Kuimarisha ukuaji endelevu na jumuishi kupitia mabadiliko ya kimuundo

Mpango wa sasa wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano - 2021/22-2025/26 -umeweka kipaumbele katika maendeleo ya viwanda na huduma katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya Tanzania ya kufikia ushindani wa ukuaji wa viwanda na biashara, na maendeleo ya watu. Mpango huo umeweka lengo la kiutendaji la kuongeza mauzo ya nje hadi asilimia 28 na kiwango cha mauzo ya nje katika masoko ya dunia kufikia asilimia 0.5.

Tanzania tangu mwanzo wa milenia ya pili imepitia kipindi cha ukuaji wa haraka na endelevu wa uchumi - kwa zaidi ya asilimia 6, na ule wa mtu mmoja mmoja, kwa zaidi ya asilimia 3.5 - ambayo ilikamilika kupitia uainishaji upya wa nchi za kipato cha chini hadi kipato cha chini cha kati Julai 2020. Jambo la kufurahisha, katika miongo mitatu iliyopita ukuaji wake umekuwa juu ya wastani wa ukuaji barani Afrika, nchi za kipato cha kati, nchi za kipato cha chini, nchi zinazoendelea na duniani kote.

Takwimu linganifu za nchi zinaonyesha kuwa wakati ukuaji wa uchumi nchini ukionekana wa kuvutia, uendelezaji wake utahitaji juhudi za ziada ili kukabiliana na kazi kubwa ya kukuza uwezo wa uzalishaji mali na kubadilisha muundo wa uchumi wake katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia mabadiliko makubwa yanayohusisha, pamoja na mengine, maendeleo ya kasi ya kiteknolojia, mwelekeo wa minyororo ya thamani duniani, na mabadiliko ya tabianchi. Mengine ni pamoja na vikwazo vya matumizi ya sera ili kukuza viwanda, ukuaji wa biashara na malengo mengine ya maendeleo ya Taifa.

Warsha ya 27 ya Utafiti ya Mwaka - REPOA

Katika kukabiliana na hitaji linaloongezeka kila uchwao la kuongeza kasi ya mabadiliko ya kimuundo na ya kiuchumi yanayotarajiwa, hasa katika kipindi hiki chenye fursa na changamoto za kidunia kwa pamoja, REPOA itaandaa kwa ushirikiano na Benki Kuu ya Tanzania, Gatsby Africa, pamoja na Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji (POPI) warsha ya siku mbili.

Ushirikiano huu utaipa Benki Kuu ya Tanzania, Gatsby Afrika na Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji fursa ya kuonyesha jinsi walivyojipanga kusaidia mabadiliko ya haraka ya kimuundo wa uchumi kwa ukuaji wa uchumi jumuishi, wenye ushindani na unaojielekeza kwenye uzalishaji wenye kuweza kukuza uchumi. Hii itajumuisha:

Ingawa hii si warsha ya kwanza ya kisera - kwa sera za kijamii na kiuchumi - kutathmini mabadiliko ya kimuundo nchini, lakini itakuwa ni warsha ya kwanza kuwahi kuandaliwa na REPOA katika zaidi ya miaka mitano ikilenga kutathmini mojawapo ya vipaumbele vya msingi vya dira ya sasa ya maendeleo ya Tanzania 2025 katika mabadiliko ya kikanda na uchumi wa dunia. Warsha hii inachochea na kuendeleza mazungumzo ya kisera na utafiti kuhusu jinsi ya kuharakisha mabadiliko ya kimuundo ya uchumi na kuboresha matokeo yake katika suala la ukuaji wa uchumi jumuishi, wenye ushindani na unaojielekeza kwenye uzalishaji wenye kuweza kukuza uchumi. Pia inaangazia matokeo ya uimarishaji endelevu wa uwezo wa uzalishaji, manufaa ya ujumuishi unaofaa katika minyororo ya thamani ya kikanda na kimataifa, na jinsi ya kuunganisha upya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi kwa ajili ya mabadiliko endelevu ya kiuchumi.

Ikienda sambamba na kaulimbiu ya warsha hiyo, mazungumzo yatajikita katika vipengele muhimu vinavyotokana na mabadiliko ya kimuundo, kuimarisha uwezo wa uzalishaji, mikakati ya ushiriki mzuri katika minyororo ya thamani ya kikanda na kidunia, na kuboresha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuharakisha mabadiliko ya kimuundo.

Kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa nchi

Ukuaji wa uzalishaji—ufanisi ambao jamii huchanganya watu, rasilimali, na zana zao—ndiyo kichocheo kikuu cha mchakato wa maendeleo ya viwanda na upanuzi wa biashara, unaosababisha upatikanaji wa mali na kupunguza umaskini.

