Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabilioni ‘Samia Infrastructure Bond’ kuchochea maendeleo ya barabara nchini

Hatua ya Benki ya CRDB kuzindua Hatifungani ya ‘Samia Infrastructure Bond’ inatarajiwa kuongeza kasi ya mwenendo wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara nchini kote.

Hatifungani hii inayolenga kukusanya Sh 150 bilioni za kusaidia ukarabati na ujenzi wa barabara za mijini na vijijini zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) chini ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ni ya kwanza kutolewa nchini ikiwa ni mahsusi kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Mpango huu unakusudia kuziba pengo la upatikanaji wa fedha kwa ajili ya malipo ya makandarasi wanaojenga barabara hivyo kuharakisha maendeleo ya miundombinu hiyo muhimu kwa usafiri wa abiria na usafirishaji wa huduma na bidhaa.

Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dk Phillip Mpango, akimwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali, amezindua ununuzi wa hatifungani hiyo akifungua njia kwa Watanzania wengine nao kunufaika na fursa muhimu ya kuwekeza kwenye hatifungani hii kwa malengo mawili ikiwamo kunufaika na riba ya asilimia 12 kwa mwaka pamoja na kuwa sehemu ya wazawa wanaoshiriki kujenga miundombinu ya Taifa lao.

“Mimi nanunua hatifungani ya Sh 100 milioni na Mheshimiwa Rais naye amesema ananunua hatifungani ya Sh 200 milioni. Nawasihi Watanzania wenye akiba ya kuanzia shilingi 500,000 kuwekeza katika hatifungani hii,” alisema Mheshimiwa Dk Mpango kwenye uzinduzi huo ulioshuhudia hatifungani ya Sh 37 bilioni ikiuzwa ukumbini.

Fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya hatifungani hii iliyoidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) zitahakikisha upatikanaji wa malipo ya makandarasi kwa wakati hivyo kuharakisha kukamilika kwake kama ilivyopangwa.

Wakandarasi kulipwa kwa wakati Ili kuharakisha maendeleo ya Taifa, Serikali imekuwa ikitekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara katika maeneo tofauti nchini.

Miradi hii hutekelezwa kwa kutegemea bajeti ya Serikali au mchango wa wahisani wa maendeleo. Pale bajeti ya Serikali inapotumika, mara kadhaa kumejitokeza kuchelewa kwa malipo ya mandarasi suala linalolazimu mradi kutokamilika kwa wakati.

Licha ya kuchelewa kukamilika hali inayochelewesha manufaa ya mradi husika kwa wananchi, hali hiyo huacha athari kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya aina hiyo kiasi cha baadhi kulazimika kukopa fedha kutoka kwenye taasisi za fedha na wakishindwa kurejesha kwa wakati kujikuta wakipoteza nyumba au mali nyingine za thamani walizoweka dhamana.

Kwa kuzitambua changamoto hizo zinazowagusa wadau tofauti kwenye ujenzi wa barabara nchini hasa upatikanaji wa fedha kwa wakati, Benki ya CRDB imekuja na suluhisho la kudumu la kuitambulisha Samia Infrastructure Bond inayolenga kukusanya zaidi ya Sh 150 bilioni zitakazotumika kuwakopesha wakandarasi wa barabara ili kukamilisha kazi zao kwa muda uliopangwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela anasema kiasi chote cha fedha kinachotarajiwa kukusanywa kitapelekwa kwa makandarasi ili kuhakikisha ujenzi na ukarabati wa barabara unaendelea bila vikwazo vya kifedha.

“Hatifungani hii itahakikisha wakandarasi wanapata fedha wanazohitaji kwa wakati unaotakiwa hivyo kuondoa ucheleweshaji wa miradi na kuhakikisha inakamilika kwa wakati,” anasema Nsekela.

