Miradi ya maji inayofadhiliwa na Ubelgiji mkoani Kigoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kulia) akizindua Mradi wa Maji wa Kakonko-Kiziguzigu wilayani Kakonko, Kigoma. Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Ubelgiji nchini, Fanny Heylen.

Muktasari:

Serikali ya Tanzania na Ubelgiji zinashirikiana kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira mkoani Kigoma.

Serikali ya Tanzania na Ubelgiji zinashirikiana kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira mkoani Kigoma.

Jana, Rais Samia Suluhu Hassan, alizindua skimu ya Kakonko-Kiziguzigu, moja ya miradi ya miundombinu ya usambazaji maji inayofadhiliwa na Ubelgiji mkoani Kigoma.

Serikali hizo mbili zilitia saini makubaliano maalum ya miaka sita ya kutekeleza mradi wa maji endelevu Julai 17, 2017.

Mradi huo uliofadhiliwa na Enabel, shirika la Maendeleo la Ubelgiji, uliandaliwa ili kukarabati miundo iliyopo ya maji na kupanua huduma kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma huku ukikuza uwezo wa jamii ili kuhakikisha kuwa huduma hizo zinasimamiwa kwa njia endelevu.

Fungu la awali la fedha kutoka Ubelgiji lilikuwa Euro milioni nane na baadaye kuongezeka hadi milioni 12, ikilenga kuzinufaisha jamii zilizokusudiwa katika wilaya zote sita za mkoa huo.

Mradi huo utakapokamilika, idadi ya watu wapatao 208,000 kutoka vijiji 22 watapata maji ya kunywa na kuboresha mifumo yao ya usafi ili kuwezesha usimamizi wa huduma ya maji salama katika ngazi ya kaya. Hivi sasa, kazi zinaendelea na ziko katika hatua tofauti.

Miradi mitano mipya inajengwa, mmoja unafanyiwa ukarabati mkubwa huku mingine ikipanuliwa ili kufikia watu wengi zaidi.

Kupitia ufadhili wa Ubelgiji, Enabel inatoa msaada wa kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika ngazi ya mkoa na wilaya ya Kigoma.

RUWASA ndio watekelezaji na washiriki wakuu katika mradi huu. Enabel imeisaidia RUWASA kupata vifaa vya ofisi na ujenzi na kusaidia mahitaji yake ya mafunzo. Kwa sasa, inashirikiana na ofisi ya mkoa wa RUWASA kuanzisha Kituo cha Umahiri Kigoma.

Kituo kitakuwa cha rasilimali za uendeshaji ambacho kinasaidia jamii kusimamia miradi yao ya maji kwa namna endelevu.

Mradi huo pia umewezesha uanzishwaji na usajili wa azaki sita za kusambaza maji (CBWSOs) ambazo zitakuwa na jukumu la kusimamia miradi ya maji itakapoanza kutumika.

Enabel pia inafadhili ujenzi wa maeneo ya ofisi kwa azaki hizo, na inatekeleza mpango wa kukuza uwezo wao. Ili kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinadumishwa kwa ajili ya miradi ya jamii, mradi unasaidia Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Tanganyika katika jukumu lake la kuanzisha na kuimarisha Jumuiya za Watumiaji Maji (WUA).

Inasaidia zaidi Bodi ya Maji ya Bonde hilo kuweka mipaka ya maeneo ya mabonde na kufanya WUAs kufahamika zaidi na kufikika kwa urahisi katika vyanzo vinavyolengwa kupitia ujenzi wa vituo vya WUA.

Mradi huo pia umeanza kuhimiza usafi na usafi wa mazingira kupitia kampeni inayosimamiwa na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania. Enabel inatekeleza ushirikiano wa kiserikali wa Ubelgiji na inafanya kazi na wafadhili wengine wa kitaifa na kimataifa.

Pamoja na washirika wake nchini Ubelgiji na nje ya nchi, Enabel inatoa masuluhisho ya kushughulikia changamoto kubwa za kimataifa ikiwa ni pamoja na, mabadiliko ya tabianchi, ukuaji wa miji, uhamaji wa binadamu, amani, na usalama, kutokuwepo kwa usawa wa kiuchumi na kijamii, na kukuza uraia wa kimataifa.