Maboresho ya muda mrefu ya kuimarika kwa kipato katika sekta za viwanda na/au kilimo ndiyo chanzo cha ajira na maisha kwa watu wengi katika nchi zinazoendelea - mafanikio haya yanaweza kupatikana hususan kwa kukuza na kuboresha tija ya uzalishaji mali kwa wafanyakazi wa viwandani na wakulima.

Faida za uzalishaji kwenye kila sekta ya shughuli za kiuchumi ni matokeo ya awali ya kuongezeka kwa msukumo wa kiuzalishaji kwenye kila kitengo cha uzalishaji mali. Ugawaji upya wa rasilimali kutoka katika kampuni zenye uwezo duni kwenda kwenye zile zenye tija zaidi katika uzalishaji huchangia ukuaji wa uzalishaji kwenye sekta wa viwanda kwenye uchumi wowote wa soko - hususan katika nchi za uchumi wa kipato cha chini ambazo kimsingi huwa na mvurugiko wa chumi zake kutokana na kukosa mfumo wa masoko kamilifu, mkwamo na changamoto za kiuratibu, pamoja na uhaba wa kiteknolojia.

Umuhimu wa kuhakikisha ugawaji sawa wa rasilimali kwa wakati kwa shughuli za kiuzalishaji wa kiuchumi za kisasa ni changamoto kubwa ya mabadiliko ya kimuundo. Kwa maana hiyo, mkusanyiko wa ujuzi na uwezo wa kitaasisi ni muhimu ili kukabiliana na changamoto ya kimsingi na kuendeleza uwezo wa uzalishaji. Usawa kama huo ni muhimu kudumisha ukuaji wa muda mrefu wenye uwezo wa kuleta athari ambukizi ambazo huongeza uwezo wa taasisi wa kutambua thamani na kutumia vyema taarifa kibiashara na mwingiliano wa sekta za uzalishaji na usambazaji katika kubadilisha sekta za kiuchumi.

Umuhimu wa kuendeleza uwezo wa uzalishaji kwa ukuaji wa uchumi, upanuzi wa viwanda na biashara unaonekana wazi kupitia uzoefu wa maendeleo wa nchi zinazoendelea ambazo zimeweza kufikia upanuzi endelevu wa viwanda na biashara na kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa katika miongo mitatu iliyopita. Sifa kuu ya sera zao ni kwamba wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kukuza upanuzi wa viwanda na biashara na wamefanya hivyo kupitia sera lengwa ambazo zimejikita kukuza na kuwezesha upanuzi wa uwezo wa uzalishaji wa ndani. Hii pia imehusisha juhudi za kukuza uwekezaji, uvumbuzi, na mabadiliko ya kimuundo.

Ukuaji wa uzalishaji mali wa ndani na wa muda mrefu unachagizwa na ubunifu, uwekezaji katika mtaji halisi, na mtaji wa rasilimali watu ulioimarishwa. Hili linahitaji mazingira rafiki ya ukuaji, yenye taasisi zinazounga mkono jitihada hizo, na uimara wa uchumi mkuu kama nchi. Umuhimu wa ubunifu na uhawilishaji wa teknolojia nje ya mipaka ya nchi, na utaalamu katika kuzalisha bidhaa ngumu na nyepesi zitakazouzwa nje ya nchi umeendelea kuongezeka, pamoja na mabadiliko yanayohusisha idadi ya watu.

Ili kufufua ukuaji wa uzalishaji, njia moja ya kimkakati inahitajika ili kuchochea uwekezaji katika mtaji halisi na rasilimali watu, na kukuza mazingira rafiki ya ukuaji wa uchumi mkuu na taasisi. Fursa ya aina yake inajitokeza hapa kutokana na ukweli kwamba rasilimali za uzalishaji, uwezo wa ujasiriamali, na uhusiano wa uzalishaji – vyote hivi havitokei wenyewe tu bali hutengenezwa na kuboreshwa kwa kadri muda unavyokwenda. Hili linapotokea, pato la uchumi huongezeka, muundo wa viwanda hubadilika kwa kuongezeka kwa thamani ya juu ya uzalishaji, na kusababisha upanuzi wa viwanda na biashara.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, akihutubia hadhira katika Warsha ya Utafiti ya Mwaka ya Taasisi ya REPOA iliyofanyika visiwani Zanzibar kuanzia Novemba 2-3, 2022. Rais Mwinyi alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo.

