Maoni ya Pamoja ya EU kuhusu usawa wa kijinsia

Kamishna wa Umoja wa Ulaya (EU), Jutta Urpilainen.

Muktasari:

  • Ni muhimu kufanikisha suala hili kwa usahihi
  • Kuupa usawa wa kijinsia kipaumbele

Ni mara chache sana duniani haki za wanawake na wasichana zimepingwa kwa namna ya kutatanisha kama ambavyo zinapingwa nchini Afghanistan.

Umoja wa Ulaya (EU) umeweka wazi kwamba usaidizi wa maendeleo kutoka EU utategemea kuheshimiwa kwa kanuni za haki za binadamu, ikiwemo haki za wanawake na wasichana.

EU itaendelea kusaidia wanawake na wasichana duniani kote, kwa kuzingatia maadili na imani zetu.

Haki za binadamu, uhuru na demokrasia, pamoja na usawa, ni maadili ya msingi yanayoiunda Umoja wa Ulaya. Maadili haya yanaboresha jamii zetu na kuimarisha ustahimilivu.

Usawa wa kijinsia ni muhimu kwa amani, usalama, ustawi wa kiuchumi, na maendeleo endelevu. Ndio maana kushughulikia kukuza na kulinda maendeleo ya usawa wa kijinsia katika ngazi zote ni kipaumbele na lengo la EU.

Mpango Kazi wa Tatu wa Kijinsia wa EU na bajeti mpya ya utekelezaji nje ya EU hutoa ramani ya utekelezaji wa kimataifa kuelekea katika dunia yenye usawa wa kijinsia.

Mwakilishi Mkuu/ Makamu wa Rais wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell.

Tunafanya kazi kwa karibu na washirika katika ngazi ya kimataifa, kikanda, na nchi, pamoja na kushirikiana na mashirika ya kiraia, ili kufikia malengo hayo. Bado tuna safari ndefu; hakuna nafasi ya kuridhika na hali iliyopo.

Katika nchi nyingi, janga la UVIKO-19 limezidisha ukosefu wa usawa wa kijinsia katika maeneo mbalimbali: elimu, mafunzo ya ufundi stadi, afya, ulinzi na usalama, afya na haki za uzazi, na fursa za kiuchumi.

Vilevile, katika sehemu nyingi, kifun-go cha UVIKO-19 kimeletea kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia, haswa ukatili wa majumbani. Wakati huo huo, sehemu kubwa ya mzigo wa kuhudumia umeangukia kwa wanawake na wasichana.

Wafanyakazi katika uchumi usio rasmi na katika kazi zenye ujuzi mdogo (ambao wengi wao ni wanawake), wahamiaji, na wale ambao ni sehemu ya makundi ya wachache, wamekuwa katika hatari zaidi na wanakabiliwa na aina nyingi za ubaguzi zinazoingiliana.

Zaidi ya hayo, kufungwa kwa shule kumewaweka wasichana katika hatari kubwa ya kunyanyaswa kingono, kupata mimba za utotoni, kufanyishwa kazi za utotoni, na kuingizwa katika ndoa za kulazimishwa.

Shirika la Mfuko wa Malala (Malala Fund) linakadiria kuwa katika kipindi hiki wasichana milioni 20 zaidi   kufikia jumla ya wasichana milioni 150 wako katika hatari ya kuacha shule na kutokuwa na matarajio ya kuendelea na elimu. Idadi hii ni sawa na theluthi moja ya idadi ya watu wanaoishi ndani ya EU.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolea hivi karibuni, fedha zilizotumika katika masuala ya kijeshi mwaka 2020 zilizidi gharama za afya za dunia nzima, hata katika mwaka ambao ulitawaliwa na janga la Korona. Ili kupata ahueni endelevu kutokana na janga la UVIKO-19, tunahitaji kuongeza juhudi zetu katika kukuza usawa wa kijinsia.

