Mama lishe wanabadilisha maisha ya watu, mlo mmoja kwa wakati

Washiriki wa tamasha la maonyesho ya vyakula vya asili maarufu kama Msosi Asili ambao ni mama/baba lishe wa wilaya ya Temeke na Zanzibar wakitekeleza majukumu yao. Picha: Victor Mapile FAO Tanzania.

Na Pauline Kisanga

Melami (34) ni mama mwenye mtoto mmoja anayeishi jijini Dar es Salaam anayeendesha familia yake kupitia biashara ya chakula pem­bezoni mwa barabara ya Sam Nujoma jijini humo.

Alifundishwa na mama yake kupika, lakini haku­wahi kuambiwa juu ya umuhimu wa usalama na usafi wa chakula.

Alitambua umuhimu wa hayo siku ambayo wate­ja wake walipolalamika kuugua matumbo kuto­kana na usalama mdogo unaotokana na uandaaji mbovu wa chakula baada ya kuhudhuria mafunzo yaliyoandaliwa na COUN­SENUTH kwa niaba ya Shirika la Chakula na Kili­mo la Umoja wa Mataifa (FAO) juu ya elimu ya msingi ya lishe na usal­ama na usafi wa chakula kupitia Mradi wa Motisha kwa Baba na Mama Lishe Kuandaa Mlo Kamili na Salama.

“Kupitia mafunzo hayo niliweza kueleza chan­gamoto nazozipatia na nikaomba nifikiriwe pale ninapohitaji msaada wa kuboresha biashara yan­gu,” alisema Melami.

Upimaji wa chakula

Kabla ya mradi, anas­ema alikuwa anaweka ugali au wali mwingi na mboga chache, lakini baa­da ya mafunzo ameweza kuwawekea wateja wake­machaguo mengi. “Badala ya kuwahudumia ugali au wali na maharage, sasa wanaweza kuchagua na aidha kuku, samaki au nyama,” anaeleza.

Uboreshaji wa mazingira ya biashara

Melami amefanya maboresho katika maz­ingira ya biashara yake. Alianza na kioski cha mbao na baadaye alipata hema linaloweza kuzuia jua kutoka kwa kampuni moja binafsi iliyompatia msaada.

Ndoto yake siku moja ni kumiliki mfano wa kiban­da kinachosambazwa kupitia mradi wa pamoja wa FAO, Serikali na Umoja wa Ulaya (EU) wa Agri-Connect kwa mama na baba lishe.

“Kioski cha kuuza chakula cha mitaani kwa baba/mama lishe kinavu­tia kwa sababu kimechor­wa picha za vyakula na pia kuna jumbe zinazoongoza uelewa wa jamii kuhusu lishe bora,” anaeleza.

Balozi wa lishe

Melami tangu hapo ameanza kubadilika kwa kuvaa apron safi, mtan­dio kichwani, viatu vya kutumbukiza, na kuweka kucha safi na fupi. Anatunza kumbukumbu ya matumizi na mauzo na kukokotoa faida baada ya kuondoa gharama za uendeshaji.

Sasa hivi ni balozi wa lishe ambaye anafundisha wateja wake juu ya mlo kamili, usal­ama wa chakula na usafi.

“Sasa hivi sipokei malalamiko ya mara kwa mara ya wateja, wateja wanaongezeka pamoja na mauzo yanazidi kupanda,” anasema Melami.

Mwandishi ni Mshauri Mwandamizi – Utawala wa Kituo cha Ushauri Nasaha Lishe na Afya (COUNSENUTH).