Je, Tanzania inapaswa kuwa na wasiwasi na nakisi ya bajeti yake?
Matumizi ya umma huiwezesha Serikali kutimiza malengo na ahadi zake kwa wananchi juu ya utoaji wa bidhaa na huduma za umma au/ pamoja na mgawanyo wa rasilimali. Hili lina ukweli kwa nchi zote tajiri na masikini, na Tanzania haijitengi kwenye hili. Kati ya 1999/00 na 2020/21, matumizi ya Serikali yaliongezeka kwa mara 26 huku mapato ya serikali yatokanayo na kodi na yasiyo ya kodi yakipanda mara 20, na kusababisha ongezeko la upungufu katika bajeti kwa mara 15 (tazama Kielelezo Na. 1).
Uhimilivu/ muendelezo wa nakisi ya Bajeti
Swali ni kama hali hii ya nakisi ya bajeti ni endelevu. Mantiki rahisi ya muendelezo wa nakisi ya bajeti ni kuhusianisha nakisi iliyopo na ukuaji wa uchumi. Wataalamu wanatofautiana kuhusu ukubwa sahihi wa uhimilivu wa nakisi ya bajeti, lakini kwa ujumla wananukuu kiasi cha asilimia 5 ya Pato la Taifa (maarufu kama GDP) au chini ya hapo (Afonso na Jalles, 2013; Akosah, 2013).
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kuwa na kiwango cha asilimia 3. Kielelezo Na 2 kinaonyesha kuwa Tanzania imendelea kujielekeza katika lengo la kufikia asilimia 3 tangu mwaka 2005/06, na 2016/17 ilifikia kiwango hicho na kubakia ndani ya lengo kwa miaka minne zaidi hadi 2020/21 iliposhindwa kubakia hapo. Kielelezo Na 3 kinaonyesha kuwa Tanzania pia ilifanya vizuri zaidi ya wanachama wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tangu 2015/16. Hivyo, kutokana na kiashiria hiki, nakisi ya bajeti kwa Tanzania imekuwa ‘himilivu’ katika miaka ya hivi karibuni.
Lakini uwezo wa Serikali kuendelea kugharamia nakisi ya bajeti yake hautegemei tu katika ukuaji na ukubwa wa nakisi ya bajeti yake pamoja na uchumi bali pia viwango vya riba kwa fedha zilizokopwa kwa ajili ya bajeti hiyo na mfumuko wa bei. (Langdana & Murphy, 2014).
Viwango vya riba huathiri gharama ya ulipaji madeni, na mfumuko wa bei hupunguza thamani halisi ya madeni ya kawaida na pia thamani halisi ya deni na gharama za huduma ya deni. Kwa mantiki hiyo, na kwa kuzingatia falsafa ya Dornbush ya uhimilivu wa nakisi ya bajeti, kwa maana ya gharama halisi ya ulipaji madeni inaweza kuonyeshwa kama ifuatavyo:
EBDS kama asilimia ya Pato la Taifa= (Deni/Pato la Taifa) x (Kiwango halisi cha riba-Kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa)
Jedwali namba 1 linaonyesha kuwa mwenendo wa gharama za madeni nchini kuanzia 2007/08 hadi 2020/21 umepitia awamu tatu tofauti. Katika awamu ya kwanza na ya tatu, 2007/08 - 2012/13 na 2017/18 - 2020/21, ulipaji madeni ya taifa haukuzidi uwezo wa uchumi wa kuendelea kuyahimili. Katika awamu hizi mbili, gharama za madeni zilikuwa himilivu. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti wakati wa awamu ya pili, 2013/14 - 2016/17, ambapo gharama za madeni zikizidi uwezo wa uchumi wa kuhimili kupitia ukuaji wa uchumi na mfumuko wa bei. Hivyo, kwenye miaka kumi kati ya kumi na nne, gharama za madeni nchini zilidhibitiwa kikamilifu kifedha.
Je, mwenendo wa nakisi ya bajeti unaleta wasiwasi kisera?
Je, inatosha kuwa nakisi ya bajeti inadhibitiwa kifedha? Tunajibu swali hili kwa kupitia muundo na mwenendo wa matumizi ya umma na athari zake katika uwanda wa sera ya kifedha. Kielelezo Na. 4 kinaonyesha mabadiliko endelevu ya kisera kati ya matumizi ya kimaendeleo na yale ya kawaida, huku yale ya kimaendeleo yakiongezeka. Kati ya 2002/3 na 2020/21 kiwango cha matumizi ya kawaida kilipungua kutoka asilimia 81 hadi 56, kutokana na matumizi ya maendeleo kupewa kipaumbele zaidi na kutengewa fedha za kutosha. Uamuzi wa Serikali uliofanywa mwaka 2015/16 wa kuboresha kiwango cha bajeti ya maendeleo kufikia asilimia 35-40, uliyapa nguvu matumizi yahusuyo maendeleo na kuilazimisha Serikali kuyatengea fedha katika kila bajeti.
