Mchango wa mazao jamii ya kunde katika mifumo ya kilimo kwa ajili ya chakula

Mazao jamii ya kunde yana historia kubwa ya kuwapatia watu lishe bora kwa miongo sasa. Sambamba na mazao ya nafaka, mazao jamii ya kunde yalikuwa miongoni mwa mazao ya kwanza kulimwa takriban miaka 11,000 iliyopita.

Leo hii, katika baadhi ya tamaduni, mazao jamii ya kunde yanaonekana kuwa chakula cha watu maskini na hubadilishwa mara tu familia hizo zinapopata nafasi ya kula nyama. Jambo hili limeenda mbali zaidi ambapo katika baadhi ya jamii vijana wamekuwa wakielezwa katika malezi yao kuwa kula maharagwe kwa wingi kunasababisha tatizo la uoni hafifu. Kwa hakika, jamii haifahamu ukweli wa mazao haya kwamba yanachangia katika kuimarisha afya, usalama wa chakula, lishe na udhibiti wa uzito.

Virutubisho vilivyomo katika mazao haya vinasaidia matibabu ya watu wenye kisukari, vinapunguza hatari ya magonjwa ya moyo, vinasababisha dosari katika mirija ya mishipa ya fahamu, inadhibiti tatizo la upungufu wa damu (anaemia), vinabeba sifa za udhibiti wa matatizo ya saratani na kuzuia matatizo ya akili.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa, nchini Tanzania, mazao jamii ya kunde ni chanzo cha pili kwa ukubwa cha chakula cha binadamu baada ya nafaka, ambacho mara nyingi huliwa kama mboga na vyakula vikuu vya nafaka. Baadhi ya mazao hayo ni kama vile kunde na maharagwe, mchicha na matembele pia huliwa kama mboga za majani.

FAO inashirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kuongeza uzalishaji na kuhimiza ulaji wa aina ya maharagwe yenye virutubisho (ya Jesca) ambayo yana madini ya chuma na zinki kwa wingi, ili kudhibiti kiwango kikubwa cha upungufu wa damu nchini.

Ili kuongeza uelewa wa faida za mazao jamii ya kunde kupitia mikakati inayohusiana na vyakula, miongoni mwa aina za mazao haya zilizotolewa, maharagwe ya Jesca yamekuwa yakilimwa katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Iringa, Njombe na Songwe.

Kati ya mwaka 2020 hadi sasa, FAO imesaidia wilaya sita za mkoa wa Kigoma na imegawa zaidi ya tani saba za mbegu za maharagwe ya Jesca yenye virutubisho katika vijiji 20 na shule 15. Katika msimu huu wa uzalishaji, FAO ilinunua na kusambaza maharagwe hayo yenye madini mengi katika shule 100 za ukanda wa Kilimo-ikolojia wa Nyanda za Juu Kusini (Iringa Njombe na Songwe).

Wakulima na shule pia walipewa mafunzo ya mbinu bora za kilimo na maonyesho ya upishi. Matokeo ya jumla ya jitihada hizi yalikuwa ni uboreshaji wa usalama wa chakula na lishe na mapato ya kaya.


Imeandikwa na Dk Nyabenyi Tipo ambaye ni Mwakilishi wa FAO Tanzania.