Ikiwa na wafanyakazi zaidi ya 2,000, Enabel inasimamia takriban miradi 170 katika nchi ishirini, nchini Ubelgiji, Afrika na Mashariki ya Kati.

Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Peter Huyghebaert.

Zifuatazo ni shughuli za maji na usafi wa mazingira zinazoungwa mkono na serikali ya Ubelgiji kupitia Enabel mkoani Kigoma.

Ujenzi wa Skimu ya Maji ya Kakonko-Kiziguzigu Wilayani Kakonko

Kupitia ufadhili wa pamoja kutoka kwa Serikali za Tanzania na Ubelgiji, skimu mpya ya maji imejengwa huko Kakonko kwa thamani ya euro milioni 1.87.

Skimu hiyo itaanza kufanya kazi muda si mrefu.Skimu ya Kakonko ni mradi wa maji ambao umefikiwa baada ya utafutaji wa muda mrefu wa chanzo cha maji cha uhakika katika Mji wa Kakonko na jamii zinazozunguka.

Maendeleo ya maji katika wilaya hiyo yamekuwa magumu kufikiwa kutokana na vyanzo vya maji kutotosheleza. Mto Mgembezi, uliopo takriban kilomita 21 kutoka mji wa Kakonko, ulikuwa chanzo cha maji pekee ambacho kilistahili kuendelezwa.

Kwa kuzingatia umbali wa eneo, kuandaa skimu hiyo kutoka katika chanzo hiki kwa ajili ya Kakonko na maeneo ya karibu mara zote ilionekana kuwa ni mradi wenye gharama kubwa.

Agosti 2020, Serikali ya Ubelgiji, ilitoa fedha za ziada kwa Enabel ili kuongeza bajeti ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Kigoma (WASKIRP) ili kuhakikisha kuwa maeneo kama Kakonko yana huduma ya maji ambayo inakidhi mahitaji ya wakazi wake wanaoongezeka kwa kasi.

“Ilikuwa vigumu kutambua vyanzo vya kuaminika vya kuendeleza. Baada ya tafiti kadhaa zilizoungwa mkono na Enabel, hatimaye tulibaini maeneo mawili ambayo Serikali ya Tanzania kupitia RUWASA, ilichimba visima hivyo viwili, ambapo hivi sasa ndiyo chanzo cha skimu hii”, anasema Mhandisi Mathias Mwenda, Meneja wa RUWASA Mkoa.

Skimu hiyo ina njia kuu ya kilomita 5.1 kutoka Kasuga na laini nyingine ya kilomita 9.1 kutoka Nyakayenzi ambapo visima viwili vilichimbwa kama vyanzo vya skimu hii.Matanki mawili ya kuhifadhia maji yenye mita za ujazo 500 kila moja, yamekamilika, yako karibu na ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kakonko.

Tanki moja linahudumia Mji wa Kakonko na lingine linahudumia Kata ya Kiziguzigu. Jumla ya kilomita 65.1 zime-jengwa pamoja na vituo vya usambazaji Kiziguzigu.

Ujenzi unaonedelea wa Mradi wa Usambazaji Maji wa Kazuramimba.

Skimu ya Maji ya Kakonko-Kiziguzigu wilayani Kakonko itahudumia wakazi 51,280 kutoka Nyakayenzi, Kasuga, Mji wa Kakonko na vijiji vitatu vya Kata ya Kiziguzigu. Gharama ya jumla ya skimu hiyo ni Euro milioni 1.87 na imejengwa kupitia mapato ya ndani.

Ukarabati na upanuzi wa mradi wa skimu ya Mkongoro

Kupitia mkataba wa kazi uliokabidhiwa na Kampuni ya Serengeti Limited, Kampuni ya Enabel kwa kushirikiana na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) inakarabati miundombinu ya usambazaji maji iliyopo na kuipanua ili kutoa huduma ya maji ya bomba katika vijiji saba vya wilaya ya Kigoma vijijini.

