MDH: Tuzo za NBAA na TRA zimetupa hamasa ya kuendelea kufanya vizuri

Mkurugenzi wa Fedha wa MDH, CPA Damasco Peter akipokea tuzo ya uandaaji bora wa hesabu kwa mwaka 2021 iliyotolewa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Mahesabu Tanzania (NBAA). MDH ilishika nafasi ya pili katika kipengele cha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s).

What you need to know:

  • Management and Development for Health (MDH) ni moja ya taasisi inayofuata sheria za kodi pamoja na ubora wa uandaaji wa taarifa za kifedha.

Management and Development for Health (MDH) ni moja ya taasisi inayofuata sheria za kodi pamoja na ubora wa uandaaji wa taarifa za kifedha.

Jambo hili limewawezesha kufanya vizuri katika tuzo za Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Mahes­abu Tanzania (NBAA) kwa mwaka wa pili mfululizo pamoja na kut­waa tuzo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama miongoni mwa walipaji kodi bora wa mwaka 2021/2022.

Mkurugenzi wa Fedha wa MDH, CPA Damasco Peter anasema tuzo hizo zina maana kubwa kwao kama taasisi kwa sababu zimewa­pa hamasa ya kuendelea kufanya vizuri hususani katika idara ya fed­ha na shirika kwa ujumla.

Tuzo hizo wamezipata kutokana ushirikiano mkubwa walioupata kutoka katika idara nyingine nda­ni ya MDH kwa sababu siku zote wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana kama timu.

"Bila ushirikiano wa idara nyingine tusingeweza kupata tuzo hizi kwa sababu tumekuwa tuk­ishirikiana na kuiwakilisha MDH vizuri. Hivyo nashukuru idara, vitengo, uongozi na wafanyakazi wote wa taasisi yetu kwa ushiriki­ano mkubwa walioutoa," anasema CPA Damasco.

Taarifa za fedha lazima zionye­she kwa namna gani taasisi imeb­adilisha maisha ya watu kuanzia wanufaika wa miradi na shughuli za taasisi mpaka waajiriwa na wafanyakazi wengine kwa saba­bu kuwa na taarifa bora za fedha kunatakiwa kuendane na matokeo chanya ya taasisi kwa jamii na wafanyakazi wake.

Serikali ya Jamhuri ya Muunga­no wa Tanzania inatekeleza mika­kati mbalimbali ili kuleta mapin­duzi ya kiuchumi yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi wake na ili kutimiza azma hii, Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika yasiyo ya serikali (NGOs).

Mkurugenzi wa Fedha wa MDH, CPA Damasco Peter (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za walipa kodi bora wa mwaka zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). MDH ilishika nafasi ya pili katika kipengele cha walipa kodi wa kati katika Mkoa wa Kikodi wa Ilala.

"Shirika la MDH ni miongoni mwa wadau muhimu katika sekta ya afya, ambao wamejikita katika kusaidia juhudi za Serikali kwe­nye kuimarisha huduma za afya na kujenga uchumi ili kuleta maisha bora kwa kila mtanzania kupitia kauli mbiu yao ya “Until Everyone is Healthy," anasema CPA Dam­asco.

MDH inafanya kazi kwa kush­irikiana na Serikali katika kutekele­za afua mbalimbali za Afya kupitia ufadhili toka kwa wadau mbalim­bali wa maendeleo wakiwemo seri­kali ya Marekani kupitia PEPFAR (CDC na USAID), Mfuko wa Kima­taifa wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) na wadau wengine.

Afua hizi ni pamoja na huduma za kinga na tiba ya VVU/UKIMWI, kifua kikuu (TB), Malaria, Afya ya Mama na Mtoto na vijana wa rika balehe, magonjwa yasiyoam­bukizwa, uimarishaji wa mifumo ya maabara, takwimu na men­gine.

Katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 MDH imejikita katika kutoa na kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU (WAVIU) katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Geita, Tabora, Pwani, Kigoma, Morogoro, Njombe, Iringa, Ruvuma, Mtwara na Lindi.

Vilevile MDH imechangia katika kuibua wagonjwa wa kifua kikuu (TB) kutoka katika jamii, kubore­sha mifumo ya maabara kwa nchi nzima, mifumo ya takwimu za afya na uboreshaji wa majengo ya vituo vya afya.

MDH pia imekuwa mstari wa mbele kusaidia juhudi za Seri­kali katika kukabiliana na janga la Uviko-19 pamoja na magonjwa mengine ya milipuko.

Miradi yote inayotekelezwa na MDH inafuata vipaumbele vya Serikali vilivyomo kwenye mipan­go mikakati ya sekta ya afya.

