Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 40 ya huduma za maji, usafi binafsi na mazingira na maazimio mapya ya WaterAid Tanzania

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akikata keki kuashiria maadhimisho ya miaka 40 ya WaterAid nchini. Wengine ni Naibu Waziri wa Maji, MaryPrisca Mahundi (wa pili kutoka kushoto), Anna Tenga Mzinga, Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania (wa pili kutoka kulia), Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shaibu Kaduara (kulia) na Ofisa wa Serikali (kushoto).

Ni miaka 40 ya kufanya kazi kwa bidii na kujitoa kwa taasisi ya WaterAid na inawakilisha maazimio mapya ya kuboresha huduma za maji, usafi binafsi na mazingira kuanzia ngazi za kitaifa hadi za kata/vijiji ili kufikia lengo la pamoja la kuwa maji safi, vyoo vyenye staha na usafi binafsi na mazingira kwa kila mmoja, katika kila eneo.

Ukweli mchungu ni kwamba zaidi ya nusu ya vituo vyote vya afya vya Tanzania havina huduma ya maji ya bomba na ni asilimia 30 pekee ndiyo ina uhakika wa huduma ya usafi wa mazingira. Upatikanaji wa huduma ya maji ni asilimia 88 kwa wakazi wa mijini na asilimia 77 kwa wale wanaoishi vijijini. Tanzania ni nchi yenye watu takriban milioni 62, idadi kubwa wakiishi vijijini. Upatikanaji wa huduma ya maji unakwamishwa na utendaji kazi hafifu wa maeneo ya kuchotea maji, huku asilimia 34 ya miundombinu hiyoikiwa hayafanyi kazi. Upatikanaji wa huduma ya vyoo bora katika ngazi ya kaya ni asilimia 66.

 Kwa wasichana, upatikanaji wa miundombinu ya huduma za maji, usafi binafsi na mazingira ni jambo muhimu lenye mchango katika mahudhurio yao shuleni, hususan wakati wa hedhi na ni moja ya sababu za wasichana wengi kuacha shule. Asilimia 34 ya wasichana wanakosa vipindi shuleni wakiwa katika hedhi kwa kukosa vyumba vya kubadilishia taulo zao na asilimia 26 walilalamikia ukosefu wa vyoo visafi na vyenye staha.

 Tangu mwaka 1983, taasisi hii imekuwa mhimili na msaada wa kutumainiwa katika upatikanaji wa huduma za maji, usafi binafsi na mazingira kote nchini, ikifanya kazi kwa karibu na Serikali, azaki na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa.

Ikisimamia katika jukumu lake la msingi la kusaidia upatikanaji wa huduma za maji, usafi binafsi na mazingira nchini ililolitekeleza huko nyuma hadi kufikia mwaka 2016 na baadaye kubadili mwelekeo wake huku msisitizo mpya ukiwekwa katika kujenga uwezo wa kitaasisi, ushawishi kama mwezeshaji na kichocheo cha kuleta pamoja ubia wa kisekta ili kufikia malengo ya huduma hizo za msingi.

Uboreshaji wa upatikanaji wa huduma za maji, usafi binafsina mazingira ambayo ni dhamira ya muda mrefu ya WaterAid nchini inawiana na mikakati ya kitaifa ya kuwa na huduma hizo katika namna jumuishi na endelevu katika maeneo lengwa kuchagiza mabadiliko makubwa na salama na kuzipa kipaumbele huduma hizo katika sekta ya afya ili kuboresha afya ya umma na kuchangia katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (UN) - hususan lengo namba 6 (la huduma za maji safi na usafi wa mazingira).