Ukubwa wa kazi za ukarabati kwenye skimu hii ya maji haukukadiriwa, hususan kwenye matanki ya kuhifadhia na mtandao wa usambazaji. Baadhi ya matanki yalihi-taji kubomolewa na kujengwa mapya. Sehemu nyingi za maeneo ya usambazaji zilikuwa na mashimo ambayo hayajatambuliwa yaliyolazimu uchimbaji na uwekaji wa mabomba mapya.

Muundo mpya kabisa wa uingizaji maji kwenye Mto Nyete umejengwa, mita 600 juu ya mto na mbali na eneo la kuvukia. Mradi pia unajenga miundo mipya ya kutibu maji inayojumuisha sehemu mbili za uchuchaji maji na tanki la kuwekea maji ili yasafishwe ipasavyo kabla ya kusambazwa kwa matumizi ya binadamu.

Skimu hiyo, ambayo ni kubwa zaidi katika eneo la huduma na idadi ya watu katika Wilaya ya Kigoma vijijini, haikuwa na kituo cha matibabu ya maji hapo awali. Vituo 134 vya usambazaji/maji vimejengwa kwa kutoa huduma kwa watu binafsi katika vijiji saba vyenye jumla ya watu 53,500.

Matenki matano ya kuhifadhia maji yanakarabatiwa huku moja likibomolewa na lingine likijengwa badala yake kulinda mradi huo kutokutengeneza eneo kubwa, mzigo na njia kadhaa katika mto huo.

Maendeleo ya jumla ya kazi katika mradi huu ni asilimia 94. Inakadiriwa kuwa kazi zilizosalia zitahitaji wiki nane tu kukamilika. Hali ya miundo tofauti ni kama ifuatavyo: ujenzi wa njia mpya za maji umefikia asilimia 80; mashine za kutibu maji asilimia 80; tenki la kuhifadhia maji asilimia 50; uwekaji njia za usambazaji maji za urefu wa kilomita 18.6 na ile za kilomita 22.7 asilimia 98 huku ukarabati na ujenzi wa vituo vya maji asilimia 96. Ukarabati wa matenki asilimia 82, hadi kukamilika kwa mradi huo, Enabel itatumia jumla ya Euro milioni 1.12.

Mradi wa Kusukuma Maji wa Mwayaya

Chini ya programu inayotekelezwa baina ya Tanzania na Ubelgiji, skimu mpya ya usambazaji maji katika kijiji cha Mwayaya wilayani Buhigwe, imejengwa. Jamii sasa zinapata maji salama ya kunywa, kutokana na pro-gramu hiyo ya pamoja. Awali mpango wa kusukuma maji wa Mwayaya ulipangwa kufanyiwa ukarabati.

Baada ya timu ya uchunguzi kufanya kazi yake, wasimamizi wa mradi walibaini kuwa programu usanifu wake ulishapitwa na wakati na chanzo cha awali kilichokuwa kikitegemewa hakiwezi kukidhi mahitaji ya sasa ya maji. Kupitia Enabel, Serikali ya Ubelgiji ilifadhili masomo ya usanifu ambayo yalifanywa na kampuni ya Howard Consulting Limited na utoaji zabuni wa kazi hizo ulihitimishwa Oktoba 2020.

Kandarasi hiyo ilikabidhiwa Kampuni ya Gopa Contractors Limited iliyoanza kazi Novemba 2020, na UWP Consulting Limited kama wahandisi wa mradi huo. Skimu hiyo imebuniwa kuhudumia idadi ya watu 19,000.

Kazi za kimkataba huu zinahusisha ujenzi wa miundo ya upitishaji maji na ile inayokinga katika mkondo wa Kivuruga, vifaa vya kutibu maji; bomba la usafirishaji maji la kilomita 3,250; ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji la mita za ujazo 400; ujenzi wa mtandao wa usambazaji maji wa kilo-mita 23,166 na vituo 31 vya usambazaji maji.