Kwa upande wa utafiti, mpaka sasa MDH imesharatibu na kushiri­ki katika tafiti nyingi nchini zikiwa na lengo la kuibua mbinu mbalim­bali za kuboresha afua za afya na kusaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi katika kutoa huduma. Kwa mfano, MDH kwa kushirikiana na Serikali chini ya ufadhili wa CDC imefanya utafiti wa kuangalia usugu wa dawa kwa akina mama wajawazito wanaoishi na VVU.

Katika utafiti huu, ilionekana kuwa asilimia 56 ya wamama ambao hawajafubaza VVU wana usugu wa dawa walizokuwa waki­tumia na wana uhitaji wa kub­adilishiwa dawa na ufuatiliaji wa karibu zaidi wa matumizi sahihi ya dawa hizo.

Taarifa za utafiti huu ziliwezesha watoa huduma za afya kuboresha matibabu na huduma kwa wama­ma hawa, na pia kuboresha sera na mipango ya serikali kuhusu kinga na tiba ya dawa za kufubaza VVU.

Je ni nini mchango wa MDH kati­ka kuchangia maendeleo?

“Tuzo ya TRA imeonyesha ni namna gani, Serikali kupitia TRA imetambua mchango wa shirika la MDH katika ulipaji kodi kwa hiari, usahihi na kwa wakati ili kuchan­gia maendeleo ya nchi na kuunga mkono jitihada za serikali za uku­sanyaji wa mapato. Na pia katika kutekeleza makubaliano ya kim­kataba na wafadhili wetu ambapo tunahitajika kufuata sheria za nchi kikamilifu”, anasema CPA Dam­asco.

Anasema, tuzo ya NBAA ambayo shirika la MDH walishika nafasi ya pili kwa taasisi zinazowasilisha taarifa bora za fedha kwa mwaka 2019/2020 na 2020/2021 mfulu­lizo, imewapa nguvu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi katika kipindi kijacho..

“Kama shirika, tuzo ya NBAA imetusaidia kuongeza imani kwa wafadhili kwa sababu MDH ni shirika linalofadhiliwa na wadau mbalimbali wa maendeleo kama nilivyoainisha hapo juu, wadau wengi wanataka kufanya kazi na mashirika ambayo yana weledi, uwazi, uwajibikaji na yanayofua­ta sheria za nchi na za wafadhi­li katika usimamizi wa fedha na utekelezaji wa miradi”. anasema CPA Damasco.

Akieleza mikakati ya taasisi hiyo kuendelea kufanya vizuri katika tuzo hizo, CPA Damasco anasema cha kwanza wanaanzia pale walipoishia kwa kuhakikisha wanaendelea kuimarisha misingi bora ya kufuata sheria za kodi na kutengeneza taarifa bora za kifed­ha kupitia mifumo mbalimbali ya kiteknolojia.

Vile vile watahakikisha taarifa zinaandaliwa kwa kufuata matak­wa yote ya kihasibu na misingi kama yalivyoainishwa kwenye kanuni zinazotoa muongozo wa taarifa za fedha kwa mashirika yasiyo yakiserikali (The Interna­tional Public Sector Accounting Standards, IPSASs)

“Tutaendelea kuweka mikakati kuhakikisha wafanyakazi wetu hasa kitengo cha uhasibu wana­hudhuria mafunzo mbalimbali yanaondaliwa na NBAA pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha uelewa sahihi wa mahitaji ya uan­daaji wa taarifa za fedha. Lakini pia kuhakikisha wafanyakazi kutoka idara zingine wanajengewa uwezo katika kuandaa taarifa mbalimbali ambazo zinaambatana na taarifa za fedha.

CPA Damasco, anawapongeza TRA na NBAA kwa ubunifu wa tuzo hizi, na kuelezea umuhimu wake kuwa inatoa chachu kwa mashirika mbalimbali kuendelea kuhakikisha wanafuata matakwa ya sheria za nchi kwa hiari pamoja na uandaaji wa taarifa za fedha. Lakini pia sherehe za tuzo hizo imekuwa ni jukwaa muhimu kwa wadau mbalimbali kukutana na kubadilishana mawazo chanya juu ya maendeleo ya nchi yetu pamoja na weledi katika utekelezaji wa majukumu.

"MDH ni taasisi yenye mifumo na uongozi imara ambayo inafuata sheria zote za nchi hivyo wadau ama taasisi yoyote inayotaka kufanya kazi na shirika letu wana­karibishwa sana," alihitimisha CPA Damasco.