Kufungua njia zenye mafanikio na endelevu katika sekta ya madini: Uendeshaji wa Kongamano la Madini na Uwekezaji nchini 2023

Kongamano la Madini na Uwekezaji nchini (TMIF) 2023.

Kampuni ya dmg events, kwa kushirikiana na Ocean Business Partners (Tanzania) na Wizara ya Madini, wanayo furaha kutangaza kwamba Kongamano la Madini na Uwekezaji nchini 2023 litafanyika kuanzia Oktoba 25 – 26, 2023 katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar Es Salaam, Tanzania. Hafla hiyo inafanyika chini ya usimamizi wa Anthony Peter Mavunde, Waziri wa Madini na kupigiwa chapuo na Wizara ya Madini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika zama za mageuzi ya nishati duniani, Tanzania inasimama kama daraja muhimu, ikijiandaa kuwa muuzaji kinara wa madini na metali anayependelewa zaidi duniani. Kongamano la Madini na Uwekezaji nchini (TMIF) 2023 linasimama kama jukwaa bora la kutumia vyema fursa hii. Kwa kuzingatia ukuaji endelevu ndani ya sekta ya madini na nafasi yake katika kuuza madini na metali muhimu, kongamano hilo linaendana kikamilifu na matarajio ya nchi yetu. Kongamano linatoa jukwaa thabiti ambapo wadau kutoka mataifa mbalimbali duniani kote wanakutana kwa pamoja, kubadilishana maarifa, na kujenga ushirikiano, ili kulisukuma Taifa mbele katika  mageuzi ya nishati safi.

Wageni rasmi waliothibitishwa kupamba Kongamano la Madini na Uwekezaji nchini 2023.

Wakati Tanzania ikijiandaa kuwa muuzaji mkuu wa madini na metali muhimu, kongamano hilo litatoa fursa kwa kampuni/taasisi viongozi wa sekta hiyo kuongoza njia kwa pamoja katika kujenga kesho yenye nishati safi, rafiki kwa mazingira na endelevu. Tukio hili huleta pamoja wadau mama, viongozi sekta ya nishati, na wataalam kutoka duniani kote, likitoa fursa ya kipekee ya kukutana, kubadilishana mawazo, kutafuta ubia wa pamoja. Ni jukwaa adimu ambapo uwekezaji wa kisekta huainishwa, biashara hufanywa na suluhisho la changamoto za sekta hutafutwa, yote ikiwa na lengo la kuchangia katika maendeleo ya sekta ya madini nchini na jukumu lake muhimu katika mageuzi ya nishati duniani.


Kufungua fursa za sekta ya madini: Kongamano la Madini na Uwekezaji Tanzania

Kongamano la Madini na Uwekezaji nchini ambalo ni onyesho la kimataifa la utajiri wa maliasili, liko tayari kuwakutanisha zaidi ya washiriki 2,000 kutoka Tanzania, Afrika na duniani kote. Kongamano hilo la kimkakati tayari lina wazungumzaji zaidi ya 90 waliothibitishwa ikihusisha Serikali, wadau, viwanda na wawekezaji, wakiwemo Marais wawili, Mawaziri watano na Wakurugenzi saba.

Watu wengine mashuhuri katika sekta ya madini waliothibitishwa kuzungumza ni pamoja na Ruth Nakanbirwa, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini kutoka Uganda, Monica Chang’anamuno, Waziri wa Madini nchini Malawi; na Ibrahim Uwizeye, Waziri wa Maji, Nishati, na Migodi akiwakilisha Burundi.

Kampuni ya DMG Events iliendesha moja ya matukio katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Wazungumzaji wengine mashuhuri ni pamoja na Dk Venance Mwasse, Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO; Mhandisi Philbert M. Rweyemamu, Mwenyekiti wa Chama cha Madini nchini (TCM); Mhandisi Yahya I. Samamba, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Tanzania; Michael Lodge, Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Kimataifa ya Mkondo wa Bahari; na Simon Shayo, Makamu wa Rais (Miradi Endelevu) kwa Ghana na Tanzania wa AngloGold Ashanti.