Utekelezaji wa kazi hizi ulikabiliwa na changamoto za kiutawala lakini baada ya kutatuliwa, ujenzi wa skimu hiyo ulikamilika Aprili 2022. Gharama ya jumla ya mradi huo ni Euro 965,617.

Mbali na skimu hiyo, Enabel imefadhili ujenzi wa jengo la ofisi kwa Azaki ya Ugavi wa Maji (CBWSO) ambayo sasa inasimamia skimu hiyo. Pia inasaidia uimarishaji wa uwezo wa Azaki ya Watumiaji Maji (WUA) huko Mwayaya ili kuhakikisha kuwa eneo dogo la vyanzo vya maji linalindwa.

Shughuli nyingine za mradi wa Mwayaya ni pamoja na ujenzi wa jengo la ofisi ya WUA na kusaidia Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Tanganyika katika kuweka mipaka ya eneo dogo la chanzo cha maji kwa ajili ya skimu hiyo.

Mradi wa Ujenzi wa Huduma ya Maji Kazuramimba

Mradi wa maji wa mkoa wa Kigoma pia unajenga skimu ya kusambaza maji katika eneo la Kazuramimba wilayani Uvinza. Kama ilivyo kwa skimu nyingine ambazo zililengwa kutekelezwa katika mkoa huo, skimu hii ilipangwa kufanyiwa ukarabati.

Hata hivyo, hali ya miundombinu ililazimu mabadiliko katika mipango ya awali. Pamoja na skimu hiyo kutegemea chanzo cha maji kilichokauka, mradi ulianza uchunguzi wa maji chini ya ardhi huko Kazuramimba ambapo maeneo mawili yalitambuliwa na kuchimbwa visima vya uzalishaji.

SHER Group, kampuni ya mipango na usimamizi wa wahandisi kutoka Ubelgiji ilifanya tafiti zilizosababisha mchakato wa kutoa zabuni kuanza Septemba 2020 ambapo Nangai Engineering and Contractors Limited skimu hiyo chini ya usimamizi wa UWP Consulting Limited.

Muonekano wa Mradi wa Kusukuma Maji wa Mwayaya.

Kutokana na sababu za kiutawala na athari za wadau wengine katika upelekaji wa nyenzo za matenki ya kuhifadhi maji, mradi umechelewa kumalizika.

Hata hivyo, kwa sasa skimu imekamilisha uwekaji wa mabomba ya njia mbili za kusambaza maji kutoka katika vituo vya kusukuma maji vya Laba na Rubona vilivyo umbali wa kilomita 1.8 kila kimoja kutoka kwenye tanki la kuhi-fadhia maji. Pia imekamilisha ufungaji wa njia za usambazaji maji zenye urefu wa mita 30,345 na ujenzi wa vituo 35 vya usambazaji.

Uwekaji wa tenki la kuhifadhia maji lenye urefu wa mita za ujazo 480 lililotengenezwa na GRP, unaendelea. Kazi zote zinatarajiwa kumalizika kufikia katikati ya Novemba 2022. Mradi utakapokamilika, utagharimu takriban Euro 889,000 na utahudumia watu zaidi ya 40,000 tu.

Mradi wa Skimu ya Maji Kifura

Huu ni mradi mwingine uliopo mkoani Kigoma ambao unafadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji kupitia Enabel. Skimu ya usambazaji maji Kifura ipo katika Wilaya ya Kibondo na ni mradi wa uendelezaji wa maji juu ya ardhi. Chanzo chake ni Mto Mkuti, na ni mpya, kinyume na mipango ya awali katika eneo la kiufundi na kifedha.

Mpango huu ulibuniwa awali na SHER Group lakini baadaye ukapatiwa ithibati na Howard Consulting Limited. Mkataba wa kazi ulitolewa ushirika wa kampuni za Nangai Engineering na Msukwa Contractors na Norplan Limited kama wahandisi wake wa mradi.

Kazi kwenye skimu hii zilianza Agosti 2, 2021 na zilipaswa kukamilika Februari. Hata hivyo, kutokana na uwepo wa maji kupita kiasi katika ardhi oevu ambayo Mto Mkuti unapita, na kutokana na baadhi ya changamoto za kiutawala, ukamilishaji wa kazi hizo kwa wakati haukufanikiwa.

