Madini ya Tanzanite yanavyomnufaisha Bilionea Laizer na jamii

Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Bilionea Saniniu Laizer amejenga ghala kubwa la kuhifadhi gunia 6,000 za mazao.
Bilionea Laizer anasema ghala hilo lililopo kitongoji cha Namelock kijiji cha Naepo kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro, litahifadhi mazao ambayo atayatumia kwa kuwauzia kwa bei elekezi ya Serikali, watu mbalimbali, taasisi na jamii ya hali ya chini.
Anasema amefanya hivyo kwa lengo la kuhakikisha chakula kinapatikana kwa uhakika na kwa wakati huku wakiuziwa kwa bei nafuu elekezi iliyotolewa na Serikali.
Shamba kubwa la kilimo
Bilionea Laizer pia, ameandaa shamba la ekari 170 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji cha mbogamboga kwa ajili ya kuwauzia watu kwa bei nafuu na waweze kujenga afya zao.
“Tumeshachimba visima vitatu ambavyo vipo tayari kwa kuandaa umwagiliaji wa mashamba ya mbogamboga kupitia umwagiliaji huo,” anasema Bilionea Laizer.
Misaada kwa jamii
Bilionea Laizer amekuwa msaada mkubwa kwa jamii inayomzunguka ikiwemo ujenzi wa shule, nyumba za ibada, taasisi mbalimbali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na watu binafsi mmoja mmoja.
Shule ya awali na msingi Saniniu Laizer ya mchepuko wa kiingereza ipo kitongoji cha Namelock kijiji cha Naepo kata ya Naisinyai, imejengwa na Bilionea Laizer kwa gharama ya sh466.8 milioni na kuikabidhi Serikali Januari 2021.
“Nilijenga shule hiyo na kuikabidhi Serikali ambayo ninaishukuru kwani imeboresha zaidi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mradi wa Boost imejenga madarasa mawili mapya na matundu ya vyoo,” anasema Bilionea Laizer.
Hata hivyo ameiomba Serikali iongeze walimu kwenye shule hiyo na pia kukamilisha bweni la kulala wanafunzi naye atajenga bwalo la chakula kama alivyoahidi kwani jiko ameshakamilisha.
Pia, Bilionea Laizer amefanikisha ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Purana mtaa wa Naepo lenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 1,000.
Amechimba visima kwenye kitongoji chake cha Namelock na ndugu na jamaa wa eneo hilo pamoja na mifugo, wanapata maji kwa karibu tofauti na awali kabla ya kuchimba maji hayo.
Bilionea Laizer pia amechimba visima vya maji kwenye vijiji vya Lengasti kata ya Naisinyai na kijiji cha Olchoronyori kata ya Msitu wa Tembo, ila wanatumia gharama kubwa kuvuta maji kwa ukosefu wa nishati ya umeme kwani bado kilomita 21 kufikiwa na umeme.
“Tumechimba maji ila kinachokwamisha ni umeme hivyo kusababisha tununue mafuta ya diseli lita 400 kwa siku ili kuvuta maji ni gharama kubwa hivyo tunaomba Serikali ifikishe umeme ili watu na mifugo wanufaike,” anasema.
Amechangia Sh20 milioni kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi wa CCM Wilaya ya Simanjiro na pia hivi karibuni kampuni yetu tumechangia Sh10 milioni kwenye taasisi ya Amani kwanza iliyopanda mlima wa Kilimanjiro.
“Hivi karibuni wachimbaji tulikutana na Mkuu wetu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga na nikachangia Sh10 milioni kwa ajili ya kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan,” anasema.
Bilionea Laizer kwenye sekta ya uchimbaji ameajiri vijana zaidi ya 400 wanaofanya kazi migodini, hivyo kuchochea ajira na kuwaepusha vijana kukosa kazi na kuzurura mitaani.
Hospitali kwenye migodi ya Tanzanite
Bilionea Laizer ameiomba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwajengea zahanati, kituo cha afya au hospitali ili wachimbaji waweze kupata matibabu na huduma za afya kwenye machimbo ya Tanzanite.
“Mtu anaweza akapata homa ya ghafla au akajeruhiwa mgodini wakati wa usiku inamuwia vigumu kupata matibabu kwani hakuna usaidizi zaidi ya huduma ya kwanza migodini,” anasema Bilionea Laizer.
Anasema kukiwa na huduma za afya ndani ya migodi ya madini ya Tanzanite itakuwa faida kubwa wa wachimbaji kwani wataweza kutibiwa muda wowote hata usiku ndani ya ukuta.
“Geti la kuingia na kutokea haliwezi kufunguliwa kila wakati hasa usiku wa manane hivyo kunaweza kukatokea ajali au mtu akaumwa na akashindwa kutolewa ila kungekuwepo na hospitali ingesaidia,” anasema Bilionea Laizer.
Ampongeza na kumshukuru Rais Samia
Bilionea Laizer anampongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyowekeza miundombinu ya elimu kwa jamii ya wafugaji ambao awali hawakuwa na mwamko wa kusoma ila hivi sasa wanapata elimu. Bilionea Laizer amesema kupitia Rais Samia jamii ya wafugaji wadogo na wakulima wadogo wanapata elimu kwa ukaribu tofauti na awali walipokuwa wanatembea umbali mrefu ili wakasome hali iliyosababisha wengi wao wakatae shule.
“Akili huwa haiji kama zawadi ila Rais Samia ametupa zawadi ya shule hivyo tutapata elimu, kwani kupitia shule watoto wetu watakuwa na akili na kunufaika wao wenyewe na jamii ya wafugaji kwa ujumla,” amesema Bilionea Laizer.
Anasema hivi sasa jamii ya wafugaji ina mwamko mkubwa mno wa kupata elimu kwani tunu kubwa waliyopewa na Rais Samia hivyo watahakikisha jamii ya eneo hilo inapata elimu.
“Mungu ambariki Rais Samia na ampe maisha marefu, azidi kumpa hekima na busara ya kuweza kutuongoza sisi watanzania na nawaomba viongozi wa mkoa wa Manyara na wilaya ya Simanjiro wasimamie ipasavyo fedha za miradi ya maendeleo inayoletwa na Rais wetu,” anasema Bilionea Laizer.