaye kukagua athari zake katika ushindani wa kampuni. Matokeo yanaonyesha kuwa:

  • Uwekezaji katika UUT una matokeo chanya katika tija ya kampuni, na kwamba uwezekano wa kampuni kuwekeza katika UUT unahusiana vyema na umri wa kampuni (kampuni kongwe zina uwezekano mkubwa wa kuwekeza katika UUT ikilinganishwa na kampuni changa), ushiriki katika biashara ya kimataifa, umiliki wa kigeni na ukubwa (kampuni ndogo zina uwezekano mdogo wa kuwekeza katika UUT ikilinganishwa na kampuni kubwa, ikiangaliwa changamoto za kiuwezo).
  • UUT ya umma na ushirikiano katika programu za teknolojia una matokeo chanya katika kukuza UUT na uboreshaji wa teknolojia kwa ajili ya ushindani wa viwanda/uuzaji bidhaa nje, hasa kwa kampuni za kati na ndogo.
  • Hata hivyo, kampuni zinazopokea ruzuku ya Serikali zina uwezo mdogo wa kuwekeza katika UUT kwa 43% kuliko nyinginezo, ikionyesha athari hasi zinazoweza kutokana na upokeaji ruzuku katika kudhoofisha uwekezaji binafsi.
  • Kwa kuangalia vichochezi vya UUT, matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa kampuni zina uwezekano mkubwa wa kuwekeza katika UUT au kuzalisha mapato yatokanayo na UUT ikiwa yanashiriki katika biashara ya kimataifa au ni wanachama wa vyama vya sekta ya viwanda na zinakabiliana na mazingira ya ushindani zaidi. Hii inaonyesha kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kampuni kupata uzoefu wa mazingira mapya kwani kufanya hivyo kunaimarisha viwango vya UUT.
  • Kwa upande wa uhawilishaji wa teknolojia, makadirio yanaonyesha kuwa faida nyingi za uhawilishaji wa teknolojia kwa viwanda vya Tanzania.
  • Hata hivyo, kinyume na matarajio, inaonekana kwamba uzoefu wa awali wa mfanyakazi alioupata katika kampuni ya kigeni si kigezo cha uhawilishaji wa teknolojia. Vile vile, eneo la kiwanda si kigezo katika uhawilishaji wa teknolojia, labda kwa sababu ya mazingira na asili ya mauzo ya nje ya kampuni zilizopo katika kanda za kimkakati za kiuchumi na ushindani mdogo na uangalizi wa moja kwa moja na kampuni za nyumbani.
  • Kwa ujumla, uhawilishaji wa teknolojia ni muhimu kwa baadhi ya sekta (kwa mfano, chuma) zaidi kuliko nyingine (usindikaji wa chakula); na kwamba kampuni kubwa hazihitaji (kunufaika na) uhawilishaji wa teknolojia kama ilivyo kwa kampuni ndogo na kati zinavyofanya.

Uzoefu gani uliopo wa kampuni katika kutumia vyema fursa za mchango wa UUT kukuza viwango vya ushindani na tija? Mafunzo gani yanaweza kuchukuliwa na kutumiwa katika sekta ya viwanda na kwingineko nchini?

Kwa sababu ya mapungufu ya taarifa zilizopo katika utafiti wa ASIP, utafiti huu ulitumia mbinu ya aina yake ili kutoa maelezo ya kina kuhusu tajriba ya kampuni zilizofanya uwekezaji katika UUT, changamoto na matarajio.

Ripoti hii ilijadili tajriba ya kampuni za zilizofanya uwekezaji katika UUT kulingana na maelezo ya mazingira, vichochezi na athari za uvumbuzi na uboreshaji teknolojia uliofanywa na kampuni mbalimbali na kuangazia changamoto na mafunzo yanayojitokeza.