Mafanikio

Sherehe hizo za miaka 40 ya WaterAid zinanakshiwa na kuboreshwa kwa upatikanaji wa mifumo nafuu ya usimamizi wa majitaka kwa maeneo ya mijini yasiyopangwa, kuboreshwa kwa upatikanaji wa maji salama kupitia uvumbuzi wa teknolojia na mifumo bora ya usimamizi na huduma na mifumo sahihi ya huduma za maji, usafi binafsi na mazingira katika vituo vya afya ili kuwezesha utolewaji wa huduma bora za afya kwa kuzingatia utu. WaterAid pia ilichangia kuboreshwa kwa usimamizi wa wazi wa skimu za usambazaji maji ambazo zilihakikisha huduma hiyo inapatikana kwa saa 24/7.

“Ningependa dunia nzima ifahamu kuwa kituo chetu sasa kiko katika hali nzuri kwa sababu ya miundombinu ya maji. Tunakaribisha kila mtu kuja kujifunza kuhusu ubora wa kituo chetu. Upatikanaji wa maji, hivi sasa unatuweka salama kwa dhidi ya magonjwa na kuilinda jamii. Ni furaha yetu kutoa huduma hii kwa jamii. Hebu fikiria mtu anayetakiwa kuwahudumia wagonjwa anapata maradhi kwa kukosa maji, hivi nani atawahudumia hao wagonjwa? – Everline Okello, muuguzi anasimulia.

Everline Okello, ni nesi ambaye hivi sasa anatumia vifaa vya kisasa vya kunawia mikono katika kituo chake cha afya huko mkoani Geita.

 Uhusiano wa WaterAid wa karibu na jamii za wenyeji ulisaidia upatikanaji wa huduma bora za maji, usafi binafsi na mazingira katika maeneo ya shule na baadaye kuanzisha vilabu vya WASH katika shule hizo lengwa, ili kupunguza kero za upatikanaji wa huduma hizo zinazozikabili shule nyingi nchini.

“Tulikuwa tukienda kuchota maji umbali wa kilomita mbili kutoka hapa hivyo muda ambao tulitakiwa tuwe darasani tuliupoteza kutafuta maji. Sasa mradi huu wa maji umefika, tumebaki salama na tunachota maji hapa hapa shuleni bila shida yoyote,” msichana wa shule mojawapo anasimulia unafuu wa upatikanaji wa maji alionao sasa tofauti na siku za nyuma.

Kwa upande mwingine, taasisi imeshuhudia kampeni zake za uhamasishaji usafi wa mikono zikifanikiwa kwa kuwafikia watu wengi kupitia jumbe mbalimbali za usafi, ikifuatiwa na usambazaji wa vifaa vingi vya kunawia mikono katika maeneo ya umma ili kuboresha usafi wa mikono pamoja na kuunga mkono mwongozo wa kitaifa wa unawaji mikono.

Ikivuka zaidi ya jukumu lake mama, WaterAid imepiga hatua kadhaa mbele kwa kusaidia baadhi ya biashara zinazohusiana na huduma za maji, usafi binafsi na mazingira kujitangaza kibiashara na kuingiza kipato. Taasisi hii ilisaidia kukuza na kutafutia masoko ya baadhi ya bidhaa zinazohusiana na huduma hizo zinazozalishwa nchini kwa ushirikiano na taasisi ndogo za fedha na wajasiriamali wadogo.

"Kazi yangu ya kuzibua vyoo hapo nyuma ilikuwa hatarishi. Mbaya zaidi inapofikia msimu wa mvua ndiyo wakati ambao mahitaji yake yanaongezeka, lakini kazi ya kuzibua vyoo ni hatari mno. Nakumbuka matukio ya ajali kazini kama vile kuporomoka kwa mashimo ya kuchepushia vinyesi/uchafu wakati marafiki zangu wakiwaa ndani na marafiki zangu kuteleza na kutumbukia kwenye shimo la choo. Sasa hivi nimekuwa nikifanya kazi na UMAWA na tunafanya kazi zetu katika mazingira salama na safi, na ninapata mshahara wa kawaida. Ninamshukuru Mungu kwa mradi huu,” mzibua vyoo mmoja anakumbuka nyakati ngumu za kazi alizokabiliana nazo.