Matokeo ya mabadiliko ya sera katika kuyapa kipaumbele zaidi matumizi ya maendeleo inaonekana katika muundo na mwenendo wa matumizi ya kawaida kama yaliyowasilishwa kwenye Kielelezo Na. 5, ikionyesha sehemu ya ‘matumizi ya kawaida’ (OC) yakipungua mara kwa mara. Hii ni kwa sababu mishahara na malipo ya riba ni sehemu ya wajibu wa Serikali unaotakiwa kutimizwa. Pia inabainisha ya kuwa kiwango cha malipo ya riba kimekuwa kikipanda kwa kasi zaidi kuliko kile cha matumizi ya kawaida. Hivyo, kiwango cha fedha za matumizi mengineyo ndani ya matumizi ya kawaida kilipungua kwa nusu nzima kutoka asilimia 68 mwaka 2003/04 hadi 34 mwaka 2020/21.
Je, kuna mustakabali gani wa kisera dhidi ya upunguaji wa fedha za matumizi ya kawaida (OC)? Mosi, ni nafasi finyu kwenye sera ya kifedha ama ukomo kwa matumizi vilivyowekwa kwa watunga sera kutekeleza maamuzi yao ya kimsingi. Pia hii ni katika kiwango ambacho hata matumizi kwa ajili ya kuongeza tija yanaweza nayo kuathiriwa. Hii inakuwa mbaya zaidi kwa kuzingatia kuwa hata kwenye kwa fedha za matumizi ya kawaida ambazo tayari zimepungua, kwani sasa kifungu kimewekwa kwa matumizi yale ya kukakikishiwa kubaki tu, yale ambayo yanayoonekana kuwa nyeti sana kukatwa bila ridhaa.1.
Mustakabali wa pili na muhimu zaidi wa kisera ni kupungua kwa bajeti ya uendeshaji kwenye miradi ya upanuzi wa miundombinu. Sintofahamu hii ya kukua kwa uwezo wetu kwa haraka katika kipindi ambacho kuna ufinyu wa bajeti za kiuendeshaji sio jambo geni nchini. Ni marudio ya kile kilichotokea miaka ya 1970 ambapo kupanuka kwa uwezo wetu kulienda sambamba na uduni wa kimatumizi katika kiwango kikubwa , na kusababisha kushuka kwa tija katika sekta ya viwanda. (Wangwe, 1979). Kupungua kwa matumizi ya kawaida (OC) kunaakisiwa na upungufu wa wafanyakazi na vifaa katika sekta za afya, elimu, maji na ofisi za umma, kwa ufupi. Matokeo yake huonekana yakijichanganya ambapo wakati miundombinu yetu ikiimarika na kuongezeka ndiyo wakati huo huo huduma jumuishi za umma zinapungua.
Hitimisho
Mahitimisho mawili yanayoonekana kukinzana yanatokea kutokana na mjadala wa hapo juu. Kwanza, nakisi ya bajeti inadhibitiwa kimifumo ya fedha; kwa kiasi kikubwa, nakisi ya bajeti ya taifa ni himilivu na haileti shinikizo lisilo la lazima kwa uchumi. Pili, kuongezeka kwa gharama za madeni, pamoja na vipaumbele vingine vya matumizi kumezalisha muundo wa matumizi unaoacha nafasi finyu kwa fedha za matumizi mengineyo pamoja na maamuzi ya kihiari kwa watunga sera (uwanda wa kisera). Matokeo yake ni utendaji duni wa upanuzi wa miundombinu ya umma, yaweza pia kuonekana pia katika uduni wa huduma za umma. Hili ni suala la kisera na kimaendeleo linalotokana na ufinyu wa bajeti na lazima litafutiwe majibu.
_______________________
1 Kati ya matumizi ya kawaida (OC) ambayo tayari yamebanwa, kuna matumizi mengine nyeti ambayo lazima yatengewe fedha. Yanajumuisha posho za mgao; chakula cha wafungwa; gharama za mitihani; posho kwa maofisa utumishi wa idara ya huduma za mambo ya nje; michango kwa mashirika ya kikanda na kimataifa; posho za wafanyakazi kwa viongozi wastaafu; ruzuku kwa vyama vya siasa; posho kwa ajili ya kazi za ziada; na posho za majimbo.
REPOA HQ
157 Migombani REPOA streets, Regent Estate, PO Box 33223, Dar es Salaam, Tanzania.
Tel: +255 (22) 270 0083 Cell: +255 (0) 784 555 655
Website: https://www.repoa.or.tz
Email: [email protected]
Branch Office
2nd Floor Kilimo Kwanza Building 41105 Makole East, Kisasa, Dodoma, Tanzania