Uzoefu wa kampuni binafsi umeelezewa kwa kina katika ripoti, lakini vipengele muhimu vya jumla na matokeo muhimu yanaonyesha kuwa:

  • UUT umekuwa mchakato binafsi mno kiasi ambacho ni vigumu kupata sampuli moja kwa wote. Licha ya ukweli kwamba kampuni zinatofautiana katika uwekezaji na uzoefu wao kwenye UUT, baadhi ya vipengele vinavyofanana vinaakisi kiwango, asili na athari ya mwisho. Hizi ni pamoja na ukweli kwamba, kampuni zote zinaendeshwa na ushindani wa soko kubwa kupitia tija na uboreshaji wa ubora.
  • Ingawa kiwango cha UUT kinaonekana kuwa cha msingi na kinachotegemea uhawilishaji wa teknolojia (kubadilika) kutokana na bidhaa zitokazo nje/ubia wa nje, kina athari kubwa kwa ushindani wa kampuni. Licha ya kutopatikana kwa taarifa za kuaminika na zinazoweza kukadiriwa ili kuonyesha athari, kampuni zilizohojiwa zilithibitisha kuwa mara kwa mara kwamba ukumbatiaji wa UUT ulichangia utendaji kazi mzuri wa kampuni. Hii ni kwa sababu kampuni nyingi zililenga kufikia masoko makubwa zaidi, kuboresha ubora na kuzikimbilia fursa za soko kutokana na changamoto fulani.
  • Ili kuhakikisha mafanikio ya kampuni, mchakato huu ni muhimu kama matokeo ya mwisho ya uvumbuzi na uboreshaji teknolojia. Mchakato wa uvumbuzi na uboreshaji teknolojia unasisitiza haja ya kupanga kwa uangalifu kabla na kuwa na mchakato/mwongozo ulioamuliwa mapema wa kuendesha mkakati wa ITU. kampuni ziliangazia changamoto tofauti zilizokabiliana nazo katika mchakato huo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa fedha zinazohitajika, sera za Serikali zinazounga mkono, na utaalamu, miongoni mwa changamoto nyingine. Zaidi ya hayo, mchakato wa UUT unasisitiza umuhimu wa utafiti na uhawilishaji wa teknolojia katika kufikia matokeo ya mwisho.
  • Sera na mfumo wa kitaasisi ni muhimu katika kufikia UUT wenye matokeo mazuri, uzoefu wa kampuni na shuhuda hutoa ishara kama kuna uthibitisho juu ya jukumu lake katika kuimarisha uvumbuzi na uboreshaji katika ngazi ya kampuni, ikisisitiza haja ya utafiti zaidi.

Mafunzo muhimu kutokana na matokeo ya utafiti

Kulingana na uzoefu thabiti na UUT, tulitambua baadhi ya mafunzo muhimu ambayo yanadadavua jinsi kampuni zinavyoweza kutumia UUT kwa mafanikio na kutoa michango katika ukaguzi wa sera/mazungumzo au uundaji wa sera, mikakati au programu bora zaidi. Haya yameelezwa kwa ufupi kama ifuatavyo:

Muundo wa shirika ni muhimu, kwa kuwa kuwa na kitengo cha UUT/T&M ni kichocheo cha uwekezaji endelevu wa kampuni katika UUT ili kusaidia ukuaji wake.

Kufanya utafiti wa awali ni muhimu kabla ya kuanza mchakato kamili wa UUT. Kwa hivyo, kiwango cha mafanikio katika uwekezaji wa UUT kinategemea uwekezaji wa awali uliofanywa kwenye utafiti (k.m. utafiti wa soko, bidhaa au pembejeo).

Upatikanaji wa fedha wenyewe husababisha mchakato mzuri na wa wakati wa UUT kwa sababu kampuni nyingi hushindwa kuwekeza katika UUT kwa kukosa fedha.

Ushindani ni nyenzo muhimu kwa UUT. Hivyo, ushindani una jukumu chanya katika kuhamasisha kampuni kushiriki katika shughuli za UUT.