 Matunda ya jitihada hizi zote zinazofanywa na WaterAid ni kwamba mpaka sasa watu milioni 8 wamefikiwa na huduma za maji safi, usafi mwili na mazingira.

“Kama ilivyo kwa wanawake wengi, nilitumia muda mwingi kutafuta maji, lakini sasa, kama mwokaji wa mikate, nina imani kubwa na maji ninayotumia katika biashara yangu ya kuoka mikate,” anasema mnufaika ambaye sasa anafurahia upatikanaji wa maji ya bomba karibu na makazi yake.


Mpango Mkakati wa WaterAid wa 2023-2028 nchini

Kupitia mkakati huu mpya wa miaka mitano, WaterAid, ikiendelea pale ilipoishia katika malengo na maazimio yake ya awali ya kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa huduma za maji, usafi binafsi na mazingira ikichanganya na mikakati mipya inayoangazia kuwa na huduma hizo katiika namna jumuishi, endelevu na safi katika maeneo lengwa na kuweka kuzipa kipaumbele huduma hizo katika sekta ya afya ili kuboresha afya ya umma. Iwapo mkakati huo utafikia malengo, yatakuwa ni mafanikio makubwa kwa huduma hizo nchini ambazo hutengewa bajeti ndogo ya wizara na fedha za wadau wa maendeleo.

 Katika hatua nyingine, taasisi hiyo imeona umuhimu wa kujumuisha makundi yasiyopewa kipaumbele, hususan wanawake na watoto ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi za upatikanaji wa huduma za maji, usafi binafsi na mazingira, katika majukumu hayo mapya ili kuruhusu sauti za wale wasio na kipaza kusikilizwa katika ngazi zote za maamuzi.

Achilia mbali hayo, pia taasisi hiyo inayo dhima ya kuwa wabunifu na kutumia teknolojia za kisasa zitakazorahisisha upatikanaji wa huduma hizo katika namna endelevu. Kwa kuzingatia hili, tutaweza kuwa na kiwango kinachohitajika cha ubora wa maji na usalama kwa kuzingatia kwamba ubunifu na teknolojia zinatumiwa ipasavyo.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akizindua Mpango Mkakati wa WaterAid wa Miaka Mitano (2023-2028). Wengine ni Naibu Waziri wa Maji, MaryPrisca Mahundi (kushoto) na Anna Tenga Mzinga, Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania (kulia).

Mkakati huu hauwezi kufanikiwa bila ushirikiano na wadau wa maendeleo, Serikali, watoa huduma, azaki, sekta binafsi, mtu mmoja mmoja na taasisi za fedha. WaterAid imejidhatiti kuvuka vikwazo na kuzifanya huduma za maji safi, usafi binafsi na mazingira kama chachu ya kufikia maendeleo endelevu nchini katika siku zijazo.


Uzinduzi wa Mpango Mkakati wa WaterAid na maadhimisho ya miaka 40

Maadhimisho ya miaka 40 yalikwenda sambamba na uzinduzi rasmi wa Mpango Mkakati wa WaterAid wa Miaka Mitano nchini (2023-2028) uliofanywa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa, kama mgeni rasmi ambaye kabla ya kuhudhuria hafla hiyo, alitembelea baadhi ya mabanda ya maonyesho ya miradi ya mifano, ikiwamo Mtambo wa Kutibu Maji na Mifumo ya Usimamizi wa Majitaka.

Akihutubia katika hafla hiyo huku akirejea Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2023 (kuhusu Taarifa ya Uchumi wa Tanzania 2023), Waziri Mkuu alisema kuwa Tanzania inapoteza takribani Sh5.6 trilioni kila mwaka kutokana na upatikanaji duni wa huduma za maji, usafi binafsi na mazingira, kiwango cha juu ambacho ni sawa na asilimia 3.2 ya Pato la Taifa.