Kuimarisha muunganiko kupitia minyororo ya thamani ya kikanda na kidunia

Kushiriki katika minyororo ya thamani ya kikanda na kidunia (RVCs & GVCs) kunatoa fursa za kuwaleta pamoja wazalishaji, wasindikaji, wanunuzi, na wauzaji katika mfumo wa muda wote - kwa nia ya kuongeza thamani ya bidhaa na huduma zinazotolewa kwa kadri zinavyopitia katika mnyororo kutoka wadau mbalimbali wanaohusika katika mchakato wa ubunifu wa wazo hadi mlaji wa mwisho katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa. Pia, wanaohusika katika minyororo hii ya shughuli za uongezaji thamani ni pamoja na watoa huduma za kiufundi, kifedha, biashara, na wengine walioko katika mnyororo wa uhusiano wa uzalishaji bidhaa. Minyororo ya thamani ya dunia hukuza uhusiano kati ya biashara moja na nyingine ambayo hurahisisha ujifunzaji na kupata taarifa ya soko ambayo nayo husaidia kuongeza mapato halisi. Kwa maana hiyo, uchumi wa sasa unaotegemea kilimo unaiacha mbali na kwa kasi sekta ya viwanda ambayo hubaki kuendeleza moja kwa moja sekta hiyo pamoja na kutoa huduma kupitia ushiriki wake katika minyororo ya thamani ya kilimo ya kikanda na dunia.

Zipo njia kadhaa ambazo Tanzania inaweza kuzitumia ipasavyo katika ushiriki wake katika minyororo ya thamani ya kikanda na dunia ili kufikia uwezo wa kupunguza utofauti mkubwa wa kimageuzi uliopo kati yake na chumi shindani zaidi za uzalishaji, na katika mchakato huo, husaidia mageuzi yake yenyewe ya kiuchumi. Minyororo ya thamani ya kikanda na dunia huwezesha uhusiano wa kisekta na biashara ambao ni muhimu kwa ajili ya kujifunza na kuchochea mabadiliko yanayotokana na mahitaji.

Minyororo ya aina hii huweza kutoa msukumo unaohitajika kwa viwanda binafsi na kuziunganisha sekta kwa jumla nchini ili kuziendea kwa dhati fursa za kuongeza uzalishaji na ujuzi unaohitajika na uboreshaji wa teknolojia. Hii pia itarahisisha kuwepo kwa shughuli za ziada zinazotoa ajira na kuongeza mapato mbalimbali kama vile usafiri na usafirishaji, huduma za benki na kifedha, bima, huduma za afya, huduma za elimu, na huduma nyingine kadhaa za usaidizi.

Hata hivyo, ili kutekeleza vyema miradi ya minyororo ya thamani ya kikanda na dunia kama nyenzo muhimu ya mkakati wa mageuzi ya nchi, umakini unahitajika ili kutambua sekta na bidhaa ambazo Tanzania imejaaliwa kuwa nazo ambazo zitaleta faida kubwa zaidi na uwezo wa kiuzalishaji kutokana na uwekezaji hai. Minyororo ya thamani ya kikanda na kidunia pia hukuza uhusiano wa sekta na biashara unaowezesha uhawilishaji, uchukuaji na utumiaji wa uwezo wa uzalishaji unaosababisha kuongezeka kwa uzalishaji, kukuza ushindani, kuboresha ujuzi, na uzalishaji wa ajira kupitia fursa zinazoongezeka za viwandani na soko.

Kuelekea mabadiliko ya kimuundo na ushiriki wa sekta binafsi

Mabadiliko ya kimuundo yanarejelea mchakato unaoendelea wa (i) kuongeza uzalishaji wa jumla kwa kuhamisha rasilimali muhimu za uzalishaji na kazi kutoka sekta ya chini hadi ya juu ya uzalishaji (mabadiliko ya muundo) na (ii) kuongeza uzalishaji ndani ya sekta kwa uboreshaji wa sekta nzima (kuondoa rasilimali kutoka katika shughuli za uzalishaji mdogo kuelekea mkubwa ndani ya sekta hiyo hiyo). Kuongezeka kwa uzalishaji wa sekta ya kilimo, kuharakishwa kwa ukuaji wa viwanda, na kuimarika kwa ushindani wa kimataifa katika sekta zinazoweza kuuzwa, yote ni malengo ya msingi ya mabadiliko, ambayo yanahusisha sera inayozingatia shabaha za uchumi halisi za hatua kwa hatua. Kadhalika, uhamishaji wa rasilimali kutoka katika shughuli zenye uwezo mdogo wa uzalishaji kwenda kwenye sekta na shughuli zenye uwezo wa juu wa uzalishaji mara nyingi hudhaniwa ni mabadiliko yanayohusisha sekta za uchumi wa nchi zilizozoeleka - kama vile kilimo - na kwenda katika sekta za ‘kisasa’ zenye uwezo wa uzalishaji - kama vile viwanda na ‘huduma za viwango vya hali ya juu’.

