Mikakati ya Tanzania katika kufikia lengo la ‘Sifuri tatu’

Muktasari:

UKIMWI ni janga la kitaifa na kimataifa ambalo ili kudhibitiwa linahitaji hatua za pamoja katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

UKIMWI ni janga la kitaifa na kimataifa ambalo ili kudhibitiwa linahitaji hatua za pamoja katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Hii ndio sababu Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi ulimwenguni ambazo zimeweka mikakati ya mapambano dhidi ya UKIMWI katika awamu zake zote za uongozi.

Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kutoa sera na miongozo inayosimamia shughuli za utoaji wa huduma mbalimbali za VVU na UKIMWI kama mapambano dhidi ya UKIMWI kwa taasisi, makundi na wadau mbalimbali.

Miongoni mwa hizo ni Sera ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ya mwaka 2001 ambayo pamoja na mambo mengine imetoa mwongozo wa namna ya kupambana na ugonjwa huo kama Taifa.

Sera hiyo imeainisha jinsi ambavyo unyanyapaa unachangia katika ongezeko la kuenea kwa VVU na kutambua kwamba kupunguza unyanyapaa ni kanuni muhimu inayohitaji kushughulikiwa na sekta zote katika ngazi zote.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) limeweka lengo la kufikia “Sifuri tatu” (maambukizi mapya, vifo na unyanyapaa) ifikapo mwaka 2030.

UNAIDS inaamini kwamba kuweza kukabiliana na vitu hivyo na kuhakikisha vinaondoka ndiyo njia pekee na muhimu katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kumaliza kabisa janga hili.

Mwakilishi Mkaazi wa UNAIDS Tanzania, Dk Martin Odiit anasema Tanzania imekuwa mshirika mzuri wa harakati za kufikia lengo la “Sifuri tatu” kwa kutekeleza afua mbalimbali zenye lengo la kuondoa maambukizi mapya, vifo vitokanavyo na VVU pamoja na unyanyapaa kwa waathirika wa VVU. Afua hizo ni pamoja na huduma za kitabibu, mabadiliko ya kitabia na afua za kimuundo.

“Kutokana na juhudi hizo baadhi ya mafanikio yamepatikana katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU Tanzania. Idadi ya maambukizi mapya kwa mwaka imepungua kwa asilimia 50 kutoka watu 110,000 mwaka 2010 hadi 54,000 mwaka 2021,” anasema Dk Odiit.

Anasema katika miaka ya karibuni, Tanzania imeongeza juhudi zake za kuzuia VVU. Kwa hiyo, kiwango cha maambukizi mapya katika miaka minne iliyopita (2017-2021) kimepungua kwa asilimia 38 ambayo ni mara tatu ya kiwango cha miaka saba iliyopita cha asilimia 13.

Dk Odiit anasema maambukizi ya VVU miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya ugonjwa huo yalikadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 8 ikilinganishwa na maambukizi ya watu wazima ya asilimia 4.5. Aidha, kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto kinakadiriwa kuwa asilimia 11 na lengo ni kupunguza hadi chini ya asilimia 5.

Kwa upande wa vifo Dk Odiit anasema idadi ya vifo vinavyotokana na VVU imepungua kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka 64,000 mwaka 2010 hadi 29,000 mwaka 2021.

“Kufikia mwishoni mwa mwaka 2021, asilimia 88 ya watu wanaoishi na VVU walijua hali zao, kati yao asilimia 97 walikuwa kwenye matumizi ya dawa na kati yao asilimia 97 walikuwa wamepata huduma za kufubaza virusi. Kwa hiyo, Tanzania iko mbioni kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya 95-95-95 ifikapo mwaka 2025 na ‘Sifuri tatu’ ifikapo mwaka 2030.”

Kwa upande wa unyanyapaa kwa watu wenye VVU, Dk Odiit anasema bado upo. “Utafiti wa mwisho wa athari za VVU Tanzania (THIS) uligundua kuwa kati ya watu wazima wenye umri wa miaka 15 na zaidi ambao wamewahi kusikia kuhusu VVU, asilimia 25.6 waliripoti vitendo vya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU).” Anasema Dk Odiit.

Anasema kuwa watu wazima katika maeneo ya vijijini (asilimia 30.7) waliripoti vitendo vya unyanyapaa kwa WAVIU ikilinganishwa na wale wa mijini (asilimia 17.3).

“Tofauti katika mitazamo ya unyanyapaa pia hutokea katika viwango tofauti vya elimu. Asilimia 41.7 ya wale wasio na elimu waliripoti unyanyapaa tofauti na asilimia 12.2 kati ya wale walio na elimu ya sekondari ya A-level na asilimia 9.3 kati ya wale walio na elimu ya chuo kikuu,” anaeleza Dk Odiit.

Kauli ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS)

Mkurugenzi wa Utafiti na Ufuatiliaji wa TACAIDS, Dk Jerome Kamwela anasema tume hiyo imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kusaidia utekelezaji wa afua mbalimbali za UKIMWI.

