Mchango wa mama lishe katika ongezeko la idadi ya watu mijini

Mwenyekiti wa Umoja wa Mama/Baba Lishe wilaya ya Temeke, Mariami Mtesa (kushoto) akimweleza Ofisa Mwandamizi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) aina mbalimbali ya vyakula vya asili katika tamasha lililofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.

Muktasari:

  • Huduma ya chakula cha mtaani ndiyo tegemeo la tabaka la kati la wafanyaka­zi wengi wanaofanya kazi katikati ya miji na kuishi katika maeneo yaliyo nje ya miji hiyo.

Na Stella Kimambo

Huduma ya chakula cha mtaani ndiyo tegemeo la tabaka la kati la wafanyaka­zi wengi wanaofanya kazi katikati ya miji na kuishi katika maeneo yaliyo nje ya miji hiyo.

Asilimia kubwa ya biashara hii hufanywa kati­ka maeneo yenye msonga­mano mkubwa wa watu, katikati ya jiji, vituo vya usafiri ikiwa ni kinyume na utaratibu wa Serikali za Mitaa.

Serikali zimejaribu kuwa­hamishia mama na baba lishe hao katika masoko yenye miundombinu safi na salama zaidi lakini juhu­di hizo hazizai matunda yanayotarajiwa kutokana na wafanyabiashara hao kurejea kule kule walikozo­ea kwa sababu ya biashara zao kuonekana kwa urahisi na kupata wateja.

Hatua za kuwaondoa kwa shuruti katika maeneo yao na kukamata vifaa vyao vya kazi inayosababisha kusi­mama kwa shughuli zao kwa muda mfupi na baa­daye kurejea, kumewafanya kutokuwa tayari kuboresha vifaa vyao vya kazi jambo ambalo linaathiri usalama wa chakula.

Kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa mama lishe

Hadi sasa, Shirika la Chakula na Kilimo la Umo­ja wa Mataifa (FAO) lim­etengeneza vioski 11 vya mfano ambavyo ni rafiki kwa mazingira ya wauzaji chakula na vyenye uwezo wa kuchukua kati ya watu wanane hadi 12.

Kwa kuwa sasa zaidi ya mama lishe 527 wanaende­sha shughuli zao katika majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, wamepatiwa mafunzo ya upangaji wa chakula, usimamizi wa biashara na kanuni za usal­ama wa chakula na usafi.

Aidha, vifaa vya jikoni (aproni na vyombo vya jik­oni) 1,050 viligawiwa kwa mama lishe katika mikoa hiyo miwili ili kuboresha usalama wa vyakula vya mitaani.

FAO pia inatekeleza ajen­da ya chakula mijini kupi­tia mradi wa Agri-Connect unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) ili kusaidia nchi katika kukabiliana na changamoto za mfumo wa kilimo wa chakula kama vile masuala ya usalama wa chakula na menyu zisizo na uwiano wa lishe.

Mpango huo unatekelez­wa kwa ushirikiano wa wizara zinazohusika na kilimo na afya, pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Dodoma (SIDO) na Serikali za mitaa za mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.

Ili kuwezesha uuzaji na usafirishaji wa bidhaa za kilimo, mifugo, samaki, na vyakula vya mitaani, FAO itabuni na kuzindua pro­gramu tumishi ya simu ya Mfumo wa Upatikanaji na Ufikishaji Chakula (FLAS). Watanzania wataweza kupatiwa mapendekezo ya lishe bora kutokana na Miongozo ya Chakula na Ulaji (FBDGs).

Mwandishi ni Mbobezi wa Usalama wa Chakula na Lishe wa FAO Tan­zania