Watu hawa mashuhuri wameandaliwa kuunda jopo kwa ajili ya kuchangia katika mada mahsusi za kongamano hilo, wakichagiza mjadala kuhusu kuvutia uwekezaji, ushirikiano na ubia, miradi na teknolojia endelevu za madini, uchangishaji fedha na uwekezaji endelevu katika sekta ya madini nchini, bidhaa za ndani na maslahi ya wazawa katika madini, uzingatiaji misingi ya usawa, na ujumuishi katika sekta ya madini, na kuboresha uwezo wa viwanda vya madini kusafisha rasilimali hizo; na kuongeza thamani ndani ya nchi.

Maonyesho haya ya kimataifa ya kongamano hili yanatengeza njia ya aina yake, inayokuza mwingiliano wa kibiashara baina ya Serikali na kampuni na kampuni kwa kampuni pamoja na msururu wa thamani ya madini tangu yanapochimbwa mgodini mpaka sokoni. Kwa upana wa mita za mraba 700 za eneo lililoandaliwa kwa ajili  ya  maonyesho na uwakilishi kutoka nchi zaidi ya 30, kongamano hili linachagiza muunganiko thabiti wa kampuni kinara wa sekta  ya madini. Miongoni mwa waonyeshaji mashuhuri ni AG Energies, AngloGold Ashanti, Auking, Mining, Barrick, Epiroc, Faru Graphite, FUCHS, Innovx-Africa, Lindi Jumbo, Mantrac, Noble Helium, Sotta Mining, STAMICO, STANVIK, TotalEnergies, Vivo Energy na Volt Resources.

Eneo la machimbo ya madini.

Kampuni ya dmg na washirika wenza katika maandalizi ya tukio hili kubwa, wanatoa shukrani zao za dhati kwa wadhamini wa tukio hili kwa msaada wao mkubwa katika kufanikisha kufana kwake kusiko na mfano. AngloGold Ashanti, mdhamini wa hadhi ya almasi, Barrick Twiga, mdhamini wa hadhi ya dhahabu, na TotalEnergies, mdhamini wa hadhi ya fedha, wamefanya kazi kubwa katika kuhakikisha tukio hilo linafanyika kwa ubora unaotakiwa. Shukrani pia ziende kwa wadhamini wa hadhi ya Bronze, Auking Mining, Solar Nitrochemicals, Benki ya Stanbic, Buckreef Gold, na Tembo Nickel, ambao michango yao ilitosha kufanikisha tukio hili.


Kufungua fursa na uwekezaji katika sekta ya madini inayokua kwa kasi nchini

Wakati dunia inaenda kwa kasi katika kufikia matarajio yake ya kuwa sehemu yenye nishati safi na endelevu, mahitaji ya madini na metali muhimu yanatarajiwa kuongezeka. Tanzania ikiwa ni nchi kinara kwa ukanda wa Afrika Mashariki, inajivunia sehemu kubwa ya utajiri wa bara hili, ikiwa na akiba nyingi za madini muhimu na metali muungo. Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Tanzania imeshuhudia ukuaji mkubwa katika sekta ya madini, ikijipambanua kama kitovu kikuu cha uchimbaji madini Afrika Mashariki na kuipatia dunia nyenzo muhimu zinazohitajika kuwezesha mageuzi ya nishati.

Fursa ya sekta ya madini nchini bado ni kubwa. Ni nchi yenye ukwasi wa akiba ya asilimia 13 ya madini  ya grafiti duniani, ikiwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa almasi barani Afrika, na kila mwaka ikizalisha zaidi ya kilo 55,603.75 za dhahabu. Kwa utajiri huo wa madini yenye thamani kubwa, Tanzania inaelekea kuwa mdau muhimu katika mageuzi ya kidunia kuelekea katika matumizi ya teknolojia endelevu na rafiki kwa mazingira.

Wakati sekta ya madini nchini ikiendelea kustawi, kongamano hilo linasalia kuwa msukumo wa Tanzania kuwa kitovu cha madini duniani. Inaendelea kuwa daraja linalounganisha hifadhi utajiri wa madini nchini na ongezeko la mahitaji ya madini muhimu duniani, na kujenga ushirikiano wa kitaasisi utakaosaidia kujenga mustakabali wa baadaye wa sekta ya madini na nishati endelevu.