Huu ndio wakati wa kutenda zaidi

Changamoto hii sasa inahitaji mwitikio wa kimataifa, wakati tunajenga mustakabali wa dunia ambayo tunatamani watoto wetu na wajukuu waishi, baada ya janga.

Dunia yenye usawa zaidi, uanuwai zaidi, na ambapo fursa sawa ni uhalisia. Tunahitaji kukabiliana na sababu za msingi za ukosefu wa usawa wa kijinsia na ubaguzi ili kufikia mabadiliko endelevu.

Umoja wa Ulaya na Nchi zake Wanachama, pamoja na taasisi za kifedha za Ulaya, zimesimama pamoja na wanawake na wasichana duniani kote katika janga hili.

Kama Timu Uropa, tayari tumeshakusanya Euro bilioni 46 kwa ajili ya kusaidia zaidi nchi washirika 130, tukiwa tunazingatia zaidi wanawake na vijana.

Nchini Tanzania, EU inaandaa mpango mpya wa Euro milioni 70 (shilingi bilioni 186) unaoitwa “Kuvunja Dari la Kioo” ili kusaidia wanawake kuishi huru dhidi ya ukatili, kupata huduma sawa za umma, kufurahia uwezeshaji wa kiuchumi, na kushika fursa za uongozi.

Hata hiyo, ili kukabiliana na changamoto zinazoongezeka, tunahitaji kufanya mengi zaidi. Hayo ndio madhumuni ya Mpango Kazi wa Tatu wa Kijinsia. Mpango huu unakuza uongozi na ushiriki madhubuti wa wanawake, wasichana, na vijana katika maisha ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, na kitamaduni, na pia katika masuala yote yanayohusiana na amani na usalama.

Tunashughulika kurudisha maendeleo ya binadamu kwenye mstari

Hivi sasa tunashughulika kufanikisha utekelezaji wa mpango huu kwa usaidizi wa chombo kipya cha Euro 79.5 bilioni cha NDICI-Global Europe ambacho kitasaidia hatua ya utekelezaji wa mipango nje ya EU kwa miaka saba ijayo.Msaada wa elimu, na hasa elimu ya wasichana, utapewa kipaumbele zaidi.

Kama ambavyo tunasaidia elimu katika nyakati za dharura, EU imefanya kazi na nchi washirika katika kipindi kizima cha janga la UVIKO-19 ili kupunguza athari zake kwa watoto, na kuwezesha wanafunzi kurudi shuleni kwa usalama.

Kama Timu Uropa, tayari tunaelekeza zaidi ya nusu ya misaada yote ya kimataifa kwenye elimu. Tutaongeza misaada tunayotoa, ili kukuza usawa wa kijinsia kupitia elimu bora katika ngazi zote.

Ahadi yetu ya pamoja ya Euro bilioni 1.7 kwa Ushirika wa Kimataifa wa Maendeleo ya Elimu mnamo mwezi Julai ili kubadilisha elimu kwa wasichana na wavulana katika nchi na maeneo yafikayo 90 ni sehemu ya mwanzo huu mpya.

Tunazidisha juhudi zetu, kuanzia kukuza elimu na fursa za kiuchumi za wanawake na wasichana hadi kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi. Kufikia mwaka 2025, asilimia 85 ya utekelezaji wote mpya nje ya EU katika sekta zote utachangia masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Ahadi hii sasa inakamilishwa na nchi washirika wetu kwa kuzingatia mashauriano ya karibu na mashirika ya kiraia, wanaharakati wa haki za wanawake, na vijana.

Tunahitaji kurejesha maendeleo ya wanadamu katika mstari na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, bila kumwacha mtu yeyote nyuma.

Ni muhimu kufanikisha suala hili kwa usahihi.

Makala ya Maoni ya Pamoja imeandikwa na Mwakilishi Mkuu na Makamu wa Rais wa Umoja wa Ulaya (EU), Josep Borrell na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa, Jutta Urpilainen