Mikakati ya TFS katika kulinda na kusimamia rasilimali za misitu nchini

Makazi ya watu yaliopo ndani ya msitu wa Sao Hill yakiwa na muonekano wa kupendeza.

Rasilimali za misitu ni eneo mojawapo lenye vivutio vya utalii vinavyotumika kwa ajili ya utalii ikolojia, utafiti, burudani za kutembea, kuendesha baiskeli na mapumziko.

Hifadhi hizi pia ni sehemu muhimu katika kuongeza makusanyo ya maduhuli ya Serikali katika jitihada za kuendeleza utalii kwenye maeneo ya misitu, ambapo mapato yanayotokana na viingilio kwenye hifadhi hizi yamekuwa yakiongezeka kila mwaka.

Kwa mujibu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) misitu ni rasilimali zote zitokanazo na misitu ikijumuisha; mazao ya mbao, mazao yasiyo timbao kama vile matunda, mbegu, na dawa, huduma za kiikolojia kama vile maji, nishati, makazi ya bioanuai na utalii.

Aidha kwa mujibuwa wakala huyo Tanzania kuna aina Misitu ya Miombo, Misitu ya milima (Montane forests), Misitu ya uwanda wa chini (lowland forests), Misitu ya ukanda wa pwani (Coastal forests), Ndarambwe (thickets), Misitu ya Mikoko na Mashamba ya miti (Forest plantations).


Utaratibu wa kuvuna rasili¬mali za misitu nchini

Uvunaji wa misitu unatekelezwa kwa kuzingatia mwongozo wa uvunaji wa misitu wa 2015 na Tangazo la Serikali (GN) na 417.

Aidha, Mwongozo unaelekeza utaratibu wa kuvuna ambapo wavunaji wanalazimika kupitisha maombi yao kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uvunaji ya Wilaya ambapo baadaye maombi hujadiliwa. Wafanyabiashara walioidhinishwa kuvuna husajiliwa na hatimaye kupewa leseni ya uvunaji katika eneo alilloruhusiwa.


Mahitaji ya mazao ya misitu hususani miti nchini

Kufuatia taarifa ya utafiti wa misitu (NAFORMA 2015), ilionekana kuwa uhitaji wa mazao ya misitu nchini ni meta za ujazo milioni 62.3 kwa mwaka na uwezo uliopo ni kuvuna meta za ujazo milioni 42.8 kwa mwaka na hivyo kuwepo kwa upungufu wa meta za ujazo milioni 19.5.


Aina ya misitu ambayo inasi¬mamiwa na kutunzwa na TFS

TFS inasimamia misitu yote inayomilikiwa na Serikali Kuu ambayo ni Hifadhi za misitu ya asili ya taifa, hifadhi za misitu ya mazingira asilia, misitu ya mikoko na mashamba ya miti. Aidha, TFS inasimamia misitu ya mataji wazi ambayo ipo katika milki ya Kamishna wa Ardhi.

Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba ukiwa umetunza maji.

Juhudi za TFS katika kuboresha usimamizi wa rasilimali za misitu nchini

Wakala unatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia mpango mkakati unaoandaliwa kwa kipindi cha miaka mitano ambao hutoa dira ya usimamizi wa misitu ya Serikali Kuu nchini.

Aidha kutokana na Mpango Mkakati wakala huandaa mpango wa kibiashara unaotafsiri utekelezaji wa majukumu yake kwa kila mwaka.

Misitu ya hifadhi nayo huandaliwa mpango wa usimamizi wa misitu wa miaka mitano ambao hutekelezwa kupitia mpango kazi wa mwaka mmoja mmoja. Uwepo wa mipango hii umesaidia kupatikana kwa mafanikio yafuatayo;

Kuongezeka wa mashamba ya miti kutoka 15 hadi 24, kuongeza misitu ya mazingira asilia kutoka 8 hadi 24, na kuongeza hifadhi za nyuki kutoka 6 hadi 21.


Namna TFS inavyokabiliana na changamoto ya kuvamia hifadhi za misitu

Wakala umeendelea kuimarisha usimamizi wa misitu kupitia juhudi mbalimbali ikiwemo; kubadili mfumo wa utekelezaji wa majukumu yake kutoka mfumo wa kiraia kuwa mfumo wa kijeshi, ujenzi wa vituo vya uangalizi wa misitu (Ranger post)

Kuboresha mazingira ya kazi mfano kuimarisha vitendea kazi ie. Magari, pikipiki, boats na mitambo; kujenga nyumba kwa ajili ya ofisi na makazi ya watumishi, kuongeza bajeti ya utekelezaji wa shughuli za uhifadhi na doria, na kuimarisha kitengo cha intelijensia.