Hitimisho na Mapendekezo ya Sera

Kutokana na tafiti zilizotangulia, utafiti huu umekuja na hitimisho lifuatalo la kisera:

  • Licha ya mwelekeo wa kiwango cha UUT kuendelea kukua (ingawa kutoka chini zaidi) kwa Tanzania katika miaka michache iliyopita, juhudi za kampuni na Serikali kuchochea mwelekeo huo ili kusaidia ushindani unaohitajika nchini ni mdogo. Licha ya mabadiliko madogo ya kimuundo, uzalishaji na mauzo ya nje nchini umetawaliwa na sekta zinazotumia teknolojia duni (hususan kampuni ndogo na za kati) na bidhaa zitokanazo na rasilimali zilizopo nchini (dhahabu).
  • Kwa hakika, uwezo na matarajio ya uwekezaji wa siku za usoni katika UUT unadhihirika kwa kampuni kubwa na zile zinazomilikiwa na wageni. Hii ina maana kwamba kampuni nyingi zimeachwa nyuma, kutokana na soko kutawaliwa na kampuni ndogo na za kati. Hii inaashiria uwepo wa haja ya Serikali kuwekeza zaidi katika programu za ubia wa teknolojia ili kusaidia kampuni ndogo na za kati, kukuza teknolojia na uhawilishaji wa ujuzi, miongoni mwa taratibu nyingine, kukuza uhusiano baina ya kampuni kubwa / za kigeni na ndogo / za ndani, hususan katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs).
  • Kupitia tathmini ya mfano halisi ilibainisha sababu kuu za mafanikio ya uwekezaji wa UUT kwa kampuni. Hii ni pamoja na umuhimu wa kuwa na kitengo cha UUT/T&M, kufanya utafiti wa awali kabla ya kuanza mchakato kamili wa UUT, kuwa na fungu la fedha la kutosha hususan kutoka katika fedha za ndani, kukumbatia ushindani; na msaada wa Serikali katika kuboresha mazingira ya kisera na udhibiti, na kuimarisha taasisi za msaada wa teknolojia na uvumbuzi (k.m., SIDO, CARMATEC, TIRDO n.k.)

Kufuatia matokeo haya, mapendekezo yafuatayo yanatolewa:

  • Kupitia upya sera na mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya kukuza UUT ili kuziba mapengo na kuimarisha jukumu la Serikali/taasisi za Umma.
  •  Kushughulikia changamoto zilizoainishwa zinazozuia kampuni kuwekeza katika UUT. Changamoto kubwa zaidi kati ya hizi ni pamoja na hakimiliki dhaifu ambazo zinachochea kunakili au kuiga uvumbuzi au ugunduzi wa kampuni nyingine bila idhini; usimamizi mbovu wa taratibu za forodha na chombo cha sera ya biashara kwa ajili ya kulinda wazalishaji wa ndani; na changamoto za uwezeshaji fedha, miongoni mwa nyinginezo.
  • Kuimarisha taasisi zilizopo kwa ajili ya kukuza UUT ikiwa ni pamoja na hatua ya kuhakikisha uwezeshaji fedha wa kutosha, kuhamasisha/kuongeza ufahamu kuhusu jukumu lao katika kusaidia kampuni katika masuala ya uvumbuzi na uboreshaji. Taasisi hizi ni pamoja na taasisi za T&M, TIRDO na taasisi za kitaaluma; taasisi za teknolojia kama vile CARMATEC, SIDO, COSTECH n.k. na Wakuzaji Viwanda (k.m., EPZA, TIC, NDC n.k.).
  • Kuboresha ubora wa elimu na ujuzi kwa kuongeza uwezo wa taasisi za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVETs) katika kutoa ujuzi unaofaa ili kukidhi mahitaji ya sekta, na hatimaye.
  • Kufanya utafiti zaidi juu ya jukumu na ufanisi wa sera ya Serikali, mifumo ya udhibiti na kitaasisi kwa ajili ya kukuza UUT.


@REPOA 2022

Matokeo ya tafiti na maoni yaliyotolewa ni ya mwandishi wa ripoti hii na si lazima yafungamane na mawazo au sera za REPOA au mshirika wake mwingine yeyote.


Makala hii imelipiwa na REPOA. Mwananchi Communications Limited (MCL) haihusiki kwa namna yoyote na bidhaa ama huduma zinazotangazwa humo na haitawajibika kwa chochote kitakachojiri ukiamua kuzitumia.