Vilevile, mkurugenzi huyo anasema Samia Infrastructure Bond ni hatua muhimu ya kuimarisha sera ya Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) nchini. Katika mnyororo wake, anasema mradi hubuniwa na Serikali kisha zabuni kutangazwa kwa sekta binafsi ili kuutekeleza na sasa fedha zitapatikana kutoka sekta binafsi ili kuwalipa watekelezaji huku serikali ikibaki kuwa msimamizi wa mwendelezaji wa miradi hiyo.

“Hatifungani hii inadhihirisha jinsi Serikali na sekta binafsi zinavyoweza kushirikiana kutatua changamoto zilizopo tukianza na hii ya miundombinu. Kwa kuunganisha nguvu za taasisi kama Benki ya CRDB na malengo ya maendeleo ya Serikali, ushirikiano huu utaongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya muhimu,” anasema Nsekela.

Fursa ya uwekezaji Uwekezaji kwenye bidhaa za fedha zinazopatikana katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ni kati ya fursa ambazo wananchi wengi wanahamasishwa kuzichangamkia kwani ni kati ya maeneo yanayotoa kipato cha uhakika wakati mhusika akiendelea na shughuli zake.

Kinachosisitizwa ni kuhakikisha unawekeza kiasi unachoona kitakupa faida uitakayo. Benki ya CRDB ni kati ya taasisi za fedha zilizoorodheshwa sokoni humo na kutoa nafasi kwa maelfu ya Watanzania kumiliki hisa zake tangu mwaka 2009 ambako mpaka hivi leo ni kati ya kampuni ambazo hisa zake zinafanya vizuri.

Licha ya fursa hiyo ya kuwapa Watanzania nafasi ya kumiliki hisa zake, Benki ya CRDB pia inaingiza bidhaa nyingine sokoni hapo ili kuwapa wawekezaji fursa ya kutanua vyanzo vya mapato ikiwamo hatifungani hii ya Samia Infrastructure Bond ambayo kwa mtaji wa walau shilingi 500,000 tu mtu au taasisi anaweza kujiunga kwenye safari hii ya kuijenga Tanzania inayopitika mahali kote, mwaka mzima.

Hatifungani hii itahakikisha makandarasi wanapata fedha za kuwawezesha kukamilisha miradi wanayoitekeleza kwa wakati kwa manufaa ya Watanzania wote jambo ambalo Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Hamad Chande alisema litawawezesha kujikita katika kutengeneza miundombinu bora.

“Samia Infrastructure Bond itawasaidia wakandarasi kuzishinda changamoto wanazokabiliana nazo ikiwamo upungufu wa fedha na kuhakikisha ujenzi wa barabara unakamilika kwa wakati,” anasema Mheshimiwa Chande.

Kuwapo kwa fedha za ujenzi na ukarabati wa barabara hasa katika maeneo ya vijijini ambako miundombinu mingi ni mibovu hali inayokwamisha usafirishaji wa huduma na bidhaa pamoja na usafiri wa abiria, kutaimarisha na kuboresha huduma za usafiri, kukuza biashara, na kuongeza shughuli za uchumi.

Kuwapo kwa fedha hizi pia kutaziwezesha halmashauri kupanga kujenga barabara imara za lami badala ya kiwango cha changarawe.

Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond ni suluhisho la muda mrefu la changamoto ya upatikanaji wa fedha za kufadhili maendeleo ya miundombinu ya barabara nchini.

Mpango huu ni sehemu ya juhudi endelevu za kufadhili miradi ya maendeleo ikiwamo miundombinu muhimu katika sekta tofauti hivyo kuipa Serikali muda wa kutosha kukusanya mapato yanayohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyoidhinishwa.

Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe kwa mfano, ambako mara nyingi hufanywa kutokana na ufinyu wa bajeti, kunaipa Serikali gharama kubwa za matengenezo kutokana na kuharibika mara kwa mara pindi mvua zinaponyesha huku uharibifu uliotokea ukikwamisha shughuli za wananchi.

Lakini, hatifungani hii ya Samia Infrastructure Bond itatoa fedha zitakazowezesha ujenzi wa barabara bora zinazodumu kwa muda mrefu na zinazopitika muda wote hata masika za mvua nyingi.