Uwekezaji wa TFS katika teknolojia

Wakala umeanzisha mifumo mingi kwa ajili ya kurahisisha shughuli za uhifadhi na huduma kwa wananchi, mifumo hii ni pamoja na ile ya ufuatiliaji wa usafirishaji wa mazao ya misitu (log tracking) na mifumo hii inarahisisha mawasiliano kati ya Wakala na wadau na hatimaye kuboresha mazin¬gira ya biashara ya huduma na mazao ya misitu na nyuki.


Juhudi za TFS kuboresha sekta ndogo ya mazao ya nyuki

Wakala umeongeza malengo katika ufugaji nyuki ambapo wakati wa kuanzishwa kwake ilikuwa ikivuna tani 3 hadi kufikia tani 31 kwa mwaka, wakala umeanzisha mashamba matatu ya ufugaji nyuki ambayo ni Mwambao (Handeni-Kilindi), Kondoa Manyoni na Kipembawe (Chunya)

Kuanzishwa kwa viwanda vya kutengeneza mizinga ya nyuki vilivyopo Kondoa na Sao hill, vilevile, Wakala umeanzisha viwanda vitatu vya kuchakata mazao ya nyuki katika shamba la miti Saohil, Manyoni na Nzega ambavyo husaidia kuongeza thamani ya mazao ya nyuki.

Watumishi TFS wakiwa kwenye gari maalumu la zima moto ambalo ni mali ya wakala. Gari hilo hutumika kukabiliana na majanga ya moto kwenye misitu ya asili na mashamba ya miti.

Fursa zinazopatikana katika soko la bidhaa za nyuki

Kila mwaka TFS hupeleka sampuli 70 za asali katika maabara za kimataifa (Ujerumani) kutoka wilaya zisizopungua 30 ambapo mara zote ubora wake umekuwa ukikidhi viwango vya kimataifa. Kutokana na ubora huu, asali ya Tanzania imeendelea kuvutia watu wengi na hivyo kupata soko kubwa la ndani na la nje ya nchi.


Maadhimisho ya siku ya misitu duniani

Sekta ya Misitu na nyuki nchini ni muhimu kutokana na mchango wake katika ukuaji wa sekta nyingine za uzalishaji kama vile utalii, maji, kilimo, mifugo na nishati pamoja na sekta ya viwanda. Aidha, uhifadhi huo unahitaji rasilimali fedha na watu kwa ajili ya usimamizi endelevu. Kutokana na umuhimu huo, uhifadhi wa rasilimali za misitu ni jukumu la msingi na linapaswa kupata mchango kutoka kwa wadau wote.

TFS imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa rasilimali za misitu nchini zinasimamiwa kikamilifu na imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya uhifadhi wa misitu ikiwemo kuanzisha misitu mipya, kuendeleza misitu ambayo halmashauri za vijiji na wilaya zimeikabidhi kwa TFS ili kuimarisha usimamizi, kuotesha miche isiyopungua milioni 30 kila mwaka na kuipanda maeneo mbalimbali nchini. Vilevile, TFS imetekeleza mikakati mbalimbali ya upandaji miti ikiwemo mkakati wa Dodoma ya Kijani.

Vilevile, TFS imeimarisha vituo vya ukusanyaji wa mbegu bora za miti kwa kuanzisha vyanzo vipya vya mbegu sambamba na kuimarisha maabara ya mbegu za miti ambavyo vinahakikisha upatikanaji endeelevu wa mbegu bora za miti.

Aidha, TFS imekuwa ikirejesha uoto uliopotea kwa kuanzisha mashamba ya miti kwa lengo la kuzalisha malighafi kwa ajili ya matumizi mbalimbali na hivyo kupunguza utegemezi wa malighafi hizo kutoka kwenye misitu ya asili.

TFS inatarajia kufanya shughuli mbalimbali za kuihamasisha jamii ili ishiriki kikamilifu katika kazi za upandaji miti na utunzaji wa misitu nchini.