Anasema juhudi hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa Tanzania kuwa katika muelekeo mzuri kuelekea kufanikisha lengo la “Sifuri tatu” ifikapo mwaka 2030.

“Sifuri tatu ni lengo ambalo linaelekeza kusiwe na maambukizi, vifo vitokanavyo na VVU na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na ugonjwa huo,” anasema Dk Kamwela.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka nane iliyobaki kufikia 2030 ambapo ndiyo mwisho wa utekelezaji wa lengo hilo, Tanzania bado tunatakiwa kufanya jitihada kubwa kuhakikisha kwamba tunafika sifuri tatu ijapokuwa kasi bado ni ndogo.

Kwa kuangalia malengo ya 95-95-95 pamoja na “Sifuri tatu” mwelekeo wa Tanzania ni mzuri katika mapambano dhidi ya VVU lakini tunatakiwa kuongeza kasi kwani muda uliobaki ni mchache.

Akizungumzia kuhusu kuhamasisha watu kupima kwa hiari Dk Kamwela anasema wamekuwa wakishirikiana na wadau, asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kama FHI360 kwa kuratibu juhudi zao za utekelezaji wa afua mbalimbali za UKIMWI nchini.

“Tumekuwa tukishirikiana na wadau katika utekelezaji wa afua hizo kupitia utoaji wa elimu kupitia vyombo mbalimbali, matangazo, kampeni na juhudi nyingine zinazolenga mtu mmoja mmoja kwa kila anayekwenda kupata huduma kwenye kituo cha afya pamoja na huduma zinazotolewa katika ngazi ya jamii,” anasema Dk Kamwela.

Anasema kupitia ushiriki wa tume katika afua za UKIMWI, wameweza kufikia makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo yaliyopo kwenye mazingira hatarishi kama vile wafanyabiashara za ngono kupitia taasisi zinazofanya afua zinazogusa makundi hayo.

“Ushirikiano wa TACAIDS na taasisi zinazofanya afua mbalimbali za UKIMWI umesaidia kwa kiasi kikubwa kufikia hapa tulipo kama Taifa katika muktadha wa kupunguza maambukizi mapya, vifo na unyanyapaa,” anasema Dk Kamwela.

Dk Kamwela alihitimisha kwa kueleza kuwa “Kaulimbiu ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu ni “Imarisha usawa” hivyo kila kundi na kila mtu katika jamii lazima ashiriki kikamilifu katika muelekeo wa Tanzania inapopambana dhidi ya UKIMWI. Hakuna mtu wala kundi litakaloachwa nyuma katika mapambano haya.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mradi wa EpiC na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la FHI360 Tanzania, Bernard Ogwang anasema wamekuwa wakitekeleza afua mbalimbali katika ngazi ya jamii kwa kushirikiana na taasisi za Serikali na wadau watekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI ili kuhakikisha wanaboresha maisha ya jamii na kufikia sifuri tatu.

“Kwa kushirikiana na wizara na wadau wetu FHI360 Tanzania tunatekeleza miradi ya VVU chini ya ufadhili wa PEPFAR na USAID. Miradi hiyo ambayo inatekelezwa katika mikoa 11 Tanzania lengo lake ni kuhakikisha wananchi wanapokea huduma za VVU wakiwa katika jamii zao,”

Anasema huduma zinazotolewa kupitia miradi hiyo ni pamoja na; upimaji ambapo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wamekuwa wakienda katika jamii na maeneo mbalimbali kuhamasiaha watu wanapima VVU kwa hiari, na wanaogundulika na maambukizi wanaanza dawa ili kupunguza athari ya maambukizi mapya.

“Miradi mingi tunayotekeleza imekuwa ikilenga makundi yaliyoko kwenye athari zaidi ya kuambukizwa VVU ikiwemo mabinti wa rika balehe kupitia vikundi. Tunatoa huduma upimaji na uzazi wa mpango kupitia wahudumu wa afya wanaokwenda katika maeneo hayo. Pia kuwapa elimu ya mabadiliko ya tabia na kuwawezesha kiuchumi.” anasema Ogwang.

Anasema ili kuhakikisha miradi na afua hizo zinakuwa endelevu wamekuwa wakiwajengea uwezo watumishi wa kada ya afya na Serikali kwa kuwapa mafunzo ili kuhakikisha wanaiendeleza hata mara baada ya kipindi cha utekelezaji kuisha.

“Tumeanza kupanga mikakati ya uendelevu kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi hivyo baadhi ya mambo tuliyofanya ni kuhakikisha miradi yetu haiwi tofauti na mifumo ya wizara, kukuza vipawa na kuwahusisha watendaji wa wizara katika miradi yetu, kuishirikisha jamii katika kila hatu na kutumia wahudumu ambao tayari wako katika vituo vya afya,” anasema Ogwang.

Siku ya UKIMWI duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Disemba moja kwa lengo la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu madhara ya ugonjwa huo na juhudi zinazofanyika katika kudhibiti madhara hayo.