Mabadiliko ya kimuundo kihistoria yamekuwa lengo kuu la sera ya maendeleo nchini Tanzania, inayojidhihirisha kwa njia mbalimbali katika kipindi hiki cha maendeleo ya kiteknolojia na utandawazi (usasa) kutoka katika matarajio ya Ujamaa baada ya uhuru hadi kufikia mfumo wa sera ya soko huria wa sasa Kama ilivyoelezwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025. Katika kiini cha ajenda ya mabadiliko, nia imekuwa ni kuhamisha ukuaji wa uwezo wa uzalishaji na kodi zinazohusiana na uchumi kutoka katika mfumo wa kilimo cha kujikimu hadi kufikia uchumi mtambuka na wa kati wa viwanda unaojumuisha kuongezeka kwa mchango wa sekta za viwanda, huduma, na uimara wa mtaji.

Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2025 inaitaka Serikali kusaidia na kuchochea wadau mbalimbali wanaoshiriki katika ukuaji wa uchumi, kwa kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika, pamoja na mambo mengine, kuendeleza miundombinu na huduma. Uwekezaji kama huo unaweza kufikiwa kupitia mifumo ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPPs). Kimsingi, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPPs) unaweza kuwa chanzo mbadala bora cha utafutaji fedha, usimamizi, na matunzo ya miradi ya sekta ya umma. Pia, ubia huu unaiwezesha Serikali kubakia kwenye majukumu yake mengine ya msingi katika kutoa bidhaa na huduma za kiuchumi na kijamii, na hii huongeza ufanisi, uwajibikaji, ubora wa huduma na kufikia kundi kubwa la watu, hivyo kuchochea mabadiliko ya kimuundo ya kiuchumi. Licha ya uwezo wake wa kuleta mabadiliko, Tanzania imechelewa kuweka mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPPs) huku sera ya kwanza ikitungwa 2009, miaka 10 baada ya kuzinduliwa kwa dira yake ya maendeleo ya Taifa. Uchanga wa taasisi za kiubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPPs), kumeleta changamoto nyingi katika kukusanya mtaji binafsi, kujenga uhusiano mzuri kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, na hivyo kuchangia ugumu wa kukabiliana na hali ya kutoaminika kwa mitaji ya sekta binafsi iliyokita mizizi katika kipindi cha Ujamaa nchini.

Uwekezaji katika mabadiliko ya kimuundo umesababisha kukibadilisha kilimo kama sekta ya huduma—hususan biashara— na viwanda na hivyo kuwa mchangiaji mkubwa wa ongezeko la thamani la Pato la Taifa (GDP). Huduma za viwanda na biashara zimekua na kuchangia pakubwa katika upanuzi wa uzalishaji na kutengeneza ajira nchini. Pia, wastani wa uzalishaji wa wafanyakazi katika sekta ya viwanda na huduma nchini umezidi ule wa kilimo kwa uwiano wa saba na mara tatu zaidi. Kwa jumla, kumekuwa na ongezeko la mchango wa ajira zisizotokana na sekta ya kilimo kutoka aslimia 25.4 mwaka 2010 hadi asilimia 34.4 mwaka 2021 na kushuka kidogo kwa mchango wa sekta ya kilimo katika Pato la Taifa kutoka asilimia 27.8 mwaka 2010 hadi asilimia 26.1 mwaka 2021.

Hata hivyo, pamoja na uwekezaji mkubwa, Tanzania haijapiga hatua kubwa katika kufikia mabadiliko ya kimuundo ya kukuza ukuaji jumuishi tangu mwaka 2011, na zaidi katika miaka 40 iliyopita. Kwa upande wa mabadiliko ya kisekta, uchumi wa viwanda umeshuka mapema zaidi, huku mchango wa viwanda katika Pato la Taifa ukishuka kutoka asilimia 11.4 mwaka 1972 hadi asilimia 7.8 mwaka 2021 huku mchango wa sekta za huduma ukipanda (hasa madini). Licha ya uzalishaji mkubwa, sekta ya viwanda nchini bado changa kwa upande wa mchango wake katika Pato la Taifa, vikisalia palepale na mchango wa asilimia nane katika kipindi cha miaka thelathini na moja iliyopita tangu 1990. Aidha, theluthi mbili ya sekta hii inaundwa na viwanda vidogo na asilimia kubwa ni vile visivyo rasmi au watu binafsi katika uzalishaji mdogo, ubunifu mdogo, na sekta ndogo ndogo zenye ukuaji duni, ikiwa ni pamoja na huduma za biashara. Huduma za biashara ni pamoja na zile za rejareja, jumla, na biashara ya vyakula na vinywaji ambayo nchini inawakilisha sehemu kubwa ya sekta isiyo rasmi, ambayo ni asilimia hamsini na tano ya biashara isiyo rasmi. Ingawa sekta hizi za huduma za biashara zina athari chanya kwa ujumla katika uzalishaji wa nguvukazi kwa kuhamisha nguvukazi hizo kutoka katika kilimo nchini, lakini mchango wake katika ongezeko la thamani ni hafifu, na hivyo basi kushusha uwezo wao wa kuweka akiba na wigo wa kupanuka zaidi.