Alisema kuwa Serikali inafuatilia utekelezaji wa Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji, Usafi binafsi na Mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya, ili kuhakikisha kuwa vituo vyote vya huduma za afya nchini vimeunganishwa kwenye mifumo ya maji safi na salama, vina vyoo bora, vyenye vifaa vya kunawia mikono, na vyumba vya kutokomeza taka.

 “Napenda kuwafahamisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imejipanga kuratibu na kusimamia mpango wa Afya Moja katika ngazi ya Taifa, Kitongoji, Wilaya, Kata na Vijiji, huku moja ya vipaumbele ikiwa ni kukabiliana na hali ya vijidudu vya magonjwa kuhimili dawa. Kwa msingi huo, ofisi yangu itashirikiana na Wizara ya Afya kubaini jinsi ya kujumuisha huduma hizo katika kutekeleza Mpango wa Afya Moja ili kupata matokeo bora,” alisema Waziri Majaliwa.

 Hata hivyo, aliitaka Wizara ya Maji kufanya harambee na wadau ili kuandaa na kutekeleza miongozo ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuimarisha uwekezaji katika sekta hiyo.

“Nawashukuru wadau wote wa maendeleo kwa kutambua umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali nchini, nawahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nanyi sambamba na kuzingatia mikataba, miongozo na taratibu zote ili kuhakikisha miradi mingi zaidi mijini na vijijini inatekelezwa kwa maslahi ya Watanzania,” Waziri Mkuu alipongeza na kumalizia.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la WaterAid nchini, Anna Mzinga alimshukuru Waziri Mkuu kwa uwepo wake kwenye hafla yao na kutoa ahadi zinazolenga kuleta mabadiliko katika sekta ya huduma za maji na usafi wa mazingira. Alisema kuwa WaterAid imepiga hatua kubwa katika sekta ya maji, usafi binafsi na mazingira.

"Nikiangalia tulikotoka, mafanikioyote yasingewezekana bila watu walioshikilia nyadhifa hii kabla yangu, ningependa kuwashukuru wote kwa kuweka msingi imara ambao umeifanya WaterAid kuwa hapa hadi sasa," alidokeza.

Kuhusu mkakati wao wa miaka mitano, aliahidi kujumuisha masuala ya jinsia na haki za wanawake katika miradi yao, ikilenga kuwaweka wanawake kipaumbele chao katika kila wanachokifanya, kwa kushirikiana na Serikali. Hii ina maana kwamba huduma za maji, usafi binafsi na mazingira zilizoboreshwa zitaongeza muda kwa wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi, uongozi na kufanya maamuzi.Kupitia msaada wa wadau wa maendeleo na washirika, Anna anaamini kuwa mkakati wao wa miaka mitano utakuwa bora zaidi baada ya kufanya vyema kwa ule wa mwaka jana uliosaidia watu milioni 8 (ikiwamo watoto wachanga watoto, watoto wadogo, wasichana na wanawake, wavulana na wanaume) kupata maji safi, vyoo bora na miundombinu ya majitaka. Pia anashukuru kuwa nao upande wake.

Mkurugenzi huyo pia alishukuru uongozi wa WaterAid nchini, Ofisa Mtendaji Mkuu, Tim Wainwright, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki, Olutayo Bankole Bolawole, timu ya IPD na timu yote ya ukanda ya Afrika Mashariki, kwa uongozi wao shupavu na mwongozo wao katika Mpango Mkakati wa WaterAid wa Miaka Mitano nchini.

Tukio hilo lilihitimishwa na mjadala wa nguvu wa jopo la wazungumzaji ambao walijadili kuhusiana njia za utekelezaji wa miradi ya huduma za maji, usafi binafsi na mazingira, hatua ambayo itakidhi mahitaji ya kibaiolojia ya huduma hizo kwa wanawake na wasichana. Wazungumzaji hao ni pamoja na Neema Lugangira Mbunge na Balozi wa WASH, Anyitike Mwakitalima kutoka Wizara ya Afya, Jane Mselle Sembuche kutoka WaterAid Uganda na Johannes Msuya wa Equity Bank.