Mradi wa Ujenzi wa Huduma ya Maji Kidyama

Enabel inafadhili ujenzi wa skimu ya kusambaza maji katika eneo la Kidyama wilayani Kasulu. Ukiwa na jumla ya njia 17,251 za usafirishaji na mita 32,065 za mfumo wa usambazaji, skimu hii itahu-dumia sehemu ya eneo la mjini pamoja na pembezoni mwa mji wa Kasulu.

Ujenzi umeanza hivi punde chini ya kandarasi iliyokabidhiwa Gopa Contractors Limited kwa gharama ya Euro milioni 1.49. Inatarajiwa kuwa ujenzi wa skimu hii mpya ya usambazaji maji itakamilika Machi 2023, na itahudumia wakazi 23,000 huko Kasulu.

Upanuzi wa Skimu ya Maji ya Nyansha na Nyantale

Serikali ya Ubelgiji kupitia Enabel inafadhili upanuzi wa huduma ya maji katika kijiji cha Mdyanda wilayani Kasulu kupitia mapato ya ndani. Mradi wa Mdyanda ni wa maende-leo ya maji chini ya ardhi.

Wizara ya Maji kupitia RUWASA imechimba kisima cha kuzalisha maji ili kiwe chanzo cha ziada cha mfumo wa usambazaji maji uliopo. Maji yaliyopo hayatoshelezi jamii za Nyansha na Nyantale, zaidi ya wananchi wa Mdyanda waliopo pembezoni mwa vijiji hivi viwili.

Mtandao wa sasa wa usambazaji maji una urefu wa mita 22,366 na unahusisha kijiji cha Mdwanda. Enabel imejenga tanki la kuhifadhi maji la mita za ujazo 500 na eneo la na inatarajia kujenga njia ya kusambaza maji ya mita 840 na kuiunganisha kwenye mtandao uliopo.

Wafadhili wa mradi wanena

Balozi wa Ubelgiji nchini, Peter Huyghebaert anasema moja ya fahari yao kubwa ni kuona sasa mkoa wa wilaya za mkoa wa Kigoma na maeneo mengine yanapata huduma ya maji ya kunywa safi na salama ya uhakika.

Akizungumzia kuhusu kwanini walichagua Mkoa Kigoma katika utekelezaji wa mradi huo, anasema “Tuliuchagua Mkoa wa Kigoma kwa sababu ya kuwa na ongezeko la idadi ya watu, lakini pili ni kutokana na mkoa huo kuwa kipaumbele cha Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa sera zake hususan katika uboreshaji wa huduma za kijamii, hivyo imekuwa jambo zuri na sisi kuiweka katika mipango yetu,” anaeleza Balozi Huyghebaert.

Balozi huyo anasema kuka-milika kwa mradi huu kutasaidia kukuza uchumi na kufungua fursa mbalimbali za kibiashara kwa Wanakigoma.Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Enabel, Koen Goekint anasema kuwa kwa ujumla wake utekelezaji wa mradi umekuwa rahisi kwa kuwa wamepata ushirikiano mkubwa kutoka katika Ofisi ya Mkoa wa Kigoma, RUWASA na azaki mbalimbali zilizopo mkoani humo.

“Mradi wa WASKIRPS uta-punguza mzigo kwa akina mama ambao wangetakiwa kutembea kilomita zaidi ya tatu kufuata maji na badala yake wataweza kupata muda maji hayo kwa urahisi na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi,” anaeleza Goekint.

Goekint anasema skimu saba za maji zilizopo katika utekelezaji zitapunguza chan-gamoto ya maji kwa mkoa huo licha ya ukweli kwamba bado kuna maeneo mengi yenye changamoto ya maji safi na salama.Pia anaeleza kuwa mwakani Machi wanatarajia kusaini makubaliano na Serikali ya Tanzania kuanza kutekeleza mradi mpya ukaokuwa ukigusa sekta za elimu jinsia, ukuzaji ujuzi, mabadiliko ya tabian-chi nk.